Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.

TFDA inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma juu ya taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuhusu kuzagaa kwa dawa bandia za malaria katika soko na ukweli kuhusu hali ya ubora na usalama wa dawa za malaria nchini.

Mnamo tarehe 25 Februari 2011, Shirika la Afya Duniani (WHO) ilitoa taarifa ya utafiti ilioufanya kwa kushirikiana na nchi sita zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara chini ya mpango wa ‘Quality of Anti-malarial Medicines in Sub-Saharan Africa – QAMSA’. Utafiti huu ulifanyika katika nchi za Nigeria, Cameroon, Ghana, Kenya, Ethiopia na Tanzania.

Kwa Tanzania, utafiti ulifanyika kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2008 na kuhusisha ufuatiliaji wa ubora na usalama wa dawa za malaria aina ya Artemether + Lumefantrine (ALu), Amodiaquine + Artesunate-co-blistered (AA), Sulfadoxine + Pyrimethamine (SP) Sulfamethoxypyrazine + Pyrimethamine (SPP) na Artesunate + Sulfamethoxypyrazine + Pyrimethamine (ASPP) zinazotengenezwa hapa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Jumla ya sampuli 144 za dawa husika zilikusanywa kutoka katika mikoa mitano (5) ya Mwanza, Tabora, Kigoma, Mtwara na Dar Es Salaam na kufanyiwa uchunguzi wa awali (screening tests) hapa nchini. Kutokana na matokeo ya uchunguzi wa awali, sampuli 45 za dawa husika zilipelekwa kwa ajili ya uchunguzi hakiki (confirmatory tests) katika maabara zilizoteuliwa na WHO zilizopo nchini Afrika Kusini na Marekani.

Matokeo ya uchunguzi huo hakiki yameonesha sampuli tano (5) sawa na asilimia 11 hazikukidhi vigezo vya ubora. Sampuli hizo ni za dawa ya vidonge vya jamii ya SP Sulfadoxine +Pyrimethamine pamoja na vidonge vya Sulfamethoxypyrazine +Pyrimethamine. Aidha, kwa upande wa sampuli za dawa mseto za malaria, matokeo yanaonesha kuwa zilifaulu kwa kiwango cha asilimia 100.

Kwa kuwa TFDA ilishiriki katika utafiti huu, baada ya matokeo haya kupatikana mapema mwaka 2010, ilihakikisha kwamba matoleo (batch) ya dawa ambazo hazikukidhi vigezo vya ubora yanaondolewa katika soko.

Aidha, kupitia kaguzi za ufuatiliaji wa ubora na usalama wa dawa nchini pamoja na uchunguzi wa ubora na usalama wa dawa katika maabara, Mamlaka imeendelea kufuatilia ubora na usalama wa kundi la dawa hizo ambapo hadi sasa hakuna dawa zinazotengenezwa ndani ya nchi na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi zilizoonekana kuwa duni (sub-standard).

Vile vile taarifa ya WHO kuhusu utafiti husika inaonesha kwamba Tanzania ni moja ya nchi zenye mifumo imara ya udhibiti wa ubora na usalama wa dawa (http://www.who.int/prequal).

Kwa maelezo haya, TFDA inawahakikishia wananchi kuwa dawa za malaria zilizopo katika soko ni bora na salama.

Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na:-

Kaimu Mkurugenzi Mkuu

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)

Mabibo External

S.L.P 77150

Dar es Salaam

Tanzania

Simu : + 255 22 2450512/ 2450751 / 2452108

Faksi: + 255 22 2450793

Barua pepe: info@tfda.or.tz Tovuti: www.tfda.or.tz

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Naomba katika kutoa taarifa muhimu utumie lugha inayoeleweka

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...