Ndugu Michuzi,
Nimejaribu kufumba macho na masikio na mdomo kwa muda mrefu lakini taarifa ya mauaji ya watu huko Tegeta imeniuma sana. Imeniumiza moyo wangu kwa huzuni kubwa ya kuona watu wakiuawa kama wanyama wa porini. Siku yangu nzima imeharibika lakini pengine ukiweka maneno yangu kwenye blogu ya jamii itapunguza machungu niliyonayo.

Suala la wananchi kuua watu kwa kutumia nguvu za umma limekuwa ni la kawaida kiasi kwamba katika kila mtaa basi mmoja katika kila watu mia amewahi kushiriki katika mauaji. Yalianza kwa mauaji ya watu wanaoshukiwa kuwa ni wezi kiasi kwamba hata wengine wameuawa kwa chuki baada ya kuitiwa mwizi. Umma ukitumia nguvu zake kuua watu wa umma huo ni UHALIFU.

Watu waliouawa wana familia zinazowategemea je ni nani atakaye beba majukumu ya familia hizo. Tanzania imekuwa ni nchi isiyo na sheria kila mtu anajichukulia sheria kutokana na nguvu zake. Vijana wengi wamepoteza maisha kwa kuiba kuku na vitu vyenye thamani ndogo kulinganisha na maisha ya mwanadamu huyo. Hii yote ni matokeo ya sera za nchi katika kuendeleza wananchi wake. kwa ufupi nchi imekosa dira hatuelewi tunakwenda wapi na naamini tumesha sahau wapi tumetoka maana kama hatujifunzi kutokana historia mambo hujirudia mpaka somo lieleweke.

Mauaji ya watu kwa jina la nguvu ya umma limekuwa la kawaida kwasababu wauaji wanajua kuwa hawatafikishwa kwenye vyombo vya sheria. Swali ninalojiuliza je Polisi waliokabidhiwa jukumu la ulinzi wa raia wako wapi wakati matokeo kama haya yanatokea. Inawezekana vipi Wapiga picha wa TV waweze kufika katika eneo la tukio na kuchukua picha za mauaji bila hata askari mmoja kutokea ni aibu kwa taifa zima. Na pia je hawa watu wa TV waliwezaje kupata taarifa za matokeo na je walitoa taarifa kwa vituo vya polisi na kama walitoa taarifa ni majibu gani walipewa ili kama ni kurekebisha tuanzie huko kwenye vyombo vya usalama mpaka kwa walioshiriki mauaji.

Serikali lazima ifanye jitihada maalumu za kurekebisha mambo haya ya mauaji ya kiholela kwa kutoa elimu na pia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote wanaoshiriki katika vitendo hivi vya kinyama. Na pia serikali iingilie kati na kutoa miongozo ya watu wanaotumia makundi ya watu kutoa ulinzi kama ajira. Na amini kuna njia salama zaidi za kuweza watu kupata haki zao bila kupoteza maisha. Haya makampuni ya Auction ambayo hutumia makundi ya watu kuchukua mali za wanaodaiwa lazima washirikishe vyombo vya usalama badala ya kujenga mazingira ya mapambano kati yao na wanaodaiwa.

Mwisho naomba ujumbe wangu ufike kwa wahusika kwamba ni lini Serikali itakomesha vitendo hivi vya kinyama na lini Serikali itatoa miongozo ya sheria na vitendo kudhibiti watu wa kawaida na makampuni kujichukulia sheria mikononi?

Ni hayo tu, ndimi mwenye kuitakia mema nchi yetu Tanzania. Mungu Tubariki sote na Uibariki nchi yetu na utuondolee mioyo ya kinyama na utuongezee imani na upendo kati yetu.

Mdau Mwanafunzi Masomoni

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 52 mpaka sasa

  1. No Comment!

    ReplyDelete
  2. Inasikitisha kweli. Yaani serikali imeacha watanzania tukafikia hatua ya kuuwana? Ardhi tunayo ya kutosha kwa nini tufikie hatua hiyo? Hayo ndiyo matokeo ya mipango mibovu katika kuendeleza ardhi pamoja na ubabe nadani ya vyombo vyetu vya dola. Wakiambiwa pimeni ardhi mgawie wanachi wanasema oooh upimaji ardhi unagharimu pesa nyingi na sisi hatuna. Na hizi zinazoishia mikononi mwa watu wachache sio hela? Ni uzembe wa serikali. Je zisingetosha kupima ardhi hata kama sio nchi nzima? serikali liangalieni hili. Yawezekana huu ni mwanzo. Huko tuendako hatukujui kama hatua za kuepusha mambo kama haya hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo.

    ReplyDelete
  3. Huyo aliyewapeleka hao watu kubomoa nyumba huku akijua eneo hilo lina mgogoro na wanachi anastahili kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kunyongwa.

    ReplyDelete
  4. Ukisikia nguvu ya wananchi ndiyo hiyo.

    ReplyDelete
  5. what kind of lawlessness is this?

    ReplyDelete
  6. Taarifa hii imeharibu siku yangu nzima ya leo kuona watu wakiuawawa kama wanyama pori katika nchi inayojisifu kuwa ina amani. nitaandika makala kwa ajili ya kueleza yaliyo moyoni kuhusu matokeo kama haya. wananchi wamegeuka wanyama na hata wanyama hawauwi ovyo wanauwa kwasababu ya kupata chakula lakini hawa wako chini ya wanyama. Serikali lazima ichukue hatua muhimu ya kufikisha wote waliohusika katika mauaji hayo kwenye vyombo vya sheria. ushahidi umo kwenye hiyo video wa kuwatambua wote waliohusika. yaani siamini mpaka sasa matendo kama haya yanatokea. UNYAMA WA HALI YA JUU.

