Mkurugenzi wa Msama Auction Mart anayemiliki pia Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kuwalaumu baadhi ya wasanii nchini na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kwa kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Msama Auction Mart, imewalaumu baadhi ya wasanii nchini na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kwa kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Auction Mart anayemiliki pia Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama alisema anawashangaa wadau hao kwa kuziba plasta mdomoni kwa kutolizungumzia suala hilo.

Alisema aliamini kutokana na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wanyonyaji na mitambo yao, wangejitokeza kumuunga mkono, lakini hawajafanya hivyo.

"Hakuna hata msanii mmoja anayeniunga mkono, zaidi ya ushirikiano wa dhati ninaopata kutoka kwa Jeshi la Polisi, lakini naamini nitafanikiwa, atakayeutambua mchango wangu atakuja kunishukuru," alisema Msama.

Msama alieleza kuwa amesambaza zaidi ya vijana 50 nchini kushughulikia tatizo hilo, ambapo sasa wanakamata wanyonyaji wa aina zote za muziki bila kujali maudhui yake.

Aliwataja baadhi ya wanyonyaji waliokwishakamatwa kuwa ni Fred Jumbe, Martin Mkinga, Abdalah Kijemi, Abdallah Salum,Yahya Salum, Razaro John, Amir Kasim, Faraj Amir, Rashid Juma na Mustafa Rashid.

Mpaka sasa kampuni hiyo imefanikiwa kukamata CD feki zenye thamani ya mamilioni ya fedha kutoka kwa wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini, hatua iliyokuja baada ya kuwekwa mitego mbalimbali ya kuwakamata wezi hao.

Msama alisema mbali ya kukamata fedha hizo, lakini pia wamefanikiwa kukamata fedha taslimu zaidi ya sh. milioni 10 kutoka kwa wahalifu hao.

Alisema kampuni yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imefanikiwa kuwatia nguvuni wanyonyaji na wasambazaji wakubwa wa kazi za wasanii zaidi ya wanane, na tayari baadhi yao wamefikishwa mahakamani.

Mbali ya kuwakamata wahusika lakini pia imefanikiwa kukatama mitambo miwili mikubwa ya kudurufu CD yenye uwezo wa kuzalisha CD feki zaidi ya 300 ndani ya dakika 20.

Alisema anaamini kazi ya kulitokomeza tatizo hilo inahitaji ushirikiano wa wadau wote wa muziki, lakini kutokana na kutopata ushirikiano atahakikisha anapambana.

"Ni kazi nzito kuifanya mwenyewe, lakini naamini nitafanikiwa tu, dawa yao nimeshaipata, nitahakikisha napunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa au kulimaliza kabisa," alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Kukamata mtambo wa kuzalisha cd sidhani kama ni sheria,labda ukute huo mtambo unafanya kazi za kukopi cd bila ya hati miliki,kuna ndege zinabeba madini na wanyama kila siku hamkamati,na hao hao mliowakama hawakutoa rushwa ndio maana mnao.
    Maisha yenyewe ya shida kazi za machinga mmewaachia wachina,sasa tukale wapi?

    ReplyDelete
  2. Huyu anony wa kwanza akapimwe, si mzima. Hata hajui Msama ni nani, jeshi ni lipi, raia ni yupi na wizi ni nini!! Tumwombee

    ReplyDelete
  3. Huo ni usanii na kuonea walalahoi, mbona hakamati wahindi ambao ndio wanyonyaji wakuu wa kazi za wasanii? kutaka umaarufu tu hakuna lolote

    ReplyDelete
  4. Lakini we Msama,huoni kama unarudisha nyuma kazi ya kueneza injili ili watu wapate kumjua Bwana Yesu?Maana hawa ndio husaidia watu wa kipato cha chini kuzipata hizo CD/VCD etc feki kwa bei nafuu na kisha kupata ujumbe wa neno la Mungu uliomo.Hilo jukumu waachie watu wa mataifa,wale wa bongo fleva,masebene,taarabu,filamu,nk.Kwa watumishi(waimbaji nyimbo za injili) neno linasema hamtapungukiwa kamwe hata mkiibiwa kazi zenu hasa kwa kuzingatia kuwa mwisho wa siku wizi huo utalenga kueneza injili.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...