Ester Muze na Salama Juma-Maelezo
WAJASIRIAMALI wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za zao la Muhogo wamelalamikia bei ndogo wanayolipwa kutokana na mauzo ya bidhaa zitokanazo na zao hilo.
Hayo yalizungumzwa na mjasiriamali wa kikundi cha Farmers Group Bi .Sharifa Masud katika Wiki ya Muhogo inayoendelea katika viwanja vya Karemjee jijini Dar es Salaam inayotarajiwa kuishia tarehe 16 .
Bi .Masud ameelezea tatizo la bei ya mazao yatokanayo na muhogo kama unga wa muhogo kuwa chini kumechangia kushusha ari ya uzalishaji wa zao hilo nchini .
“Tunatumia gharama nyingi katika kuzalisha muhogo mpaka unafika kwenye soko lakini soko linatukatisha tama kutokana na bei kuwa chini ukilinganisha na gharama nyingi tunazotumia kuzalisha muhogo zikiwemo pembejeo na dawa za wadudu wanaoshambulia mihogo.”alisema Bi Masud.
Aidha amesema zao la Muhogo linafaida nyingi na linatumika katika kutengenezea bidhaa mbalimbali za vyakula ambazo hutumia ngano kama, Maandazi ,Keki na Chapati vilevile, hutumika katika viwanda vya kutengeneza madawa na viwanda vya vipodozi lakini kiwango kidogo cha bei kinazorotesha ongezeko la uzalishaji wa zao hilo.
Kwa upande wake Afisa Mazao wilaya ya Rufiji Bw. Bainga Ismaili ameishukuru serikali kwa mchango wake mkubwa wa kuendeleza kilimo cha zao hilo kwa kuwapa wajasiriamali fursa ya kupata elimu na pembejeo za kilimo kwa bei nafuu.
Aidha Bw.Ismaili amezitaja baadhi ya changamoto zinazokabili zao hilo kuwa ni pamoja na bei kuwa chini, Wanyama mbalimbali kama Nguruwe kulishambulia zao hilo pamoja na wadudu na fangasi kuwa tishio kwa muhogo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...