    ReplyDelete
  7. Hayo ni matokeo ya uonevu na kupuuza maoni ya wananchi. tusingefika hapo tulipo. Sawa, sheria zipo na lazima zichukuliwe kwa wote waliohusika akiwemo huyo kiongozi aliyewaamuru watu kwenda kubomoa nyumba za wananchi. Lakini kama serikali haitabadilisha namna yake ya kutawala nchi, haya ni madogo tunaweza tukashuhudia mengi huko tuendako.

    Watu wakishafikia hatua ya kukata tamaa matokeo yake ndio hayo. Sasa ubomoe nyumba ya mtu anayeishi kihalali eti kisa eneo kauziwa mwekezaji, unatarajia huyu aliyebomolewa akaishi wapi? Hasira yake ataimalizia kwa huyo mbaya wake hata kama sheria zipo.

    ReplyDelete
  8. Kwani mahakama si zipo. Sheria ya Tanzania inasemaje. Hapa kuna watu waliouawa sasa watafutwe waliaouwa wapelekwe mahakamani. Inaonyesha nchi haina sheria.

    ReplyDelete
  9. Nimesikitika sana kuona unyama huu unatokea kwetu Tanzania hii inaonyesha wazi huko tuendeka amani ahaitakuwepo kwa wenzangu wanaoamini huu ni mwisho wa dunia tumkumbuke Mungu jamani. siku ya leo inaisha vibaya kwangu nimekosa amani kuona watanzania tunakuwa wakatili kiasi hiki jamani

    ReplyDelete
  10. Hii ilikuwa mara ya pili kwenda pale na kuvunja. Hivyo lawama zote ziwaendee wale waliosikia juu ya tukio la kwanza na kunyamaza. Najua ssasa wata-act

    Observer

    ReplyDelete
  11. hiyo imeletwa na uongozi wa jamii yetu, daily tunashuhudia watu wanakuja na mabouncer kuvunja nyumba za raia, tena bila notice, sini shida why wameuawa ni mesegi sent kwa govnt, viwanja vipimwe kila mtu ajue yupo wapi na mipaka yake, manispaa ziache utapeli kuuzia watu viwanja vyenye wamiliki au open spaces, wizara ya ardhi na manispaa zimelala usingizi daily wanantutengenezea mabomu kama hayo! okay thts people power, tukichoka tunaingia front!

    ReplyDelete
  12. Tatizo la wananchi siku hizi ni kuvamia viwanja vya wenyewe kwa madai ni msitu. Watu wengi tu Tanzania tuna viwanja lakini bado tunasaka pesa za kujengea. Wenye uwezo wa kujenga faster faster ni mafisadi tu. Sasa wakati bado unatafuta pesa za kujenga wanavijiji wanavamia maeneo ambayo wamayauza kihalali kabisa.

    Huu mtindo wa kujenga kwenye viwanja vya watu kiholela ukome. Kila mtu ana haki zake

    ReplyDelete
  13. Hii ni Tanzania ama DRC au Ivory Coast? Sijapata kuona upuuzi wa nguvu za dola kushindwa kuwajibika kiasi hicho, kisheria huyo dalali alitakiwa aje na ulinzi wa vyombo vya dola na si raia, halafu uamuzi wa kisheria hutolewa na mahakama na si kampuni binafsi,halafu hii tabia ya wananchi kuchukua hatua ya kuadhibua mpaka kuuwa nayo si jambo la busara, uhai wa binadamu huwezi kulinganisha na thamani ya kitu chochote, hata kama wangekuwa wamevunja nyumba still kuuwa mtu si sahihi, nina laani vikali uzembe wa serikali na uamuzi wa kipuuzi wa viongozi wa kata. Kwa familia waliopoteza wapendwa wao nawapa pole na kuwashauri wachukue hatua za kisheria kuwakamata wote waliojihusisha na mauaji hayo.

    ReplyDelete
  14. Binafsi nilishangazwa sana na ukatili uliopindukia uliooneshwa moja kwa moja kwenye ITV na wananchi wanaodaiwa walikuwa na hasira kali waliokuwa wakitumia kila aina ya silaha kuwaua wabaya wao. Sikuamini hii ni Tanzania ambayo kwa miaka mingi waasisi wa taifa hili wamekuwa wanahimiza amani. Nachoshauri ni kuwa viongozi wote waliohusika kuwahamasisha wananchi waingie vitani wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake. Tuachane na taarifa za polisi tulizozizoea eti fulani kauawa na wananchi wenye hasira kali wakati TV zinaonesha bayana anayeua ni nani.

    ReplyDelete
  15. Pole sana kwa familia zote zilizo athirika, my heart goes out to you.

    I think its time that our media thinks seriously about displaying these type of images! Simply put, by beholding we become. This is certainly not the picture of what Tanzanians are like, but just a few segment of people who prefer this mode of action in resolving issues. What will it profit a man if he gains the whole world and loose his own soul? Sad to say that whoever is responsible for this, whether the police, the locals or the company in question, the damage done to our reputation as a nation has been dragged in the mud!

    ReplyDelete
  16. ...Hapa tatizo kubwa ni kwamba kama polisi wangeshilikishwa haya yote yasinngetokea.kama polisi wangelipewa taarifa nadhani wangelikuwa na namna ya kuchukua hatua ambazo zingeepusha yaliyotokea.

    Mimi nadhani polisi ni muhimu katika kushirikishwa katika mambo kama hayo.Maana polisi nao hawatakurupuka watawasialiana na wakubwa na wakubwa watatoa maelekezo na kufuatilia.katika kufuatilia ulinzi utaimarishwa na pengine hata njia nyingine kupatikana ili kutatua matatizo ya namna hiyo.

    Napinga hoja ya polisi kusema kwamba acha wauane na kisha wa mwisho atatoa taarifa.Huo sio uwaledi kama hakuna askari wa kutosha ni vyema polisi akanyaamza.Ni nini maana ya polisi jamii wanayoihubiri ????.

