Watu 24 wamethibitika kufa katika ajali ya milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania kikosi cha 511, Gongo la Mboto Dar es Salaam tarehe 16/02/2011.
Taarifa ya Serikali imeeleza kwamba marehemu wote 24 walitambuliwa na Serikali kugharamia mazishi yao kama ilivyoahidi. Baadhi ya marehemu walisafirishwa kwenda kuzikwa makwao katika Mikoa ya Kagera, Mara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Lindi, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.
Hata hivyo maiti moja ya kichanga cha miezi minane mpaka sasa haijathibitika kuwa kifo chake kilitokana na milipuko ya mabomu, kutokana na taarifa zake za awali kutopatikana katika orodha ya majeruhi waliopokelewa katika dispensari ya Kitunda, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.Taarifa ya awali kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospital ya Muhimbili ilimworodhesha Bwana Abdallah Magadi kuwa ni miongoni mwa marehemu wa milipuko hiyo, wakati yeyé ndiye aliyepeleka mwili wa marehemu Itato Madafu ambaye kifo chake kilitokana na ajali ya gari tarehe 29/1/2011 maeneo ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.
Katika milipuko hiyo ya mabomu zaidi ya watu 512 walijeruhiwa, ambapo Hospitali ya Amana iliwapokea majeruhi 256, Temeke 139, Muhimbili 87, na Zahanati ya Chanika 30.
Katika tukio hilo hadi sasa nyumba 75 zimethibitika kubomolewa, nyumba hizo zilikuwa na kaya 115 zenye watu 539.Aidha, hadi taarifa hii inaandaliwa jumla ya watoto 140 hawajulikani mahali walipo na hivyo Serikali inatoa wito kwa wananchi pindi wawaonapo watoto ambao wanasadikiwa kupotea kufuatia tukio ya milipuko hiyo kutoa taarifa katika vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika vyombo vya habari ili kurahisisha utambuzi wao.
Hadi hivi sasa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa fedha taslim shs. 500,000,000/= kwa ajili ya kulipia huduma za awali zikiwemo gharama za mazishi, rambirambi na kununua vyakula kwa ajili ya waathirika. Pamoja na fedha hizo ofisi hiyo imetoa vifaa vifuatavyo mahema (101), magodoro (538), vyombo vya kupikia makasha (80), seti ya vifaa vya usafi wa mwili (100) Blanketi za wakubwa (400) na Blanketi za watoto (200).
Wakati huo huo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inayoratibu shughuli za maafa ya milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto imepokea misaada mbalimbali fedha na vifaa ikiwemo magodoro, blanketi, shuka, mito, vyandarua, nguo mchanganyiko sabuni, dawa mbalimbali, vyakula kwa ajili ya kuvigawa kwa waathirika.Serikali kwa namna ya pekee inatoa shukrani za dhati kwa wale wote waliotoa misaada ya hali na mali kusaidia waathirika wa janga hili.
Aidha, Serikali inawahakikishia kuwa kazi ya ukusanyaji mabomu inaendelea na inawaomba wananchi kutoa taarifa pindi wayaonapo katika maeneo yao.
Imetolewa Na:
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
24 Februari, 2011
Sasa Idara ya maafa kwa kushirikiana na vikosi vya ujenzi vya JKT/JWTZ waanze mara moja ujenzi wa nyumba zilizobomoka Gongo La Mboto. Zoezi la kujenga lianze mara moja na ziwe zimekamilishwa ndani ya miezi tisa toka leo.
ReplyDeleteNa kusiweko mtu anayelala ktk mahema wote wakodishiwe makazi ktk nyumba za wageni karibu na maeneo zilipokuwapo nyumba zao au wakodishiwe nyumba za kukaa kwa muda karibu na maeneo yao ili watoto wahudhurie shule bila hekaheka, mpaka nyumba zao aikamilike kujengwa na serikali. Hakuna haja ya kufanya thamini kwa nyumba za kawaida labda liwe ni liji-ghorofa.
Pia wazikarabatiki nyumba zilizopata athari lakini hazikubomika, zoezi liishe ndani ya miezi mitatu toka leo.
Urusi wakati wa 'ajali' ya moto mwaka jana, Rais Putin alitoa agizo nyumba zote zilizoungua ktk 'ajali' ya moto wa misitu zijengwe ndani ya miezi sita na agizo hilo lilitekelezwa mara moja na idara za serikali yake.
Mdau
Gongo-La-Mboto.
Na ishirini na nne wamekufa sawa ila bado mtihani upo hao watoto wapatao mia na arobain tuseme vipi! jamani hapa pazito huu msiba ni mkubwa sana.
ReplyDeletesawa watafutwe hao watoto kwanza,
Sasa kama mabomu yametapakaa, kuna uhakika gani hayataangukia kwenye mikono ya wahalifu? Majambazi na hata ma-terrorists?
ReplyDeleteSawa serikali na raia wema wamejitoa kwa hali na mali ili kuweza kukidhi mahitaji ya watanzania waliokumbwa na ajali ya milipuko ya mobumu, suala hili linaonyesha jinsi gani watanzania tunaumoja. LAKINI SASA SERIKALI INAMWAJIBISHA NANI KWA UZEMBE HUU AMBAO UMETOA UHAI WA WATANZANIA WEMA?????????. Si kujenga nyumba na kuwapatia waathirika misaada tu ni lazima viongozi husika wawajibishwe haraka iwezekananyo. Angalau kiongozi hata mmoja wa ulinzi lazima astep down.
ReplyDelete