Unko Michuzi tafadhali niwekee mada hii ili wadau wapate kuchambua

Nyumba imara huanza kwenye mipango (plan) maalum inayozingatia vipengele muhimu vitakavyotumiwa ili nyumba itakayojengwa ihimili purukushani za maisha ya kila siku ya mtumiaji wa jengo hilo. Na nyumba imara huanzwa kwa kujenga msingi ulio imara uliothibitika kuweza kubeba uzito wa kuta na paa la nyumba na vitu vitakavyokuwemo na watumiaji wa nyumba hiyo. 

 Nyumba ninayozungumzia hapa ni mfumo mzima wa maisha ya mtanzania na mazingira yake. Wote tunajua kuwa ili tuweze kupata maendeleo ya kweli lazima tuweke msingi imara wa maendeleo hayo.

Maendeleo yako mengi tunaweza kuyapima kwa kutumia kigezo cha muda kama kuna tofauti kati ya muda uliopita na wasasa basi kuna maendeleo. Maendeleo yanaweza kuwa chanya ama hasi. Kama tofauti iliyopo ni bora kuliko tulipoanzia basi tuna maendeleo chanya na kama hali ya sasa ni mbaya zaidi ya iliyopita basi tuna maendeleo hasi ama tunapiga hatua za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Tanzania tunahitaji maendeleo katika Nyanja nyingi tofauti kuanzia nyumbani mpaka makazini. Ni lazima tuamshe fikra zetu kuelewa tulipo na wapi tungependa tuwepo. Naamini wote tunapenda kuishi maisha bora kama tunayoona kwenye TV zinazoonyesha vipindi vya nchi za n’gambo japo mimi nisingependa tuishi kama kopi ya maisha ya TV hizo kwasababu tuna mengi ambayo ni vyema kujivunia na utamaduni ni moja ya mambo muhimu kuyashikilia na kuyaendeleza kwa mtazamo wetu wenyewe badala ya kushurutishwa mabadiliko na wageni. Lakini wengi wetu hatuna muda hata wa dakika moja kufikiri kwanini tupo katika hali hii na tufanye nini kuibadilisha. Wengi wetu huamini maisha bora huja kwa ngekewa ama njia za mkato ambazo wengi wenu mnazijua.

Wengi wetu tumegubikwa na giza la UBINAFSI linalotufanya tusiweze kuona jukumu la mchango wetu na wenzetu katika kubadilisha jamii inayotuzunguka Giza la UBINAFSI huanzia nyumbani na kuhamia makazini na serikalini na kutanda nchi nzima. Ubinafsi unatufanya tusiweze kutoa nafasi kwa yeyote mwengine zaidi yetu.

Nikirudi kwenye misingi bora ya nyumba ya maendeleo lazima kwanza niweke wazi kuwa mipango (Planning) na vitendo(action) ndio chanzo cha mafanikio. Wengi wetu tna mipango mingi na serikali yetu ina mipango mingi lakini vitendo ni tatizo kubwa. 

Wengi wetu hupanga lakini mara nyingi hupangua na kuamua kutotekeleza mipango yetu. Na serikali yetu imepanga mambo mengi lakini utekelezaji wa mipango hiyo hakuna. Mipango imebaki kwenye makabati ya kuhifadhia nyaraka ikioga vumbi. Na hata hiyo ambayo inayotekelezwa basi utekelezaji wake ni asilimia chache inayoshabihiana na mipango ya awali.

Kwa hiyo tumekosa watendaji na pia tumekosa wahakikishaji wa vitendo hivyo. Tunasheria nyingi lakini ubabe ndio unaotawala maamuzi yetu. Na hii inaonekana zaidi katika serikali kufanya uwekezaji toka nje ndio sera namba moja. 

Tunatumia mali nyingi kuliko faida itakayopatikana kuwavutia watu wa nje waje kuwekeza kwenye nchi yetu wakati kama ni uchimbaji wa madini hata hayo makampuni makubwa yalianza kwa kuchimba kwa kutumia sururu na matoroli na wakajiendeleza kielimu na kimsingi mpaka wakaweza kununua mashine za kuchimbia na magari ya kusomba mawe. 