    Mwenyekeiti wa hilo eneo awe mtuhumiwa na yule mama naye awe mtuhumiwa pili washitakiwa wote wanaonekana kwenye hii clip ni watu wanatambulikana ushahidi upo na kila kitu kipo.

    Ni vipi waandishi wa habari walitabiri kuwepo kule na polisi wasiwepo eneo la tukio???????

    t

    ReplyDelete
  17. HII NDIO MATOKEO YA SERIKALI INAYO ENDESHWA kiungwana BADALA YA KUFUATA SHERIA. RAIS NI MTU MUUNGWANA, IGP NI MTU MUUNGWANA, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NA NAIBU WAKE NI WAUNGWANA NA HATA SHEIKH WETU MKUU NI MUUNGWANA SASA WANACHI WATAFANYA NINI?

    ReplyDelete
  18. hawa wananchi ni waongo huko wazo kazi yao kuvamia tu... mimi kwangu binafsi wameamua kufanya hivi makusudi mbaka kuwauwa siyo mchezo kweli hawa watu wa wazo ni wanyama kabisa.

    ReplyDelete
  19. Common mwananchiApril 08, 2011

    Je amani tunayojivunia iko wapi hapa? Au kwa vile haya si mauaji ya kisiasa? Ndugu zangu, zamani hatukuwa na utamaduni wa kuuwana hadharani namna hii, lakini ilianza kidogo kidogo kwa vibaka na baadhi ya koo ukanda fulani wa nchi na sasa tunaona vita ya kaeneo kamoja. Hapa inatoa picha moja kwamba ILE HOFU TULIYOKUWA NAYO IMETOWEKA NA SASA WATANZANIA TUNAWEZA KUUWANA WENYEWE KWA WENYEWE.

    Hii ni hatari na si dalili nzuri wala ya kuupuuzwa maana imetokea katika ngazi ya mtaa (Tegeta). Najiuliza, kama leo hii kutatotekea tofauti kubwa za kuchochea vurugu kubwa katika eneo kubwa la nchi au nchi nzima baina ya makundi (makabila, dini au vyama vya siasa), je hakutaweza kutokea mauaji ya makubwa ya aina hii??? Tumeshaingiwa na ile roho ya kuuwana na inaweza kufanya kazi popote na kwa ukubwa wowote.

    Sasa badala ya viongozi na wananchi kutumia muda mwingi kujisifu tuna amani na kuwasimanga watu wa nchi nyingine wanaouwana wenyewe kwa wenyewe, ni vizuri tukakemea hili jambo kwa nguvu zetu zote na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria (hata kama itamaanisha kunyongwa) ili kutoa fundisho kwa watu wote wanaofikiri tumefikia mahali pa kuuwana hovyo hovyo. Ni heri tupoteze watano kwa fundisho kuliko kuachwa na wafundishe wengine elfu moja jinsi ya kusababisha na kutekeleza mauaji.

    Kwa bahati mbaya sana,hili jambo kwa viongozi wetu na wale wenye dhamana ya kuchukua hatua, linaweza kuwa sio tatizo kubwa sana kwao, pengine ni kwa kuwa sio jambo la kisiasa au hawajapoteza ndugu na hivyo wanaweza wasichukue hatua stahili kutokana na uzito. Sana sana watasema vyombo vya sheria vipo. Tunaomba, pamoja navyo mchukue hatua kali stahili. Serikali ina nguvu za kutosha kabisa. Wakatisheni tamaa watanzania katika hii tabia ya kuuwana inayokuwa kwa kasi. Kumbukeni mkiacha hii tabia ikue kuna siku itawakuta na nyie wakati ambapo hamtaweza kuchukua hatua tena.

    Namaliza kwa kusema, kwa dhamira hii ya kuuwana tunayoiona sasa haina tofauti na inayotokea nchi nyingine tunazozisimanga. Kuuwa ni kuuwa tu. Ila tatizo ni pale tunapofikiria kwamba mauaji hayo inabidi yawe ya kisiasa au kugombania madaraka ndio tuseme nchi haina amani. Watu watatu wakifa kwa maandamano ya kisiasa kila kiongozi serikalini na taasisi za dini wanajitokeza kulaani kwa nguvu zote na na kusema amani ya nchi ipo mashakani, lakini wakifa watu watano au kumi kwa vita ya ardhi, inaonekana nchi ina amani na utulivu na hatuoni kasi ya kukemea. Tunajidanganya maana uzoefu wa kuuwana kwa ardhi unaweza kutumika kwenye siasa siku moja. Dadisi.

    ReplyDelete
  20. NASIKITIKA KWA MAUAJI YALIOTOKEA MWENYEZI MUNGU AWAPUMZISHE KWA AMANI.
    NAOMBA NITOE MAONI YANGU KAMA IFUATAVYO
    1. SHERIA ZETU NI NZURI LAKINI TARATIBU NI MBOVU MAANA SWALA LA KUPIMA ARDHI NI LAZIMA KWA NCHI NZIMA MAANA ARDHI NDIYO KILA KITU SASA KWETU KUPIMA ARDHI NI HADITHI.
    2. SERIKALI KUGAWA VIWANJA BILA KUPELEKA HADUMA MUHIMU MAANA SHERIA INASEMA LAZIMA KUWE NA HUDUMA ZA KIJAMII KAMA BARABARA NA SHERIA INASEMA NDANI YA MIEZI 36 LAZIMA UWE UMEJENGA, SASA HAPO NDIPO TATIZO LINAPOANZIA MAANA MTU KAPEWA KIWANJA NI MSITU MIAKA KUMI HADI ISHIRINI HAJAJENGA NA HUWEZI KUMYANGANYA MAANA SHERIA INAUMA HUKU NA HUKU KWAMBA HILI UMYANGANYE LAZIMA HUDUMA HIZO MUHIMU ZILIKUWEPO HALAFU UKASHINDWA KUJENGA.SASA HAPO NDIPO WANANCHI HUWA WANAVAMIA MAENEO YA WATU NA KUANZA KUISHI
    3.MKANGANYIKO KATI YA WIZARA YA ARDHI NA MANISPAA KWA MAONI YANGU MAJUKUMU YOTE YA ARDHI YANGEONDOLEWA MANISPAA.

