| Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon |
. Serikali yake yaamua kufundisha Kiswahili tokea shule ya msingi
. Binafsi aomba Rais Kikwete ampelekee mwalimu wa kumfundisha lugha hiyo
Tanzania imeombwa kuisaidia Gabon kubuni, kuanzisha na kusimamia mitaala inayofaa kuanzisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za nchi hiyo kufuatia uamuzi wa Serikali ya Gabon kuanza kufundisha lugha hiyo tokea elimu ya msingi.
Aidha, Rais wa Gabon, Mheshimiwa Ali Bongo Ondimba amemwomba binafsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho kusaidia kumpatia mwalimu binafsi wa kumfundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada zake za kuonyesha mfano wa kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wananchi wake.
Maombi hayo mawili ya Serikali ya Gabon yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika usiku wa Ijumaa, Julai Mosi, 2011, kwenye Ukumbi wa Kijiji cha AU cha Sipopo, nje kidogo ya mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo, ulioko katika Kisiwani cha Bioko.
Viongozi hao wawili, Rais Kikwete na Rais Ondimba walihudhuria Mkutano huo wa siku mbili na Rais Kikwete amekubali maombi hayo ambayo yanathibitisha utekelezaji wa azma yake ya kueneza lugha ya Kiswahili katika Afrika na duniani pote ambayo aliitangaza tokea mwanzoni mwa Urais wake mwishoni mwa 2005.
Gabon inakuwa nchi ya kwanza katika Afrika kukumbatia na kuamua kufundisha Kiswahili mashuleni nje ya nchi za Jumuia ya Mashariki za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda hata kama lugha ya Kiswahili inazungumza na mamilioni ya watu nje ya eneo la Jumuia hiyo ndani na nje ya Afrika.
Kiswahili ni moja ya lugha kuu zinazotumiwa kwa shughuli za mawasiliano katika Umoja wa Afrika na wakati anakubali kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo Januari 31, 2008 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete alitoa hotuba yake ya kukubali nafasi hiyo kwa lugha ya Kiswahili, hatua iliyomjegea sifa kubwa miongoni mwa viongozi wenzake na Waafrika wengine.
AU inazitambua lugha zote za Waafrika kuwa ni lugha rasmi za Bara la Afrika lakini katika shughuli zake za mawasiliano Umoja huo hutumia lugha sita ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno na Kihispania.
Mara baada ya kupokea maombi hayo, Rais Kikwete alimkabidhi jukumu la kufanikisha utekelezaji wa maombi hayo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi, ambaye alikuwa kwenye ujumbe wa msafara wa Mheshimiwa Rais Kikwete kwa ajili ya mkutano huo wa Malabo.
Rais Kikwete ambaye alirejea nchini jioni ya jana, Jumamosi, Julai 2, 2011, leo, Jumapili, Julai 3, 2011, ameanza ziara fupi za mikoa ya Kagera na kigoma.


Safi sana, Mimi mwenyewe Ticha hapa Mhe. Nchimbi, hebu nipe kazi hiyo. Hii inaonyesha namna gani Kiswahili ni lugha pendwa na nchi nyingine duniani. Nadhani sasa umefika wakati iwe ya Computer pia...maana kwenye Software mbalimbali hata kwenye Simu utakuwa unaweza kuchagua kutumia lugha mbalimba lakini huwezi kutumia kiswahili. Ifikie wakati kuwe na PC ziwe na option hizi: Tanzanian Swahili, Kenyan Swahili, Ugandan, DRC, Ruandan n.k. Mbona lugha km kichina, kihindi,kifaransa, kijerumani, kispanyola n.k ni lugha za Computer pia? Bandugu zanguni, huu ni mwanya pia wa ajira kwa Watanzania, hata kuanzisha mashule ya lugha ya kiswahili Afrika nzima, itakuwa poa sana, maana sisi ndo wataalamu wa kiswahili. Naamini wajasiriamali wa kibongo mtatumia nafasi hizi, sio lazima ufanye biashara ya duka...hata kufundisha lugha nayo ni kazi nzuri, tena inalipa si kawaida...kila la heri
ReplyDeleteKazi hizo..tunaomba haki itendeke hapo kupata walimu wazuri wa kufanya kazi hiyo..siyo mambo ya sijui mtoto wa "fulani',shemeji yake na fulani...nk
ReplyDeleteDavid V
Bwana Michuzi, ahalan,
ReplyDeleteBila shaka waweza kukumbuka,nimewahi kujulisha kuwa nawaambia jamaa wengi hapa ughaibuni kuwa njia moja ya kuendeleza utaalamu na matumizi ya lugha, wasisahau kupitia kwenye blog ya jamaa.Bila shaka kuna njia ya kuwapa ujumbe huo hawa jamaa huko Gabon pia.