Sasa kwanini na sie tusianze huko kwa kuendeleza kampuni za ndani ya nchi ambazo tuna uhakika wa kuunda ajira ya ndani na pia kujenga teknolojia ya ndani ambayo itahakikisha kuwa ajira inakuwa na utaalamu unazidi na pia pato linabaki ndani ya nchi na hayo ndio maendeleo ya kweli. Kwa nini tunapenda kuwa na ustawi wa tawi kutoa maua bila ya shina na mizizi.

Na msisitizo ni kwamba si ukweli kuwa hakuna watekelezaji ila hawapewi nafasi na kizingiti kikubwa ni ubinafsi uliopo. Hatupeani nafasi ya kujikuza na hatuna upendo wa kweli chuki na ubinafsi ndivyo vinavyotawala nafsi zetu, tunapenda kuona wenzetu wakiwa na tabu hatupendi kuona jirani ana hali nzuri zaidi yetu tunapenda sie tuwe juu zaidi. 

Na kama watu wana sifa za ubinafsi na chuki hata serikali inakuwa na sifa hizo kwasababu serikali ni mkusanyiko wa watu. Kwa hiyo chuki na ubinafsi zinatawala katika maamuzi muhimu ya taifa. Mfano ni hivi karibuni ambapo viongozi wetu wanasema hadharani kama pesa iliyoamuliwa kurejeshwa kwa wananchi wa Tanzania haitapelekwa serikalini basi watazuia hao watakaopewa pesa kunufaisha wananchi..kauli hii inaonyesha chuki na ubinafsi uliopo. Badala ya kuwa hii ni ushindi kwa jamii (WIN WIN situation) imekuwa bora tukose sote.

Na sasa viongozi wanataka kuruhusu kampuni za kigeni kuchimba madini ya Uranium katika mbuga ya Selous, kampuni zitakazochimba zinategemea kupata dola milioni 200 kwa mwaka na kuigawia serikali dola milioni tano ambapo ni sawa na asilimia mbili na nusu ya mapato. 

Je asilimia mbili na nusu inatosha kudhibiti uharibifu wa mazingira utakao tokana na uchimbaji wa madini haya ya hatari. ni Kweli tunataka kuendeleza uchumi lakini tunapapatikia vijichenji wakati noti tunawaachia wageni wakizipeleka kwao huku tukibaki na mashimo na madhara kwa mazingira na kwa watu na wanyama wanaozunguka machimbo.

Tunapenda njia za mkato bila kazi ngumu tunataka mambo ambayo yameshatengenezwa (ready made) wakati tunajua kuwa nchi zilizoendelea hazikuendelea kwa njia ya mkato kwa nini sisi tuweke njia ya mkato mbele. Njia ya mkato ndio inayofanya majumba yakaporomoka na hivyo hivyo uchumi wa nchi kudorora na kudumaa na kuwaacha wananchi wakiwa katika hali mbaya.

Inaonekana kama kwamba viongozi wako katika haraka ya kumaliza malighafi tulizonazo kama vile hawatarajii nchi hii kuwepo baada ya miaka mingi inayokuja. Ni kama hawajaelewa kuwa malighafi ndio itakayofanya nchi kuwa na nafasi katika mataifa siku zijazo.

 Ni kama mfanyabiashara mwenye kuuza mali zake kwa bei ya chee haraka apate kuhama. Nchi yenye kuelewa misingi ya maendeleo kwa mfano Marekani ni nchi yenye mafuta mengi kuliko zote duniani lakini wao ndio wanunuzi wakuu wa mafuta kutoka nchi nje. Inaonyesha jinsi walivyo na mipango ya nchi yao kujikimu kimahitaji miaka mingi inayokuja.

Msingi bora wa maendeleo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kila hatua ya kujenga nchi na kuleta mabadiliko ambayo yanatokana na mikono yao wenyewe. Na nyumba isiyo na msingi si imara na hatimaye huporomoka.