    MWISHO, MIMI NAWEZA KUMALIZA MATATIZO YA ARDHI TANZANIA KWA MIEZI SITA TU, PENDEKEZENI JINA LANGU MHESHIMIWA NITAFANYA HIYO KAZI BURE BILA MALIPO

    ReplyDelete
  21. Haya yote ni matokeo ya serikali na wanasiasa wa bara la Africa, lililoporomoka kisiasa, kiuchumi, na kimadili bila kutambua au kuweshimu utu wa mwanadam, kumekua hakuna khaki katika utu wa mwanadam ilimradi tu kama wavyama wanaoishi mwituni kwa kuwindana na kuwana,

    ReplyDelete
  22. Kwa Mujibu wa NIPASHE, Mwenye kiwanja ni DANIEL CHACHA.Ndie mhamasishaji mkuu wa Mabaunsa wale.Na Polisi wanamshikilia.But guess what?Jamaa ni mkwe wa Kingunge mmoja TANZANIA.hakuna litakalotokea amini , usiamini.
    Pole nchi yangu TANZANIA.

    ReplyDelete
  23. Mtoto wa coastApril 08, 2011

    Natoa pole kwa wote walifiwa, majeruhi na wahanga wa tukio hili la kinyama la kujichukulia sheria mkononi.

    1.Sheria ichukue mkondo wake kwa yeyote aliyehusika kushiriki, kusababisha na kuua au kuumiza raia hawa.

    2. Sheria ichukue mkondo wake kwa yeyeote aliyeonyesha uzembe (kama yupo) kushindwa kuzuia fujo hizo

    3. Sheria ichukue mkondo wake kwa yeyote aliyekiuka taratibu za nchi juu ya umiliki wa ardhi na au ubomoaji majengo na kusababisha tafrani hii.

    Jana pia tumesikia kwenye Tv, Vijana wetu UVCCM - Arusha wakitamka hadharani eti tuko tayari kuwashughulikia, kuwatia adabu, kupambana na Vijana wa CHADEMA wanaoitisha maandamano na kutoa vitisho.

    Polisi & Usalama wa Taifa nadhani tayari mnalifanyia kazi hili na hatua zote muhimu zinachukuliwa kukinga uchafuzi wa amani ambao unaelezwa waziwazi kwenye vyombo vya habari utafikiri wao nao wamekuwa vyombo vya usalama. Mimi sijali chama hapa, uwe CHADEMA au CCM au CUF n.k ukitoa vitisho vya kuleta magomvi mimi nakuripoti polisi na usalama maana hilo halina maslahi Kitaifa.

    Aidha nashauri kuwa serikali iingilie kati (kwa nguvu zote sasa hivi) kutafuta suluhisho katika mgogoro wa kiti cha Umeya wa Arusha pasi kupoteza muda.

    Hatuko tayari kuona nchi yetu yenye amani inakuwa kama aitawaliki huko Arusha kisa eti ni CHADEMA v/s CCM. Nasema enough is enough! Wananchi tunaochukizwa na hali hii tusikae kimya sasa maana yatakaporipuka huko Arusha, tutakuja tena hapa kwa Michuzi na kuanza kutoa pole as if hatukujua kinachofukuta huko.
    Kukinga ni bora na nafuu kuliko kuponya.

    ReplyDelete
  24. Japo sijafuatilia, mdau unaesema sijuhi mahakama ipo. Wewe unaweza kumpeleka muwekezaji au tajiri yeyote mahakamani na ukapewa haki yako? Watu hawana imani na mahakama, polisi wala serikali kwa ujumla ndo maana wanachukua sheria mkononi. Unavunja nyumba ya mtu alafu unategemea aende mahakamani kuendesha kesi miaka kumi, wakati huo familia yake inalala wapi?

    ReplyDelete
  25. Nimesikitika sana kusikia eti Polisi waliitwa kabla, wakakataa kuja kuepusha maafa wakisema ''waache wauane kwanza na yule atakayepona atakuja kuripoti''.
    Hivi kweli hiii ni kauli ya jeshi la polisi???
    Tunaomba aliyetoa kauli hiyo na viongozi wote wa usalama katika eneo husika wachukuliwe hatua kali sana, maana hawafai kabisa katika jamii yoyote duniani.

    ReplyDelete
  26. Jana sikulala. Mwili ulinisisimka kwamba wananchi wako peke yao katika masuala mengi ikiwa ni pamoja na ardhi. Wakati viongozi wao na vyombo vya dola wanakula kwa mrija. Basi kama wako peke yao inabidi watoe hukumu wenyewe kama polisi wako busy. Sio kwamba iwe mazoea kuuana, ila kifo cha watano kiwe fundisho katika suala zito kama kubomoa nyumba iliyojengwa kwa miaka tele. Ni fundisho ili utendaji ubadilike kuepusha kisitokee tena au sio jamani.

    Uvunjaji halali inatakiwa uwe umeandamana na ulinzi wa vyombo vya dola vikiwa na hukumu ya mahakama ambayo haijakatiwa rufaa .. yaani hukumu ya mwisho na kwamba mshitakiwa kakubali kosa na hukumu iliyotolewa. Pia wavunjaji wasiende kimabavu, maana viongozi wa mtaa wapo wawasiane nao kwanza na kama pingamizi linazidi warudi siku nyingine kama kweli wana haki. Mambo ya kutumia pesa bila maarifa ndio matokeo yake sasa haya.

