Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue, ambaye kwa niaba ya Tanzania kwa miezi ya Novemba na Desemba amekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa. Baadhi ya majukumu ya Mwenyekiti wa mwezi wa Kundi hilo ni pamoja na kutoa matamko ( statements)kwa niaba ya Afrika yanayolenga kusimamia na kutetea maslahi ya nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Kimataifa kwa ujumla .
Nembo ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu, maarufu kama RIO+20, mkutano huo unatarajiwa kufanyika mwezi Juni mwakani huko Rio de Janairo, Brazil. Pamoja na mambo mengine, mkutano utatumika kufanya tathinimi ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyopitishwa katika mkutano wa Mazingira na maendeleo ( Earth Summitt ) uliofanyika mwaka 1992 ikiwa ni miaka ishirini imepita tangu kufanyika kwake pamoja kujadili kwa kina suala zima la maendeleo endelevu, kupanga na kutoka na maamuzi mapya kuhusu hatima ya baadaye ya maendeleo ya mwanadamu hususani katika miaka 20 ijayo.

Na Mwandishi Maalum

New York
Wakati maandalizi ya mkutano wa kimataifa kuhusu Maendeleo Endelevu ( United Nations Conference on Sustainable Development) maarufu kama RIO+20 yakiwa yanaendelea,Afrika imetoa vipaumbele vyake ambavyo inataka vizingatiwe wakati wa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni,2012 huko Rio de Janairo, Brazil

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe.Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya kundi la nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa. Amesema vipaumbele hivyo vinapashwa kuzingatiwa kwa kuwa ni muhimu katika kufikia malengo ya kuondoa umaskini hasa kwa Afrika kupitia mkakati mpya wa uchumi wa kijani.

Anavitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na, uboreshaji wa uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula, kupambana na kudhibiti kuenea kwa jangwa na uharibifu wa ardhi, usimamizi wa mazingira ya bahari, uimarishaji wa matumizi endelevu ya maliasili ikiwa ni pamoja na maji safi, misitu na viumbe hai.

Vipaumbele vingine ni kukuza matumizi na uzalishaji endelevu na maendeleo ya viwandani na kuhakikisha usimamiaji wa kemikali taka, kukuza utalii endelevu na kuhakikisha upatikanaji wa nishati salama na endelevu.

Kwa siku mbili wadau mbalimbali wakiwamo mabalozi walikutana katika majadiliano ya ya siku mbili hapa Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili maandalizi ya mkutano huo muhimu na ambao utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka duniani kote, wakiwamo wakuu wa nchi na serikali, wanadiplomasia, wanasiasa, wataalamu wa masuala ya maendeleo endelevu, mazingira , tasisi binafsi na za kiraia

Balozi Sefue anasema ni matarajio ya Afrika kwamba, washiriki wa mkutano huo siyo tu watajituma bali pia wataonyesha utashi wa kisiasa katika kuhakikisha kwamba mkutano huo unafanikiwa na kutoka na malengo yanayotekelezeka na ambayo yatakuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.

“Kundi la afrika linatoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuonyesha dhamira na utashi wa kisiasa ili katika mkutano huo wa RIO+20 tuwezwe kutoka na habari yenye matumaini kwa vizazi vijavyo . Afrika pia inapenda kukaribisha kuanzishwa kwa mfumo ambao utasimamia na kufuatilia makubaliano yatakayofikiwa na, pamoja na utekelezaje wake kama suala la dharura” akasema Balozi Sefue.

Akitilia mkazo wa vipaumbele vya Afrika katika suala zima la maendeleo endelevu, Balozi Ombeni Sefue ambaye kwa miezi miwili mfululizo, Tanzania imekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika. Anasema mtizamo wa Afrika ni kutaka kuona kwamba nguzo kuu tatu muhimu kwa maendeleo endelevu zinapewa umuhimu unaolingana bila ya mmoja kupewa uzito wa kipekee.

Anasema “ Afrika inapenda kutoa wito na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa uwiano katika nguzo hizo tatu hasa nguzo ya kuondoa umaskini, bila ya kuongeza mzigo wa ziada kwa nchi zinazoendelea au kuwekwa vikwazo au kuhoji kuhusu matarajio yetu ya maendeleo”

Akaongeza Afrika ingepeda kuona pia kwamba harakati zozote za kubadili mifumo ya kiutendaji ya taasisi za Umoja wa Mataifa ikiwamo ile ya mazingira UNEP inazingatia maslahi ya Afrika.

Wakati maandalizi ya mkutano huo yakiendelea, kumejitokeza dalili za waziwazi mbapo nchi zilizoendelea zimekuwa zikilipa uzito wa aina yake nguzo ya mazingira na kutoa mkazo kidogo katika nguzo ya kuondoa umaskini na hasa ikizingatiwa kwamba nguzo ya mazingira inalenga kuwanufaisha zaidi nchi zilizoendelea kuliko nchi zinazoendelea ambazo kwao nguzo ya muhimu zaidi ni kuondokana na umaskini.

Mkutano wa RIO+20 utafanyika ikiwa ni miaka 20 kupita tangu mkutano mwingine kama huo uliobeba ajenda ya Mazingira na Maendeleo maaruku kama (Earth Summit) ulipofayika mwaka 1992 huko huko Rio de Janairo. Mkutano wa mwakani utatoa fursa ya kufanya tathmini ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1992, kipi kimefanyika, wapi pameshindikana na kwa nini na hali kadhalika kutoa mwekeleo wa miaka 20 ijayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...