Ndimi Mdau Saidi Ally Saidi aka Mwanafunzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 02, 2011

    This is one great perspective..it's fully evidently we don't know what we really want for us individually and nation wise and that has been a problem for this country so far

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 02, 2011

    Saidi umenena mambo ya maana kwa Taifa letu. Nakuunga mkono mia kwa mia. Hata mimi nilishngaa eti kusikia uchimbaji wa madini ya Uranium katika mbuga ys Selou umepata baraka za watu wa nje. Lakini ndio hao hao wakishirikiana na wakenya waliopinga barabara ya lami isijengwe kukatisha mbuga ya Serengeti. Sasa tunajifunza nini kwa hili? Kwa barabara kujengwa Serengeti ni wazi kuwa wasingepata maslahi yoyote zaidi ya biashara zao zilizopo Kenya kuwa katika wakati mgumu wa kukosa wateja. Na kwa sababu hakuna maslahi kwao wakaamua kutumia kigezo cha uhifadhi wa wanyama ili barabara hiyo isijengwe. Sasa imekuja mbuga ya SelouS, kwa vile kuna madini yatakayowanufaisha basi hakutakuwa na madhara kwa wanyama. Madini yachimbwe tu. UNAFIKI MKUBWA HUU. Bunge la mwaka jana na lile la wakati Daniel Yona akiwa waziri wa nishati na mdini walikataa kata kata madini yasichimbwe mbugani. Leo imekuwaje serikali imekubali jambo kama hilo bila kupitia bungeni? Ubinafsi uliousema ndio unaotumaliza. Lakini mimi na wewe na wengine wenye nia nzuri bado tuna nafasi ya kuamua hatma ya nchi yetu. Mnafikiri ni nini tunaweza kufanya ili hali hii iondoke? Tuatendelea kutoa malalamiko kwenye blogs mpaka lini? Kumbuka kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 02, 2011

    Ubinafsi ni maumbile ya binadamu, huwezi ukauondoa. Isipokuwa nchi inaendeshwa kwa misingi imara iyokubaliwa na wengi. Misingi hiyo ndio inayofanya katiba ya nchi. Watanzania inabidi tuandike katiba ambayo itakuwa ikilindwa na bunge, mahakama na vyombo vya dola. Kilichobaki wananchi wapendekeze katiba mpya ya nchi ambayo itamuhusisha kila raia wa nchi hii.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 02, 2011

    Anony wa tatu, usitetee ubinafsi. Ubinafsi hata kama upo unaweza kumalizwa na utashi wa kuangalia gharama na hasara za ubinafsi. Leo hii wanaotawala wanafurahi kuendeleza ubinafsi kwa vile watanzania wengi hawajaamka na wakazijua sheria. Aliyekuwa mbinafsi atajuta kwa nini aliitumia mali za umma kwa manufaa yake binafsi wakati zilikuwa za watu wote.

    Kuandikwa katiba ni sawa lakini mbona hata hiyo iliyopo inavunjwa na hakuna anayechukuliwa hatua kwa kuvunja katiba? Polisi wanaoua raia kwa visingizio vya uongo je katiba inawaruhusu kufanya hivyo? Katiba peke yake haitakuwa suluhisho kama wananchi wataendelea kulala.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 02, 2011

    Jamani hizi hubiri tunazitoa kila kukicha, Hawa viongozi hawasikii na kibaya zaidi wamelewa madaraka cha msingi hapa apatikane mzalendo DICTATOR maana naamini 65% ya vijana wamechoka kusukumwa kama matahira tutawadhibiti hawa kisha hukumu ifuate ili iwe fundisho hiyo mikataba mibovu kila siku tunaisikia kelele zinakuja baadaye binaadamu gani tusiosikia maumivu nchi ina watu takribani 40 million ila watu wanaonufaika na nchi hii angalia utaona, imefikia wakati hata aibu hawana.Dharau usiseme kumbukeni huu msamiati MASIKINI AKIPATA ...........?

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 02, 2011

    Anony wa pili unastahili kuungwa mkono. Hasara ya ubinafsi ni kubwa kuliko faida yake "in the long run". Hivyo basi mtu anayeona mbali hawezi kuwa mbinafsi hata kama ni kitu amezaliwa nacho. Hata Wazungu walioendelea ni wabinafsi lakini waliona hasara yake ndio maana waliachana na ubinafsi na maendeleo yalipatikana kwenye nchi zao. Hasara za ubinafsi ni vita huko baadae ambayo itamuathiri aliye nacho na asiye nacho, maendeleo duni hasa katika huduma muhimu n.k.

    Fikiri mara mbili kabla hujaamua kuutekeleza ubinafsi.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 03, 2011

    I applaud you for the well thought out article. You have summed it up what I have always been thinking. Your thought really touched me with sadness as you hit the nail on the head. I am sad and emotional because you have managed to make pictured my beloved future Tanzania and picture is not good, I can picture, poverty, suffering, chaos and destruction. People of Tanzania let us wake up and do something now.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...