Na Mwandishi Wetu.
Wizara ya Maji imeanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Taarifa na Takwimu za Maendeleo ya Sekta ya Maji. Mfumo huo unaowezesha kupata taarifa za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa njia ya mtandao wa kompyuta umeanza kutekelezwa na Wizara ya Maji na Taasisi zake zikiwemo Ofisi za Maji za Mabonde, Mamlaka za Majisafi za Miji Mikuu ya Mikoa na Miji Midogo, Miradi ya Kitaifa ya Maji, pamoja na Wakala zinazofanya kazi chini ya Wizara ya Maji.
Watekelezaji wengine wa mfumo huu ni Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo tayari Mafunzo yameanza kutolewa kwa Wahandisi wa Maji kwenye Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji. Mafunzo haya yanafanyika sambamba na matumizi halisi ya mfumo ambapo Mamlaka hizo zimeanza kuweka taarifa zao kwenye mfumo huo wa kompyuta unaotumia mtandao wa intaneti.
Mratibu wa Mafunzo hayo Bw. Joash Nyitambe amesema mafunzo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa yameanza kutolewa tarehe 20 Juni 2011 na yanatarajiwa kukamilishwa tarehe 31 Julai 2011 ambapo takribani Wahandisi wa Maji 153 wa Sekretarieti za Mkoa na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji watapata mafunzo hayo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo mkoani Morogoro, Nyitambe alisema, mfumo huo ulioanza kutekelezwa kwa Awamu utasaidia wadau wote wanaohusika na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo hivi sasa mipango na matumizi ya fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji yatakuwa wazi kwa wadau wote na pia wananchi watakuwa na ufahamu wa miradi ya maji na matumizi ya fedha za miradi kwenye maeneo yao. Lengo ni kuimarisha mfumo wa utendaji na ufuatiliaji wa pamoja katika utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini.
Nyitambe, aliongeza kuwa mfumo huo utarahisisha ukusanyaji wa takwimu na taarifa za Sekta ya Maji kutoka sehemu mbalimbali nchini ukilinganishwa na hali ya sasa ambapo taarifa hazipatikani kwa wakati na vilevile taarifa hizo haziko wazi kwa wadau wote. Kwa kutumia mfumo huu watekelezaji wote wa miradi ya maji watakuwa wakiweka kwenye mfumo wa kompyuta taarifa zote zinazohusu mipango, mikataba na matumizi ya fedha zote za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ili wananchi na wadau wengine waweze kupata ufahamu wa miradi ya maji na fedha zinazotumika kutekeleza miradi hiyo pamoja na Wakandarasi.
“Wizara inaamini kuwa mfumo huo utasaidia kuimarisha dhana ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Wizara kwani utawawezesha wadau wote kupata taarifa za miradi iliyopangwa kutekelezwa na fedha zilizopatikana na matumizi yake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji”. alisema Nyitambe.
Kwa sasa mafunzo yanaendelea katika kituo cha Morogoro yakihusisha Wahandisi wa Maji kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Dodoma, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro. Kituo cha Mbeya kitahusisha mikoa ya Iringa, Rukwa, Ruvuma na Mbeya.
Kituo cha Arusha kitahusisha mikoa ya Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Arusha. Mafunzo yatahitimishwa katika kituo cha Mwanza kwa kuhusisha Halmashauri zilizomo katika Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kagera, Singida, Mara, Kigoma na Mwanza.
Mwelekeo wa Wizara ya Maji katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ni kuimarisha matumizi ya TEKNOHAMA ili kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu, utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa chini ya Sekta ya Maji. Kwa kuanzia taarifa zinazoweza kupatikana kwenye mtandao zinazohusu mipango, mikataba na matumizi ya fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kuanzia mwaka wa fedha 2006/2007 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...