Ofisa wa benki ya Azania Tanzania Twisakunketa Mwambona (katikati mwenye shati jeupe) akimkabidhi sehemu ya msaada wa vyakula vyenye thamani ya sh.mil 5/- Mkurugenzi Hezekia Mwalugaja (kushoto) wa kituo cha watoto yatima cha Hananasif Orphanage Centre kilichopo Kinondoni Dar es Salaam walipokitembelea mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii.Wanaoshudia ni maofisa wa benki pamoja na baadhi ya watoto wa kituo hicho.
Watoto wa kituo cha kelelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu cha Hananasif Orphanage Centre (HOCET) kilichopo Kinondoni Dar es Salaam wakishusha vyakula na mahitaji mengine yenye thamani ya sh. 5m/- ikiwa ni msaada waliopewa na benki ya Azania Tanzania mwishoni mwa wiki kama sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii.
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Azania Tanzania imetoa vyakula na mahitaji mengine mbalimbali ya thamani ya sh. mil 5/- kwa kituo cha kulea watoto yatima na waishio katika mazingira magumu kinachojulikana kama Hananasif Orphanage Centre (HOCET) kilichopo Kinondoni Dar es Salaam.
Ofisa wa benki hiyo Twisakunketa Mwambona alikabidhi vitu hivyo kwa Mkurugenzi wa kituo hicho Hezekia Mwalugaja mwishoni mwa wiki na kuwataka wadau zaidi kujitokeza kusaidia kituo hicho chenye changamoto nyingi za uendeshaji.
Alisema hatua hiyo ni katika kuthamini utu wa watanzani wenzao wanaojitolea kulea watoto waliopoteza wazazi na wale wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni namna moja au nyingine ya kujenga nguvu kazi ya taifa hivyo wanapaswa kuungwa mkono.
Alisema pamoja na hilo, benki hiyo imekuwa karibu na jamii ya kitanzania katika matukio mbalimbali na kwamba watanzania hao ndio wanaochangia kukua kwa benki hiyo hivyo msaada huo kwa kituo hicho ni miongoni mwa majukumu yake ya kijamii kwa watanzania.
“Tumeguswa kwa namna ya kipekee na mahitaji ya kituo hiki pindi tulipopokea maombi yenu hivyo nasi tukiwa miongoni mwa wadau tunatoa msaada wetu wa vyakula na vitu vingine vyenye thamani ya sh. milioni 5/= ziwasaidie walau kwa uchache kumudu majukumu ya ulezi katika kituo,”
“Lakini pamoja na hilo msaada huu kwa watoto wetu hawa ni sehemu ya uwajibikaji wa benki yetu kwa jamii ya kitanzania ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wetu, hivyo hii ni sehemu ya kazi inayotuimarisha kiutendaji,” alisema Mwambona.
Vitu vilivyotolewa na benki hiyo ni pamoja na Unga wa Sembe,Mchele,Mafuta ya kula, Sukari,Chumvi,Maharagwe,Sabuni na vinywaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo Hezekia Mwalugaja aliishukuru benki hiyo na kuiomba kuongeza tena msaada mwingine kama uwezo utawaruhusu kwani mahitaji bado ni mengi.
Aliwapongeza kwa kutambua umuhimu wao katika kusaidia jamii ya kitanzania kwani uwepo wa benki hiyo unawategemea watanzania kwa kiasi kikubwa hivyo ni vyema kuhakikisha watoto ambao ni taifa la kesho wanapata malezi bora.
Alisema kituo hicho kwa sasa kina jumla ya watoto 114 wenye umri tofauti ambapo changamoto kubwa kwao ni gharama za kusomoesha kwa wale walio sekondari na vyuo lakini pia wamekuwa na kazi kubwa katika kumudu gharama za chakula na matibabu.
Mwalugaja alifafanua kuwa kwa sasa watoto walioko shule za msingi ni 18, walioko sekondari ni 96 na wanaosoma vyuo ni sita.
haya ndio majukum yetu watanzania tusijisahau...Naunga mkono na kuipongeza Azania Ban na wengine wenye jitihada kubwa kama hiz ktk kukabiliana na changamoto hz ktk jamii zetu tunapotokahaya ndio majukum yetu watanzania tusijisahau...Naunga mkono na kuipongeza Azania Ban na wengine wenye jitihada kubwa kama hiz ktk kukabiliana na changamoto hz ktk jamii zetu tunapotoka
ReplyDelete