Mtandao wa Wanataaluma Tanzania (TPN) unawaletea kongamano la kwanza kabisa la aina yake katika historia litakalowakutanisha pamoja Wanataaluma kuchanganua wajibu wao katika kuleta ufumbuzi wa maendeleo ya Nchi yetu.
Mtandao wa Wanataaluma Tanzania (TPN) ni shirika la hiari na lisilo la kibiashara. Uanachama wa TPN ni wa wazi kwa mwanataaluma yeyote na madhumuni yetu ni kuimarisha uwezo na wajibu wa Wanataaluma kuendeleza jamii ya Tanzania.
TPN inashawishi maamuzi katika ngazi mbalimbali katika sekta za umma na sekta binafsi kwa kutoa hoja madhubuti kitaaluma na maarifa.
TPN ni wadau muhimu katika maendeleo ya Tanzania, ambapo tangu kuanzishwa kwake wamekuwa wakihamasisha wanataaluma wa Kitanzania kuungana katika kushiriki katika maamuzi, pia kuunga mkono na kutekeleza sera nzuri, huku wakihakikisha kuwa pia wanawasaidia Watanzania wengine katika maendeleo yao kijamii na kiuchumi.
TPN imeamua kuitisha kongamano la Wanataaluma ili kujadili mafanikio na changamoto za Tanzania tangu Uhuru, na kuchambua majukumu yaliyotekelezwa na Wanataaluma katika safari hiyo ndefu. Yatakayoazimiwa kwenye kongamano hili yatakuwa mwongozo kwa mipango ya TPN kusonga Mbele.
Kongamano litawakutanisha Wanataaluma wa Nyanja mbalimbali, watunga sera, wanasiasa na wawekezaji katika viwanda kwa nia ya kujadiliana juu ya majukumu yao ya pamoja kwa njia ya kukosoana kwa njia ya majadialiano yenye kujenga, huku wakitoa mikakati thabiti ya kuendeleza nchi.
Kongamano lina malengo yafuatayo;
· Kuchambua jinsi wanataaluma walivyofanya au ambavyo walipaswa kufanya katika miaka 50 iliyopita
· Kuchambua iwapo sera za sasa na mifumo ya nchi vinaweza kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati, tukitilia maanani mpango wa MKUKUTA na dira ya maendeleo kufikia mwaka 2025
· Kuchambua mfumo wa elimu nchini na kuangalia iwapo una ubora wa kuendeleza nchi
· Tutajadiliana juu ya Taaluma na Maadili
· Kuimarisha uhusiano na Watanzania Wanataaluma wanaoishi nje ya Tanzania.
Siku ya Kongamano zitafanyika shuguli zifuatazao;
Wazungumzaji (Wachokoza mada) watawasilisha masuala ya kimkakati katika kuendeleza nchi ya Tanzania, mathalani (1) Muungano wa Kikanda, utandawazi na kimbilio la ardhi, (2) Biashara ya Kikanda au Kimataifa baina ya nchi za Kiafrika kama njia ya kupunguza utegemezi kwa wafadhili na madhara yake katika maendeleo ya Afrika na (3) mabadiliko ya tabia nchi na nini inachotakiwa kufanya Afrika kunusuru hali hiyo.
Kumtambua Mwasisi wa taifa letu, Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Mada juu ya kujenga uwezo wa pamoja na kunufaika na maarifa. Maada hii itatolewa na mwakilishi wa Jumuia ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi
Hotuba toka kwa Mgeni Rasmi
· Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa TPN wa miaka Mitano (2012-2016)
· Majadiliano katika vikundi vidogovidogo
· Kujenga mtandao miongoni mwa washiriki wa kongamano hili.
Tumemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo. Tuna matumaini kuwa atakuwepo na kufungua rasmi kongamano hilo.
Kutakuwa na Washiriki wapatao 500 tu , jiandikishe sasa ili upate nafasi ya kushiriki.
Tarehe: Jumapili Desemba 4, 2011; Mahali: Mlimani City, Muda: saa 3 asubuhi –saa 7 mchana
Kiingilio ni Shs 20,000 tu, lakini wanachama wa TPN wataingia bure.
Kwa maelezo zaidi na kujiandikisha tafadhali wasiliana na : Ms. Janet Mbene, Katibu Mkuu wa TPN Barua Pepe: Maorchid@gmail.com,
Simu: +255 784 596444, +255 755 067 594.
Karibuni sana tushirikiane wote ili kuijenga nchi yetu,
Phares Magesa
Rais wa TPN,
Barua Pepe: magesa@hotmail.com
+255 (0784/0767/0713) 618320


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...