![]() |
Na Mwandishi wetu
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI wamemchagua bwana Constantine Nyilawila (pichani) kuwa Katibu wa Baraza hilo.
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa uchaguzi huo Afisa Elimu Kazi Mwandamizi kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana bwana Sebastian Inoshi alimtangaza bwana Nyilawila kuwa mshindi wa nafasi hiyo baada ya kupata kura 19 dhidi ya mpinzani wake Bibi Ziada Msangi ambaye alipata kura 18. Kabla ya kufanyika uchaguzi huo, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Bibi Ziada Msangi ambaye sasa anakuwa katibu Msaidizi.
Bwana Nyilawila ambaye kitaaluma ni Mhasibu kwa sasa ni Mkaguzi wa ndani Mwandamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na aliingia katika baraza hilo la wafanyakazi kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2007 akiwa Mwakilishi wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani.
Mnamo mwaka 2009, alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza, akijaza nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na bwana Apolinary Tamayamali ambaye alihamishiwa Ofisi ya Rais.
Mara baada ya uchaguzi huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Kapteni Mstaafu George Huruma Mkuchika aliwapongeza Viongozi hao na kuwataka wawe wawakilishi wazuri wa wafanyakazi wa Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mkuchika alisisitiza umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuhakikisha kuwa wanalitekeleza kwa ufanisi jukumu kubwa la uratibu wa shughuli za Kisekta katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Hapa tujiulize, Je tunaisaidiaje Mikoa na Halmashauri kutekeleza wajibu wao kikamilifu? Tunapaswa kujipanga sawasawa katika ngazi ya Wizara ili kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu muhimu wa uratibu,” alisema.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma bwana John Mchenya aliupongeza uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa kuhakikisha kuwa inasimamia vizuri maslahi ya watumishi wake.
Aliongeza kuwa kutokana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuwajali watumishi wake Ofisi ya TUGHE Mkoa wa Dodoma katika mwaka uliopita haikupokea malalamiko yoyote kutoka kwa watumishi wa wizara hiyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...