![]() |
Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi |
Na Bebi Kapenya – MAELEZO- Dar es salaam
Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa wiki ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo katika maonyesho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara kwenye kijiji cha Butiama mkoani Mara .
Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati akitoa tamko kwa waandishi wa habari juu ya shughuli mbalimbali zitakazofanyika Kijijini hapo wakati wa maonyesho ya Wizara hiyo.
Alisema kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwafahamisha wananchi kuhusu mafanikio , changamoto tangu Tanzania bara ipate uhuru katika sekta ya habari, vijana , utamaduni na michezo.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa maonyesho hayo yatashirikisha Idara, Taasisi na Mashirika yote yaliyo chini ya Wazira Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo kwa kuonyesha machapisho ,picha za tangu uhuru hadi leo zikiwa zinaelezea shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa ambazo Tanzania imeshiriki na historia ya nchi hii kwa ujumla.
Alisema kuwa katika maonyesho hayo Wizara hiyo itashiriki katika michezo mbalimbali kama vile mchezo wa bao, soka , mpira wa pete , mbio na kuendesha baiskeli ikiwa ni sehemu ya sherehe.
Katika hatua nyingine Dkt. Nchimbi alisema kuwa Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwashwa Kijijini Butiama mkoani Mara tarehe 14 Mwezi huu ambapo Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal atakuwa mgeni rasmi.
Alisema kuwa Mwenge wa uhuru mwaka huu utakimbizwa katika makao makuu ya mikoa ili kuweza kwenda na muda ambapo kilele chake ni Desemba 9 mwaka huu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tupa alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya shughuli ya Wizara na uwashaji Mwenge yamekamilika na hali ya usalama ni nzuri.
Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kutembelea kijiji hicho kwa ajili ya kuona jinsi Tanzania ilivyothtbutu , kuweza na kuzidi kusonga mbele katika kuleta maendeleo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...