    Sitalala tena leo kwa details nilizosoma. Jamani TZ tuna matatizo makubwa sasa hivi. Tunahitaji utawala bora haraka. Watu wako desparate na mambo mengi ikiwa pamoja na matibabu(mfano; kikombe).

    Msomaji toka Sweden

    ReplyDelete
  27. Nyie mnaokimbilia kuhukumu wananchi 'walioua' mna pesa sana na labda baba zenu ni akina fulani huko serikalini. Hamjui kwamba kwa watanzania walio wengi kujenga ni kitu kinachogharimu karibu maisha!. Zaidi sana kwa walio wengi kupata ardhi ni dream come true. Mimi nimenunua ardhi (hata ya kitapeli!), nikajenga kajumba kangu ka vyumba viwili kwa kujibana miaka mi-5, wewe ni nani mpaka uje kunivunjia ndani ya nusu saa bila taarifa wala makubaliano yoyote! Dhuluma hii mnaifanya sana nyie wenye kipato kikubwa na wengine ni watoto wa mafisadi. Mnanunua mashamba ekari na ekari, hamziendelezi miaka 10, 15, yanakuwa mapori, ofcourse kwa kuwa mmeishika serikali mikononi haiwachukulii hatua yoyote. Walala hoi wakiona pori wanajimilikisha wanaanza kuuziana, mara pori linakuwa kijiji, fisadi ukiona eneo lako limesafishwa na kuwekewa miundo mbinu ndo unaibuka unataka kuwafukuza maelfu ya wananchi wewe uendelee kulimiliki bila kuliendeleza. Hii nchi lazima ifahamike kwamba kukosekana kwa haki na usawa, na matabaka ya walionacho na wasionacho ni bomu linalosubiri kulipuka. Haya tunayoyaona sasa ni onyo kwa serikali na vyombo na watu husika wote. Waache kuwanyima haki walala hoi na kuwapendelea wenye pesa. Fimbo ya mnyonge ni umoja!

    ReplyDelete
  28. si hayo tu ila mengi yatatokea kama serikali haitakuwa makini, ni kiasi gan imeshindwa jukumu lake la dhamana iliyochukua kwa mtanzania,tukisema biashara zao ndio zinazoangaliwa tu sikosei sana na si mwananchi ambaye yupo chini ya mwangalizi wake na ambaye ni serikali!! sasa ona haya mwananchi kwa mwananchi wanauwana!? inasikitisha sana, tena serikali wanasema kila siku inchi yetu inaongozwa kwa sheria na utawala bora, sasa huo utawala bora gani hapo? polisi wanaitwa unasikia majibu yao, itawezakaneje muandishi tena wa tv mpka awepo polis akosekane inachekesha sana, aibu sana tena, mkuu inatuumiza sana mambo kama haya, maisha yenyewe ni magumu sana hebu serikali jaribuni hata kidogo kujali kama mnaongoza watu na si kuangalia ya kwenu tu kama yanaenda,
    sasa hiyo ni aibu gani hii!!

    mdau jp.

    ReplyDelete
  29. Sidhani kama kuna haja ya kuilaumu serikali kila kitu, sisi wenyewe ndio tuna jukumu kwanza la kutendeana haki na kufata sheria b4 hatujailaumu serikali. Uzembe mwingi pia unafanywa na wananchi wenyewe kwa mfano wanaojenga kwenye reserve ya barabara na huku wakiziona alama then wanapewa notes ya kuondoka hawaondoki, serikali inabomoa kwa nguvu wanaanza kuleta fujo na kuwapiga wajenzi. hatukatai pia hao wawekezaji wanajinufaisha kwa kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza hayo ni makosa pia.Lakini ustaarabu na namna nzuri ya kuishi huletwa na watu wenyewe kwanza then serikali inawasimamia na kutekeleza mambo mengine. Hapo juu mtu mmoja ameandika habari ya WAUNGWANA....Nadhani hiyo ni kejeli kwa raisi kwa dini yake,na hizo ndizo jazba zitakazotufikisha Pabaya zaidi, maana vita vya KI-DINI ndivyo vibaya zaidi kuliko hicho kinacoonekana hapo.

    ReplyDelete
  30. Mimi nawaunga mkono wananchi waliowashushia kijapo hao walinzi na kuwaua baadhi. Nyumba haijengwi kwa siku moja. Sasa hapo kuna wakazi zaidi ya 1000. Ina maana kipindi wanajenga, huyo anayejisema kuwa ni mmiliki halali alikuwa wapi? Si angemzuia mtu wa kwanza aliyeanza kujenga??? Hapa kuna usanii, huyo anayejiita mmiliki halali ni FISADI, ana pesa nyingi, hivyo anataka kuwadhulumu wananchi wanyonge. HONGERA WANANCHI KWA MSHIKAMANO MILIOUONESHA

    ReplyDelete
  31. pippoz power

    ReplyDelete
  32. Moshi ulifuka, wakapuuzia, wakaendelea kuongeza kuni na mafuta ya taa, hatimaye moto umewaka ndio wanazinduka. "Nendeni mkauane atakayepona wa mwisho ndiye aje kuripoti" Tafakari!

