Yoshie akikabidhiwa i Kiibo na wazee wa Ibungu na Kalalo kama zawadi ya kwaheri kwa kuishi nao vizuri na kusaidia katika miradi ya maendeleo
Barabara ya Ibungu-Kalalo baada ya kupigwa mkeka. Chini wadau wakiwajibika katika kampeni ya mkeka kwa mkeka
Na Mpeli Nsekela
Mwisho wa kukaa kwa Yoshie Shitomi nchini Tanzania ulikaribia alipoagwa na wanavitongoji wa Kalalo na Ibungu katika viwanja vya ghala la kahawa kitongojini Ibungu, wilayani Rungwe, Mkoani Mbeya.
Yoshie- maana yake Neema kwa Kiswahili- ni mfanyakazi wa kujitolea aliyeletwa nchini na JICA (Japanese International Cooperation Agency) na amekaa kwa muda wa miaka miwili; katika kipindi kikubwa cha muda huo amekaa Ilenge wilayani Rungwe, kwenye Chuo cha Mafunzo Cha Teknolojia ya Nguvukazi (Appropritae Technology Training Institute, ATTI).
Shitomi amejihusisha na miradi ya maendeleo ya ujenzi wa barabara kwa kutumia nguvukazi wilayani Rungwe ikiwemo barabara inayounganisha vitongoji vya Ibungu na Kalalo katika vijiji vya Katabe na Lufingo.
Gwalusako Mafwenga (mwenyekiti wa Kalalo) na Albert Mahena (Mwenyekiti wa Ibungu) walitoa shukurani zao za dhati kwa kazi aliyoifanya Shitomi na kusema alifanya kazi kana kwamba mwisho wa siku angeibeba barabara hiyo kwenda nayo nyumbani Japan.
Shitomi ameonyesha uadilifu, uchapa kazi, uvumilivu na moyo wa kujitolea katika ujenzi wa barabara hiyo na alisimamia fungu la takribani 2,500,000/= lilotolewa na JICA kama mchango wa kujenga barabara ya Ibungu-Kalalo, walisema.
Wadau wengine waliojitolea katika ujenzi wa barabara hii ni pamoja na: Chuo cha ATTI ambao walitoa vifaa vya kuchimbia kushindilia na kusombea mali ghafi na waalimu na mafunzo kwa wananchi wa Kalalo na Ibungu katika ujenzi wa barabara hiyo; mzaliwa wa Kalalo Gwamaka Mafwenga aliyetoa shilingi 470,000/=; familia ya mzaliwa wa Kalalo Professor Tuli Kassimoto (pia ni Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Teofilio Kissanji) iliyochanga 200,000/=; familia ya mzawa wa Kalalo Kasyanju 50,000/=; familia ya mzawa wa wa Kalalo Kasyanju 50,000/=; familia ya mzawa wa Ibungu Kasyanju......... iliyotoa 50,000/=; familia ya Nsekela ambayo imechangia gharama za uratibu, maombi ya vibali, mawasiliano, uhamasishaji wa michango na misaada na usafiri ya barabara hiyo na wananchi wa Ibungu na Kalalo ambao nguvukazi yao inatathminiwa kuwa zaidi ya 10,000,000/= ifikapo mwisho wa ujenzi wa barabara hiyo.
Mpaka sasa kilomita 0.8 zimejengwa kati ya kilomita 3. Michango ya fedha kugharamia diseli na posho za wakufunzi na waendesha mitambo bado inadendelea kusakwa kutoka kwa Wanarungwe na wadau wote wa maendeleo. Wanavitongoji wa Kalalo na Ibungu wamefungua akaunti maaluum kwa shughuli zao za maendeleo za pamoja, ikiwemo barabara hii, Ibungu-Kalalo Maendeleo Account 6142300927, National Finance Bank, tawi la Tukuyu. Takribani 6,000,000/= zinasakwa kumalizia barabara hii.
Shitomi alipewa zawadi za pekee za kitamaduni za ukumbusho kwa kutambua mchango wake mkubwa katika mradi huu wa maendeleo kama kiungo muhimu kati ya wana-Kalalo na Ibungu na JICA na wana-Kalalo na Ibungu na ATTI.
David Malango wa Kalalo, aliyetolea maelezo zawadi za kitamaduni alizopewa Yoshie, alisema barabara ya Ibungu-Kalalo ingeleta neema kwa wana-vitongoji sawa sawa na maana ya jina lake Yoshie kwa Kiswahili, yaani Neema.
