
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (aliesimama) akitoa changamoto kwa wasichana kutilia mkazo Elimu badala ya kujihusisha na vitendo vya mapenzi na vinginevyo vinavyohatarisha masomo yao alipokuwa katika ziara yake mkoani Iringa hivi karibuni..

Mh. Naibu waziri katika picha ya pamoja na wanafunzi na mwalimu mkuu.

Wanafunzi wakimsikiliza kwa makini mh.naibu waziri.
Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ametoa changamoto kwa wasichana kutilia mkazo Elimu badala ya kujihusisha na vitendo vya mapenzi na vinginevyo vinavyohatarisha masomo yao.
Mhe. Ummy Mwalimu alitoa rai hiyo wakati alipoongea na wasichana wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa iliyopo katika manispaa ya Iringa na Shule za Sekondari za Maria Nyerere na Makambako zilizopo wilayani Njombe. Katika mikutano yake hiyo, mhe. Ummy Mwalimu aliwaeleza wanafunzi hao kuwa Tanzania haitaweza kuwa na maendeleo ya kweli kama asilimia kubwa ya wanawake hawana elimu.
Alisema hii ni sababu wanawake ndio wanaofanya sehemu kubwa ya malezi ya watoto na familia na pia shughuli za kilimo na uzalishaji mali. Mhe. Mwalimu alisisitiza kuwa mojawapo ya shabaha ya Lengo la Tatu la milennia (MDG3) ni kuleta usawa wa jinsia katika elimu katika ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vya Elimu ya Juu.
Naibu waziri aliwaeleza wasichana hao kuwa serikali imechukua hatua za makusudi za kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike. “Wakati nchi imeweza kuwaandikisha wasichana wengi katika elimu ya msingi na sekondari, ninakerwa kuona kuwa idadi kubwa ya wasichana wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu ya mimba na utoro”, alisema.
Akiongea kwa lugha ya kirafiki na wasichana hao, Mhe. Ummy Mwalimu alisema “mashosti zangu, msichana mjanja ni elimu, hayo mambo mengine baadae”.
Kauli iliyowafanya wasichana kushangilia sana. Aliwataka wasichana hao kumuona yeye kama mfano mzuri kuwa msichana anaweza kufika mbali kimaisha kama atatilia mkazo Elimu.
Huku akisitiza kuwa yeye amesoma shule za serikali kuanzia msingi na sekondari kama wao, aliwaeleza “mashosti zangu nyie ndio Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wachumi, Wakurugenzi, Madaktari, Wanasheria wa kesho. Nawaona kina Anna Makinda zaidi ya 10 hapa”. Kauli iliyowafanya wasichana wa Makambako sekondari kulipuka kwa furaha.
Mhe. Ummy Mwalimu aliwataka wasichana hao kuitumia nafasi waliyopata ipasavyo kwani ni wavulana wengi tu wenye sifa kama za baadhi yao ambao hawakuweza kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Pia aliwapa changamoto ya kufanya vizuri zaidi ya wavulana huku akiwahamasisha kuwa “Hivi ni kitu gani kinatufanya tushindwe na wavulana katika masomo yetu?? Wao wanatuzidi nini zaidi? Wasichana hao walijibu kwa sauti kubwa hakunaaaa”.
Kama ni hivyo basi tunakubaliana Iringa girls bila division zero inawezakana. Wanafunzi wote wakasema Inawezekanaa!!!.
Mh Ummy Mwalimu alimalizia kwa kusema kuwa kama Tanzania itaweza kutimiza kwa ukamilifu Lengo la Milenium namba 3 ambalo ni usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake, basi itakuwa ni chachu kwa nchi kuweza kutimiza malengo mengine ya millennia kama lengo namba 4 (Afya ya Mtoto), lengo namba 5 (afya ya Mama) na lengo namba 6 ( kupambana na Ukimwi/VVU) na lengo namba 2 (Elimu ya Msingi kwa Wote).
Katika ziara hiyo ya mkoa wa Iringa, Naibu Waziri Ummy Mwalimu alitembelea pia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vya Njombe, Ulembwe na Ilula na Vyuo vya Maaendeleo ya Jamii vya Ruaha na Rungemba, katika vyuo hivi aliongea na watumishi na kukagua uendeshaji wa vyuo. Vilevile aliongea na watumishi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri za Iringa Manispaa, Njombe na Kilolo.
Mhe. Ummy Mwalimu alieleza kuwa madhumuni ya ziara yake hiyo yalikuwa kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike, kukagua uendeshaji wa vyuo vilivyopo chini ya wizara yake mkoani Iringa, Maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na matumizi ya Majumba ya Maendeleo (Community Centers).
Kwani kuwa waziri wa wizara ya Jinsia na watoto maana yake ni waziri wa wanawake? Ukitoka hapo tuone pia unaongea na watoto wa kiume. Usipofanya hivyo ina maana watoto wa kiume unawaruhusu waendekeze vitendo vya mapenzi. Tumieni akili!!!
ReplyDelete