Wakatabahu
Hongera Rais wetu katika kukuza na kuisambaza lugha yetu, itafika wakati Kiswahili itakiuwa lugha ya waafrika na ndio itakayo yuunganisha. Sasa KAZI KUBWA IKO KATIKA UTEKELEZAJI. Jamani wa Tanzania UTEKELEZAJI ni ziro.... Mh Nchimbi ni mwana siasa, utekelezaji angepewa mtu ambae si mwanasiasa, labda kazi hiyo wangepewa chuo kikuu, au Baraza la Kiswahili Tanzania (KIU)
ReplyDeleteItakuwa aibu na hasara kama Rais wa gabon atasubiri hadi muda wake wa utawala utaisha bado haja pata waalimu wala wataalam....
kazi kweli kweli, Gabon wanataka kujifunza kiswahili, sisi kiswahili kama somo tu shuleni, mashuleni tunatakiwa umombo,dah tumelala sana
ReplyDeleteBasi sasa watakaoenda kufundisha kiswahili huko malupulupu ya fedha za mafuta watakazopata wataziweka mfukoni mwao! Hiyo nchi ni masikini lakini Raisi huyo na mawaziri wake wanakula hela ya nchi vibaya sana, na nadhani watalipa donge nono tu kuwalipa watu watakao tumwa kufundisha kiswahili kwa rais huyo na ndugu zake!
ReplyDeleteAnonymous wa kwanza anafurahisha sana. Kiswahili alichoandika anajua mwenyewe halafu anataka apewe kazi ya kufundisha Wagabon Kiswahili. Kufundisha Kiswahili sio lelemama. Wagabon hawataki kufundishwa kiswahili chetu cha mtaani, wanataka kufundishwa Kiswahili halisi.
ReplyDeleteSerikali yetu ichangamkie nafasi hizi za kazi kwa waalimu wetu wa Kiswahili. Tukizubaa Wakenya watatunyang'anya tonge mdomoni kama kawaida yao.
Kwa mtazamo wa mbali zaidi, Wagabon wanataka kujifunza Kiswahili ili waweze kuja kufanya biashara maeneo ya Afrika Mashariki kwa urahisi zaidi. Na sisi tujiandae kikamilifu kufanya nao biashara vinginevyo tutaishia kulalamika tu.
JAMANI! SWALA LA KUFUNDISHA LINAKABIDHIWA KWA WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO!HATA MIMI SIWEZI KUFANYA HIVYO!
ReplyDeleteHaya hizo ni habari njema kwa lugha yetu ya Kiswahili. Mimi nawakumbusha tu wale mnaokibeza na kuona hakina maana ila kuzungumza kiingereza ndi sifa, basi mjue hamjafikiria sawasawa.
ReplyDeleteNimewahi kufanyakazi hapa Tanzania na watu wa Cameroun, Nigeria na Ghana walionesha nia kubwa ya kujifunza kiswahili wao binafsi na hata katika nchi zao lakini wakalaumu kwamba hawakupata waalimu hata walipotuma maombi kwa serikali ya Tanzania. Kiswahili kitamu eti, nyie acheni mchezo.
Ndio maana kakipenda, kumbe yeye mwenyewe anaitwa BONGO.
ReplyDeleteHizi ni habari njema kwa wadau na watetezi wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.
ReplyDelete