Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, akiwa chini ya ulinzi wa askari magereza
Liyumba ambaye kwa sasa anatumikia adhabu katika Gereza la Ukonga kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya umma wakati wa akifanya kazi BoT, anatuhumiwa kukutwa na simu hiyo gerezani na Septemba 2, alifikishwa katika kituo cha Polisi Stakishari kwa mahojiano na polisi.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), John Minja alisema Dar es Salaam jana kwamba kitendo alichokifanya Liyumba kilivunja sheria za nchi na kanuni za jeshi la Magereza.
Hatua hiyo ya Magereza imekuja baada ya polisi kutangaza kwamba haina kanuni inayoweza kutumiwa na jeshi hilo kumtia mtuhumiwa hatiani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alikaririwa mara baada ya Liyumba kuhojiwa akitoa wito kwa Jeshi la Magereza kutoa kanuni zinazoonesha kuwa hilo ni kosa.
Minja alisema Liyumba atapandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo wakati wowote mara baada ya polisi kukamilisha upelelezi wake.
DCP Minja alisema Liyumba alivunja Sheria ya Magereza Namba 34 ya mwaka 1967, Sura ya 58 kifungu cha 85 pamoja na Kanuni za Magereza Tangazo la Serikali (GN) Namba 13 la mwaka 1968.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye hana mamlaka ya kisheria atakayeingiza au kutoa kitu chochote gerezani kilichopigwa marufuku atakuwa na hatia. Kanuni hiyo ya Magereza inabainisha kuwa ni kosa kwa mfungwa yeyote kumiliki kitu chochote asichoruhusiwa kuwa nacho gerezani.
“Simu ni miongoni mwa vitu vilivyopigwa marufuku gerezani. Si mfungwa wala mahabusu tu lakini hata askari wa kawaida haruhusiwi kuingia na simu gerezani isipokuwa mkuu wa gereza na wasaidizi wake tu,” alisema.
Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 85 (1) adhabu ya kukutwa gerezani na kitu chochote kilichopigwa marufuku, ni faini isiyozidi Sh1,000 au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja.
Alisema athari za mahabusu au mfungwa kuwa na simu gerezani ni uwezekano wa kuathiri usalama wa gereza kwa kuwa mhusika anaweza kuitumia kupanga njama za uhalifu au hata kuvuruga ushahidi kwa kuwatishia mashahidi, hakimu au jaji.
“Kwa hiyo Liyumba alipokamatwa na alifikishwa katika kituo cha Polisi Stakishari kuhojiwa na alifunguliwa jalada namba STR/IR/8661/2011 na baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema DCP Minja na kuongeza;
“Wapo wengi tu ambao tulishawakamata na kuwapeleka mahakamani ambao walipatikana na hatia ya kosa na wakatumikia adhabu”.
Akizungumzia suala hilo wakili mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema: “Hili ni kosa la jinai. Ni hatari sana kwa usalama wa gereza kwani mfungwa au mahabusu akiwa na simu anaweza kushirikiana na watu wa nje kupanga njama dhidi ya gereza.”
Wakili huyo aliongeza: “Kwa kuwa anakuwamo ndani, basi anakuwa ameyajua mazingira yote ya gereza na udhaifu wake. Hivyo anaweza kutoa kwa watu wa nje ambao wanaweza kufanikisha kuvamia au kuingia na kuwatorosha wafungwa na mahabusu gerezani.”
Alisema kutokana na kosa hilo, mfungwa au mahabusu anayekamatwa na simu gerezani anafunguliwa mashtaka mahakamani na akipatikana na hatia adhabu yake huwa ni faini au kifungo jela au vyote viwili.
Baada ya kubainika alikuwa na simu gerezani , Liyumba alifikishwa kituo hicho cha Stakishari saa 3:00 asubuhi na kuhojiwa kwa muda wa takriban dakika 30.
Ili kukamilisha uchunguzi wake, Polisi inatarajiwa kushirikiana na kampuni ya simu iliyotumiwa kumwezesha mtuhumiwa kuwasiliana pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kujua alichokuwa akikifanya kwenye hiyo simu.
Liyumba alihukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 24, 2010 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi. Hadi sasa Liyumba amekaa gerezani kwa muda wa miezi 15 tangu alipohukumiwa.
mbona hata bangi imo gerezani seuse simu?
ReplyDeleteFaini isiyozidi Tsh 1000!, sawa na bei ya nzizi mbivu mbili?
ReplyDeleteJe wadau wa haki za binadamu wanasemaje kuhusu hili? Nafikiri tubadilike, wafungwa wapatiwe simu, tv, vyandarua, choo na tuondoshe viboko. Lengo la jela ni mtu asikuwepo kwenye jamii na sio kumtesa na kumzalilisha!
ReplyDeleteHiyo faini si mchezo jamani, ni sawa na nauli ya daladala ya kwenda kazini na kurudi nyumbani. Lakini si ajabu maana sheria inayotumika ni ya mwaka 1968. Kipindi hicho serikali ilikuwa chini ya Nyerere. Kama tunavyomjua Nyerere, alidhibiti mfumo wa bei hivyo pesa ilikuwa na thamani. Siyo hawa wa sasa wasokuwa na mikakati yoyote ya kuendeleza nchi na kutegemea tu kudra za mwenyezi Mungu. Mkifanya utafiti mtagundua kwamba shilingi 1000 ya mwaka 1968 ni hela nyingi sana kwa sasa. Sasa hapa kuna umuhimu wa kubadilisha sheria hii kwa upande wa faini
ReplyDeleteAfadhali bangi ni mmea umeumbwa kuliko simu inayouza nchi...
ReplyDeletemmmm fine soda mbili.Jamani mbona ndogo sana kwa mtu kama yeye?
ReplyDeleteWewe namba moja juu umenichekesha kweli..Bangi kibao kwenye magereza yetu..Sembuse simu!!'Sina mbavu' hapa nilipo
ReplyDeleteDavid V
sasa kama faini ni sh.1000 kuna haja gani ya kumsumbua mzee wa watu waseme tu hata sisi tunaweza kumlipia akila jambo ni siasa
ReplyDelete