Waziri wa Fedha, Uchumi na Maendeleo ya Mipango wa Zanzibar, Omar Yusuf Mzee (kushoto) akitazama kwa makini jinsi majina ya shule za sekondari 104 nchini yanavyopatikana kuweza kupokea msaada wa vitabu katika airtel. Katikati ni meneja wa Huduma za Jamii wa Airtel, Tunu Kavishe. Droo ya kupata shule 104 za sekondari imefanyika jana katika shule ya sekondari Haile Sellasie, Zanzibar.


Serikali imeipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kutokana kwa kuwa na mfululizo wa jitihada za dhati katika kuchangia maendeleo ya elimu nchini na hivyo kuinua maendeleo ya jamii.

Akizungumza visiwani Zanzibar leo, Waziri wa Fedha, Uchumi na Maendeleo ya Mipango, Omar Yusuf Mzee amesema kuwa Airtel imedhihirisha umahiri wake katika mpango wake wa kuhudumia jamii kwa kufukia mamia ya shule za sekondari nchini.

“Tunawashukuru sana kwa msaada na tunawapongezeni sana. Kwa kuangalia idadi ya shule za sekondari ambazo tayari mmekuwa mkizisaidia kwa vitabu kila mwaka, ni uthibitisho tosha juu yadhamira yenu katika kuleta maendeleo ya kizazi kijacho, kama wahenga walivyosema Elimu ni Ufunguo wa Maisha”, alisema.

Waziri Mzee aliyasema hayo wakati wa hafla iliyoandaliwa na Airtel kwa ajili ya kutangaza shule za sekondari 104 zitakazonufaika na msaada wa vitabu, baada ya droo kufanyika katika shule ya sekondari ya Haile Sellassie, Mkunazini.

Aidha, aliongeza kuwa kushiriki kikamilifu kwa sekta binafsi katika kusaidia maendeleo ya elimu nchini ni sehemu muhimu pia katika kudhihirisha ufanisi wa wawekezaji kuhusuana na huduma zao kwa jamii.

Kwa upande wake, Meneja Huduma za Jamii wa Airtel, Tunu Kavishe amesema kuwa kampuni imejiwekea utaratibu wa kudumu wa kurudisha kwa jamii ya watanzania sehemu ya faida ipatayo katika bisashara, kwa kuchangia maendeleo ya elimu.

“Iwapo wanafunzi watapata vitabu na kuhimizwa kuvisoma kwa makini, huweza kuwasaidia kwa namna nyingi na za kipekee, hii ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kufanya vizuri zaidi kitaaluma. Leo hii tumeshuhudia kupatikana kwa shule nyingine 104 za sekondari nchi nzima ambazo zitapokea vitabu kutoka kwetu na hivyo kuendelea kuwahakikishia watanzania kwamba tunayo dhamira ya dhati ya kuendelea kusaidia jamii nchini,” alisisitiza Kavishe.

Kwa zaidi ya miaka saba sasa, kampuni ya simu ya Airtel imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii, hususan vitabu kwa shule za sekondari kwa kuweza kufikia shule zaidi ya 800 nchi nzima.

Kampuni imetenga jumla ya shilingi milioni 104 kwa ajili ya kugharamia msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwa shule za sekondari 104 kutoka mikoa yote Tanzania nzima, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia jamii hapa nchini.

Jumla ya shule za sekondari 520 kutoka nchini kote ziliingizwa katika droo maalumu leo na kisha kupata shule 104 zitakazonufaika na vitabu hivyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...