Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akihutubia wananchi na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye uzinduzi wa Maonesho ya Wizara hiyo jana katika viwanja vya Mnazi mmoja,Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akikata utepe kufungua maonesho ya mabanda ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akimkabidhi cheti Balozi Paul Rupia, aliyewahi kuwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje. Balozi Rupia, amewahi pia kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais Ikulu.
Maonesho ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru yalifunguliwa jana huku Majeshi ya Ulinzi na Usalama yakimwagiwa sifa lukuki kwa kazi ya kutetea amani Afrika na kulinda mipaka ya nchi yetu.
Akifungua maonesho hayo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Waziri wa Mambo ya Nje Mhe. Bernard Membe, amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kipindi cha miaka 50 linastahili pongezi na heshima kubwa kwa ushiriki wake katika vita ya kueneza demokrasia katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Mhe. Waziri amesema ushiriki wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kukomboa Kisiwa cha Anjuani nchini Comoro bila kumwaga damu ni moja ya mifano mingi inayoonyesha kwamba Tanzania inajeshi dogo lakini lenye umahiri mkubwa.
Kuhusu Vita Vya Ukombozi Barani Afrika Mhe. Waziri alisema Tanzania na hususan jeshi letu limekuwa kinara kwa kupigana vita nyingi za ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika kuliko nchi nyingine yoyote.
Alizitaja nchi za Comoro, Sychelles, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, Angola, Afrika Kusini na Burundi kama miongoni mwa nchi ambazo Tanzania imeshiriki kuwapelekea demokrasia aidha kwa kutatua migogoro yake ama kwa kupeleka majeshi kusaidia kuleta amani katika nchi hizo.
Mhe. Waziri alitumia fursa hiyo pia kuelezea mafanikio lukuki ambayo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imeyapata katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Hadi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana duniani ambazo zimeendeleza utamaduni wa kupokezana madaraka ya uongozi wa Nchi kutoka awamu moja hadi nyingine bila kumwaga damu na kuheshimu misingi ya demokrasia kwa njia ya upigaji kura.
"Tuna bahati ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu bila vita vya wenyewe kwa wenyewe, hii ni nadra kwa nchi za kiafrika. Kumbukeni kilichotokea masaa 24 yaliyopita nchini Libya" alisema Mhe. Waziri kwa hisia kali.
Aidha, Wizara katika kutambua mchango uliotolewa na viongozi mbalimbali hususan mabalozi wastaafu waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, walitunikiwa vyeti kama ishara ya heshima kwa utumishi wao kwa Wizara na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Waziri alisema nyota ya Tanzania imezidi kung'aa katika medani za kimataifa kiasi kwamba Mhe. rais amekuwa akiletewa mialiko mbalimbali wakimtaka akasaidie kutatua migigogoro mbalimbali duniani.
Aidha, alitaja kuteuliwa kwa Dr. Asha-Rose Migiro na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mama Liberata Mulamula kuwa Katibu Mtendaji wa kwanza kwenye Jumuiya ya Ukanda Maziwa Makuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...