    ReplyDelete
  33. kingangitiApril 08, 2011

    Kaka michuzi na wadau wote ukweli ni kwamba kwa nchi yetu hili jambo ni la huzuni.Samahani naomba nirekebishe hiki sio kizaazaa ni vita au maafa kwa sababu inaonyesha toka mwanzo ilikuwa ni zako zangu au zao zetu.hapakuwa na mzaha hata kidogo.Eh! toba wee tuliona ya Tarime Labda wenzetu ni wa aina yao sasa tayari roho hiyo ipo Dar ambapo basi si wakazi wa kabila moja wanaishi sehemu moja.Tumechanganyika watu tofauti kila sehemu moja ya jiji la Dar na pembezoni mwake.Lakini tayari tunaweza kuungana nakufanya hili la kutwanga shoka, chapa upanga.Kubaya tunakwenda wandugu.Roho zimeanza kuota sugu kutokana na kuona vibaka wanavyouawa sasa bila woga tunachanja mbuga kwenye miti mibichi.Wacha bwana hata kama ni hasira ya Ardhi ndo iwe jibu kuuana.E Mola tusaidie.Amen

    ReplyDelete
  34. Jaribu kujiweka katika position ya hao wakazi waliokuwa wanavunjiwa nyumba zao. Lazima watu wachanganyikiwe. Hapo ni biita ama zako ama zangu. Univunjie nyumba nikae wapi na familia. Try to be on their shoes. Mimi ni mwanamke mwenye huruma sana. Lakini suala la kumharibia mtu makazi ni sawa na kumuua. Wana haki ya kupigania mali na utu wao. Anayekuvunjia nyumba ni mbaya kuliko jambazi kwani jambazi ataiba TV au ela. Niambie hawa raia (wa kawaida) imewachukua miaka mingapi kujenga? Nambie kama wana uwezo wa kujenga nyumba nyingi? Huyo kijana mmiliki wa eneo (tajiri) utakuta ana nyumba si chini ya Tatu Dar anendelea kujilimbikizia mali. Wacha wawakomeshe itakuwa fundisho kwa wengine

    ReplyDelete
  35. hili ni sakata la kutisikitisha,
    kiasi watu kupoteza uhai wao,wakati chanzo cha mogogoro kinajulikana,
    serekali imekaa kimya,heti mabaunza 400 wanatumwa na kampuni binafsi kuvamia makazi ya wananchi,kama vile hatuna vyombo vya dola????
    Kingine kinachoshangaza hivi kweli Dar mtu ana haki ya kumiliki hekta 200 za Ardhi,wakati Rais wa awamu ya tatu Mstaafu Benjamin Mkapa alishafuta hati zote za kumiliki mashamba makubwa yaliyopo jijini Dar.sasa leo huyu tajiri katokea wapi? je wananchi wanao daiwa kuhama waende wapi?
    Hili ndilo tatizo la kukwepa ukweli

    ReplyDelete
  36. JAMANI TUANGALIA PANDE MBILI. SIYO SAWA KUVAMIA KIWANJA CHA MTU HATA KAMA MWENYEWE HAONEKANI. SIKU HIZI KILA PORI LINA MWENYEWE.

    UTAWALA WA SHERIA NI MZURI. WANAVIJIJI WENGI WAMEKUWA MATAPELI WANAUZA VIWANJA WANAGAWANA PESA WATU KIBAO KIJIJINI. MAPORI YAKIISHA WANAANZA KUDAI WALIONUNUA WAMESHINDWA KUENDELEZA. HAYA NDIYO YALE YALE YA EPA "ETI HIZI HELA HAZINA MWENYEWE". HAKUNA KITU KISICHOKUWA NA MWENYEWE WATU WOTE TUZINGATIE SHERIA. UKISHAUZA KIWANJA INABIDI UTAFUTE MRADI MWINGINE.

    KUVAMIA MALI ZA WATU NA KUWA SKWATA KWENYE MALI YA MTU SIYO SAWA. SHERIA ZIZINGATIWE KWA WOTE.

    ReplyDelete
  37. Mdau aliyepinga mahakama hapo juu. Mahakama ipo kutoa uamuzi. Uamuzi unaweza kutolewa baada ya dakika moja, au, siku moja, au miaka kumi. Mahakama haiwezi kutoa uamuzi bila kuchunguza vizuri. Kama uamuzi haujakuridhisha unapewa nafasi ya kukata rufaa, mpaka mahakama ya mwisho. Sasa kama kuna mtu anapinga amri ya mahakama basi vyombo vya dola vinatakiwa viingilie kati kuhakikisha uamuzi wa mahakama unafuatwa. Sasa kama kuna mtu anahisi kuwa hatapata haki na kuchukua sheria mikononi mwake hiyo itasababisha nchi igeuke kuwa mwenye nguvu ndie mwenyehaki. Kama yule tajiri wa kubomoa alikuja na mabouncer wenye silaha unafikiri ingekuwaje? Wasingelifa watu watano bali ni wengi! Kutawala sio kupanda benzi tu bali kuhakikisha raia wanaishi kwa salama na amani, wanakula, wanalala, wanatibiwa. Je umeiona Iraq au Libya walipofikia, baada ya wanafiki kuwafitinisha raia eti demokrasia hakuna! Muda haukupia mwanamke anakwenda kwenye vyombo vya habari analia baada ya kubakwa. Anaona atapata haki kwa waandishi wa habari, wapi haki kaipata? Nchi hakuna? Mahakama hakuna? Hata kama jaji kala rusha hiyo ni mahakama na wewe kubali uamuzi, sasa kuuwa mtu ndio wewe mbabe? Je wale ndugu zao waliouawa hawezi kwenda tegeta kulipiza kisasi? Ndio maana wazungu wemechemsha kwa Gagbo maana mahakama imeamua kuwa yeye ndie mshindi, sio AU. Sasa mahakama pekee ndio inaweza kubadilisha uamuzi huo, je mahakama imefanya hivyo? Je mnataka kila mtu atembee na silaha yake?

    ReplyDelete
  38. nasikia hawa watu sio watanzania ni wakimbizi waliotoka kigoma ni wacongo ndio maana mnasikia tabia hizo zimetokea... warudi kwao ovyo sana hawa watu..

