Na Gladness Mushi, Arusha
MKUU wa wilaya ya Simanjiro,Khalid Mandia amesema wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoani Manyara kupitia meneja wake wa mkoa huo Mhandisi Yohani Kasaini,Novemba 9 mwaka huu watakutana na watu wa mji mdogo wa Mirerani ambao nyumba zao zilizopo barabarani zimewekewa alama ya X.
Mandia aliyasema hayo wakati akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa huo ambaye alitaka ufafanuzi wa suala la watu waliowekewa nyumba na mali zao alama ya X waliopo mji mdogo wa Mirerani.
Alisema Novemba 3 mwaka huu,Tanroads mkoani Manyara watakuwa na kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo,hivyo wapo kwenye mchakato wa kushughulikia suala hilo na pindi watakapomaliza watakutana na wadau hao.
Hali hiyo imejitokeza baada ya mkuu wa mkoa huo kumtaka diwani wa kata ya Mirerani Justin Nyari,kuelezea tatizo hilo kwani mkuu huyo wa mkoa alielezwa kuwa watu wa Mirerani hawataki barabara ya lami ya Kia-Mirerani ijengwe.
Nyari alimueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa watu wa mji mdogo wa Mirerani ambao nyumba na mali zao zimewekewa alama ya X hawapingi maendeleo ya kujengwa barabara ila kinachowakwaza ni kutoshirikishwa kikamilifu kwenye jambo hilo.
Alisema watu hao hawakuelezwa juu ya hatima ya kupata fidia kuhusiana na suala zima la mali na nyumba zao,zilizopo pembeni ya barabara hiyo kuwekwa alama ya X,zaidi ya nyumba na mali zao hizo kuwekewa alama hizo.
“Hawapingi maendeleo ya kujengwa barabara ya lami ila kinachowatatiza ni namna ya kulipwa fidia zao,kwani barabara hiyo imepandishwa hadhi kutoka barabara ya kijiji hadi kuwa ya mkoa,bila kuwa ya wilaya,” alisema Nyari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...