TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Naibu Waziri wa Utamaduni wa china Mhe. Madam Zhao Shaohua anatarajia kuwasili hapa nchini tarehe 27 Julai, 2011 kwa ziara ya kikazi na ataongozana na ujumbe wa viongozi 8 kutoka Wizara na Asasi za Utamaduni nchini China.
Akiwa hapa nchini, Naibu Waziri huyo pamoja na Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo watafungua maonyesho ya picha ambazo zilikuwa matunda ya Mradi wa ‘African Arts –in- Residence Project’ulioratibiwa na kufadhiliwa na Wizara ya Utamaduni ya China.
Maonyesho hayo yatafanyika Makumbusho ya Taifa Mtaa wa Shaban Robert tarehe 27 Julai, 2011 saa 12 jioni.
Aidha, siku ya Alhamisi tarehe 28 Julai, 2011 Ugeni huo utaelekea Dodoma kwa ajili ya kumtembelea Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Mhe. Naibu Waziri Madam Zhao Shaohua anatarajia kutoa msaada wa Dola za Kimarekani 30,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya utamaduni ili kusaidia kukuza na kuendeleza utamaduni wetu.
Pia Wageni hao watatembelea mbuga za wanyama za Lake Manyara na Ngorongoro ili kujionea utajiri wa kitalii wa nchi yetu.
Tarehe 29 Julai, 2011 ugeni huo utatembelea kijiji cha Wachongaji wa vinyago kilichopo Mwenge Jijini Dar es Salaam pamoja na kukagua bustani iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la kuwawekea mazingira mazuri Wachongaji wa kijiji hicho.
Mradi wa African Artists- in-Residence Project uliwashirikisha Wasanii 15 kutoka nchi 15 za ki –Afrika, Tanzania ikiwa moja wapo, kati ya mwaka 2008-2010 huko China.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu Na Mawasiliano,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...