    ReplyDelete
  39. Kwa kweli serikali ya Tanzania inatutia aibu saaaaaaana.

    ReplyDelete
  40. Hii inaonyesha jinsi gani tulivyofikia kwamba FISADI Vs WATU MASKINI. Wannchi maskini watakwenda jela, FISADI aliyeleta yote haya atakuwa huru. Kwa sababu Hatuna sheria( MAHAKMA) yoyote INYOTOWA HUKUMU kwa FISADI. Sheria ya nchi yetu ni kwa ajili ya maskini tu. Kwa hivyo Nawapongeza wannchi hao kwa kai nzuri waliyoifanya. Maskini pambana na mkono wako hutakaa utambulike popote.

    ReplyDelete
  41. Swali ni je, zile nyumba ambazo zilivunjwa kabla ya kipigo, na yule mama ambaye mwanae mgonjwa alikuwa ndani je angeangukiwa na ukuta nyie mnaoandika kulaani mgesema nini? Je, hata kweli huna kazi wawezaje kukubali kwenda kuvunja nyumba ya mtua ambayo mwenzio kaijenga kwa miaka zaidi ya kumi kwa kujinyima na hali wewe labda unaishi mitaani tu?

    Na wewe mwenye kiwanja una amri ya mahakama kwenda kuvunja? hata kama je ulipeleka written notec ambayo umepewa mahakamani kukuruhusu kuvunja hizo nyumba? je mali zilizomo ndani utazilipaje?

    Tujiulize mengi kabla ya kulaumu walioua. Watu wamechoka, serikali imekuwa ya wenye nacho, Police ndo hao akina Zombe, mawaziri ndo hao akina Mzee wa vijisenti na madowns sasa unataka watu wafanyeje? Watoto wao ndo hao wanapelekwa kwenye shule za kata ambazo sidhani Ridhiwani angesoma au hata matoto wa mwenyekiti wa mtaa haendi huko.

    Mnashangaa wakati mmeona yanayotokea kaskazini mnafikiri huku watu wamelala?? KUMEKUCHA BONGO!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  42. Hivi mtu kama unayo pesa kuliko kwenda kuwalipa hao mabaunsa nadhani ingikuwa bora zaidi angewalipa wanasheria wakashughulikia hiyo kesi kupitia mkono wa sheria.Hapa TZ wako watu wanajifanya kama hii ni nchi yao na yote haya yanasababishwa na elimu finyu.Jamani TZ imebadilika wako wengi tu wameamka wamebakia wachache wapo kwa BABU wanapata kikombe.
    Haya yetu macho tusubiri KATIBA MPYA inasemaje labda itaimarisha ulinzi zaidi.

    ReplyDelete
  43. I always believe that owning land is the graviest sin human could commit. God send us in this world naked and owing our own selfs only. Why should some one then claim land to be his? ownig and even trade with it? Do you all agree with me that most of the world conflics are caused by land and territory desputes?? SIN

    Malisa(BG)

    ReplyDelete
  44. aisee eneo hilo kaka michuzi sitapita na hata kiwanja siwezi kununua maana unaweza kuuwawa.

    Something must be done

    ReplyDelete
  45. KUNTRY BOYApril 09, 2011

    wAKULAUMIWA NI POLISI FULL STOP. BEFORE ANYTHING HAPPEN WALISHATAARIFIWA NA HAWAKUTOKEA. WANGEFIKA MAPEMA MENGI YANGEEPUKIKA.
    MWEMA THIS IS A STAIN IN YOUR CARRIER.
    hii ndo kazi yenu panapotokea mgogoro nyi ndo wakuwepo pale kuweka usalama mpaka usuluhishi utakapo patikana.Hii ndiyo product ya rushwa na ufisadi.

    ReplyDelete
  46. Mi nawaonea huruma waliokufa sijui walipewa shilling ngapi kwenda huko kubomoa. Ila Serikali inatakiwa kuangalia pande zote. Mimi nina kiwanja na kuna tajiri mmoja alianza kujenga kwenye kiwanja changu. Mungu mkubwa mama yangu sijui ilikuaje alikwenda huko kwenye kiwanja na kukuta watu wanajenga kuwaulizia wanasema wanajenga nyumba ya huyo kiboba..mama naye akatuma fundi na matofali kidogo sijui na vikorokoro gani naye akawa anajenga kesho yake. Wale watu wakamwambia huyo boss wao sasa yule mtu akaja juu na kusema eti hata kama ni changu lakini yeye ameshaanza kujenga hivyo tumlipe hela. Mama alishaanza kumsikiliza mi nikamwambia mama kwanza sijui alikua anajenga nini na liyemwambia ajenge ni nani? Nenda mahakamani upeleke documents zote waweke stop ya mtu kujenga hapo na bahati nina cousin lawyer akatushauri the same. Mara alivyoona hatumwachii tumepewa barua ya kumsimamisha kujenga akaja na na ujinga mwingine akasema aninunulie kiwanja kingine sijui wapi huko. Alizania amekutana na mama basi mjinga tu. Mama akamwambia aliyekutuma uanze kujenga kwenye kiwanja siyo chako mwambie aje abomoe. Hakuja kubomoa ila hakuendelea kujenga na mimi naendelea kujenga upande mwingine ila sijui huko alikoanza kujenga alikua anajenga nini...

    Mafisadi ndio wanaweza kujenga kwa mwaka mmoja lakini siye wabeba box tumejikusanya kununua kiwanja. Unahangaika kuweka hela ujenge mara mtu anachukua kiwanja chako bila hata huruma. Au ndio hivyo anatuma watu kuvunja nyumba bila hata kibali. Utajuaje nani ndio mmilikiji wa kiwanja hicho bila mwakilishi wa sheria hapo? We unatuma watu tu hujui nani ni nani...Watu wa pande zote wako responsible...