Malango alisema kikapu cheusi kiitwacho ‘i Kiibo’ kwa kinyakyusa ni kikapu ambacho kilikuwa hakikosekani katika nyumba ya mama wa kinyakyusa na kilitumika kwa kupelekea zawadi na chakula kwa ndugu na jamaa na kwenye shughuli kama harusi na misiba.
Malango aliongezea kwamba i Kiibo husukwa kwa kutumia matete yaliyopasuliwa na kusukwa na kamba za asili zilizotengenezwa na mimea ya porini na ilikuwa zawadi ya akina mama wa vitongoji hivyo viwili.Rangi nyeusi ya i Kiibo hutokana na moshi kwa kukitunza kikapu hicho darini juu ya sehemu ya kukoea moto.
Zawadi ya akina baba ilikuwa ‘i Kitana’ ambacho ni chombo cha asili cha kukamulia, kuhifadhia na kunywea maziwa.I Kitana hutengenezwa kwa kutumia mianzi mikubwa. Kiasili ukamuaji wa maziwa na ufugaji wa ng’ombe ulikuwa ukifanywa na wanaume wa Kinyakyusa aliongezea Malango.
Yoshie vile vile alipewa kuku ajulikanae kama Makongolosi kwa Kinyakyusa ili Yoshie aweze kumuandaa kama chakula cha njiani anapolekea Japan. Kuku huyo anasifika kwa ladha na nyama bora na nzito zaidi ya kuku wengine Unyakyusani alisema Malango.
Aidha Yoshie alipewa mkeka uliosukwa na mwanamama wa Ibungu kamaa ishara nyingine ya shukrani kwa mchango wake wa ujenzi wa barabara itakayowakomboa wanawake na adha ya kubeba mizigo mizito ya mazao kupeleka barabara kuu kutafuta soko: kama Yoshie alivyosaidia kuusuka ‘mkeka’ (barabara) wa Ibungu-Kalalo basi nae alisukiwa mkeka wa kumbukumbu ya kazi yake nzuri, mkeka ambao angeweza kuubeba kwenda nao Japan.
Yoshie alishukuru kwa zawadi za kipekee na alisema alifurahishwa kushirikiana na wana Kalalo na Ibungu katika ujenzi wa barabara; lakini aliasa ushirikishwaji zaidi wa wanawake katika miradi yote ya maendeleo. Alisema hakuona wanawake wakijitokeza vya kutosha katika ujenzi wa barabara ya Ibungu-Kalalo kama alivyoona katika kitongoji jirani cha Ipagika katika Kijiji cha Ilenege. Aliahidi kudumisha uhusiano na wananchi wa Tanzania na kufuatilia wanavyokabiliana na changamoto za maendeleo. Yoshie ameanza safari kurudi nyumbani Japan jana 28 Desemba, 2010 asubuhi.




Ndaga mwe mubombile, mulilime unsebo. Kyala abatulege.
ReplyDeleteJoune Mandwembe
Viongozi wa Tanzania wajifunze kwa mjapani huyo kuonyesha uzalendo kwa nchi isiyo mhusu
ReplyDeletehapo ingekuwa mtanzania ndiye anasimamia ujenzi wa barabara hiyo basi pesa zote zingeliwa
jamani tuwe wazalendo tujenge nchi yetu
ndagha ni mbombo jha kyala iji mukubhomba.Kyala abhasajebhosa abha bhasosisye indalama.
ReplyDeletena sisi wengine tunaohitaji maendeleo ya wilaya yetu maridhawa ya RUNGWE mstari wa mbele kuunga mkono kwa hali na mali.
NEGWAKO ADAM.
Tanroad mmesikia habari hiyo? sawa sio barabara ya kiwango cha juu sana........lakini km 3 kwa makadirio ya Tshs 10mill.
ReplyDeleteMheshimiwa John Pombe Makufuli kuna somo hapo, barabara zetu za mitaani za kujaza vifusi tu zina quotes kubwa kiasi gani?
Mheshimiwa kuna kitu cha kuangalia katika michakato ya wataalam wetu.....kumbe kugrade barabara ndogondogo kunaweza kuanzia chini kabisa (Tshs 2.5mill)?
Nadhani tumepungukiwa dhamila ya kweli na uadilifu samahani kama nawakwaza wahusika.