    ReplyDelete
  47. jamani ndugu zangu mnaosema huu ni unyama mnaijua adha ya kubomolewa nyumba ambayo ndiyo kitu pekee ulichojiwekea ili usilale mitaroni siku ya kesho? Wewe unayesema huu ni unyama mtu akija kukubomolea nyumba pekee uliyo nayo,utaenda polisi ili hali unajua wazi pale ni rushwa kuingia, ni rushwa kutoka?? Mtu mwenye uwezo wa kipesa wa kuajiri majambazi 400 unaweza kusimama naye mahakani, kwa maana kwamba atashindwa kuhonga hakimu mmoja? Sasa kwa kuwa ukifuata sheria au sharya kwa vyovyote utapoteza, kwanini usitafute njia ya kuwaangamiza hawa maadui kabla hawajakudhuru?? Wito wangu kwenu nyote; ukiona dalili ya ujmbazi popote UA. Kinga ni bora kuliko kutibu akija mtu anayeonyesha dalili za kupokonya Ardhi yako kijanja janja ita majirani MALIZA. Haifia kuona mtu mmoja analiza watu 100 ili kwamba adhulumu mali yao kwa kuwa yeye ana pesa. Hizo pesa nazo keba. Halafu kitu kingine ambacho hakiingi akilini; wale wabomoaji walikuwa hawaonekaini kama watu taahira!! Ajira gani ya kwenda kubomoa nyumba za watu ndiyo ulipwe; yeye huyu aliyeuawa angekuta mtu anabomaoa nyumba ya mama yake kwa maelezo kwamba katumwa na ChAcHa angemsamehe?? pumbavu kabisa!!
    Tumieni akilia zenu. uA.

    ReplyDelete
  48. hii kesi inaonekana iko wazi kabisa. Uongozi unauza viwanja mara mbilimbili. Wanauza mara ya kwanza wakiona hela tamu na hakuna maeneo mengine wanaanza kuuza mle mle walimouza kwanza. Sasa inaonekana huyu aliyeleta mabaunsa ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo. Lakini uongozi uliwachopeka watu ndani ya eneo la walilokwisha muuzia huyu jamaa aliyeleta mabaunsa.

    Kama umewahi kuwa na mgogoro wa kiwanja utaelewa nini kinaendelea hapa. Huku maeneo ya madale, tegeta, wazo, mbweni na maeneo ya bagamoyo wanakijiji wanatabia ya kuuza viwanja na kisha kuja kuvivamia ili wauze tena. Ukienda polisi kuhusiana na masuala ya viwanja hata siku moja hawasaidii chochote.

    Ndio maana jamaa alijioganaizi kivyake vyake sema ndiyo moto umemlipukia. Serikali ionyeshe mfano kwa uongozi wa eneo la mivumoni kwa kuwachukulia hatua kali. Hakuna ardhi inayokaa bila mwenyewe. Watu wasirukie tu viwanja na kuanza kujijengea kiholela

    ReplyDelete
  49. Nampongeza sana mweyekiti wa serikali ya mtaa kwa ushujaa wake aliouonesha kwa kuwakusanya wale anaowaongoza kupigana na majambazi wa mwangata! Tanzania haina sheria na ndio maana walioletwa kuvunja hawakua na hati yoyote ya kisheria. Hongera wakazi wa Tegeta kutokutaka kutawaliwa bali kuongozwa, sasa nchi yetu inayobebwa na chama kinachojiita tawala badala ya kiongozi na kama ambavyo wamekua wakilalama kua nchi inaelekea kutotawalika wanadhani kuna wajinga wa kutawaliwa Tanzania wapo tena? Watanzania wamekua wafungwa ndani ya miaka 50 ya uhuru wa bendera sasa wamekosa uvumilivu waache wavyunje gereza hilo! Kumekucha Tanzania watu watafute haki kwa upanga maana hakuna sheria ya kutoa haki kwani 'watawala' wana roho ya ulafi! Tanzania tunahitaji viongozi kama Deogratius Kamugisha mkt wa serikali ya mtaa ya Tegeta na sio kama tuliowazoea wanaojiita watawala wa Tanzania yetu! By Dingi- Arusha

    ReplyDelete
  50. Duhuuu, wananchi wana nguvu aisee. Hii yaashiria nini?

    ReplyDelete
  51. hawa mabaunsa hawakwenda kwa ajili ya vita wala ugomvi. walikua na baraka za mahakama kuwaondoa hao wavamizi. na kwa utaratibu wa eviction and demolition broker anaenda kubomoa na kama akishindwa ndo anarudi mahakamani kuomba nguvu ya dola kumsaidia. kwa hili la mivumoni hii ndo ilikua attempt ya kwanza na hao wavamizi wakawaua hao mabaunsa wa hiyo kampuni ya udalali. deo kamugisha (mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa mivumoni)na mama makete (mvamizi na sponsor) ndo walikusanya vijana toka maeneo mbali mbali kuzunguka hilo shamba na kuwapa hela ili wawaue hao vijana wa kampuni ya udalali wa mahakama tena wakiwa wamekimbia 1.5 KM toka eneo la tukio. hii inaonyesha kua walidhamilia kufanya hivyo.

    ReplyDelete
  52. Kosa la kwanza kwa wote wanakijiji na mabaunsa wa dalali.

    Ikiwa ubomoaji wenyewe unaweza kuhatarisha maisha ya watu je wanakijiji wangengoja ukuta uwaangukie?. Pande zote zina makosa kwa kuwa njia ya mazungumzo haikutumika.

    Kosa la pili

    Polisi wakakosa kuwepo katika sehemu ambapo usalama wa raia ulikuwa umeisha tishiwa.

    Hukumu ya tukio hili isiwe one sided!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...