Jaji William Hussein Sekule ambaye pamoja na Jaji Joseph Chiondo Masanche wote kutoka Tanzania wameingia katika orodha ya majaji wa Mfumo mpya wa Kimataifa wa kushughulikia kesi za Mashauri ya Masalia ya Mahakama za Makosa ya Jinai ( International Residual Mechanism for Criminal Tribunals) majaji hao wameingia katika orodha hiyo wakiwa ni sehemu ya majaji 25 walioshinda baada ya kupingiwa kura ya siri kati ya majaji 36 walioomba nafasi hiyo. Upigaji kura huo ulifanywa na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa na umekamilika siku ya Jumanne.
Na Mwandishi Maalum
New York
Majaji Joseph Chiondo Masanche na William Hussein Sekule ni kati ya Majaji 25 waliopitishwa na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kuingia kwenye orodha ya majaji wa Mfumo Mpya wa Kimataifa wa kushughulikia kesi za mashauri masalia ya mahakama za makosa ya jinai. (International residual mechanism for criminal tribunals)
Majaji hao wawili walichuana vikali na majaji wengine 36 waliojitokeza kuwania nafasi 25, kwa kila mmoja wao kupigiwa kura ya siri.Upigaji kura uliomalizika jana jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Kufuatia ushindi huo, majaji Masanche na Sekule pamoja na washindi wengine 23 kwa utaratibu wa Mfumo huo wa Kimataifa hawatakuwa majaji wa kudumu isipokuwa watatimiza majukumu yao pale tu watakapoitwa/hitajika.
Ushindi wa Majaji hao licha ya sifa zao binafsi, kwa kiasi kikubwa umetokana na kazi kubwa iliyofanywa na Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na Wizara Mama ( Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) ya kuwafanyia kampeni majaji hao kwa kupita huku na kule kuwaombea kura
Akitangaza majina ya majaji walioshinda, Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Matafa, Bw. Nassir Abdulazizi Al-Nasser amewapongeza na kuwatakia kila la kheri majaji hao.
Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa liliridhia majina ya majaji yaliyopendekezwa kwa Baraza hilo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na kisha majina hayo kupelekwa katika Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa ambako yalipigiwa kura hiyo ya siri.
Mwaka jana, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio namba 1996 la kuanzishwa kwa mfumo huo wa Kimataifa wa kushughulikia umalizaji wa mashauri ya masalia ambapo tawi la ICTR makao yake yatakuwa Arusha ,Tanzania na tawi la ICTY makao yake yatakuwa the Hague, Uholanzi
Kwa upande wa ICTR mfumo huo utaanza kazi Julai mosi mwaka 2012 na ICTY utaanza kazi Julai Mosi 2013 na mifumo yote itakuwa na haki, stahili na wajibu kama ilivyo kwa mahakama hizo ambazo zinatarajiwa kukamilisha kazi zake zote si zaidi ya Disemba 31, 2014
Majaji wengi ambao wameshinda katika kura zilizopigwa hadi mzunguko wa tatu huku wengine wakiachia ngazi njiani, na nchi zao kwenye mabano Liu Daqun ( China),Gberdao Gustave Kam ( Burkina Faso), Aydin Sefa Akay ( Turkey), Carmel Agius ( Malta), Lee Muthonga (Kenya) na Mparany Mamy RichardRajohson (Madagascar).
Wengine ni Patrick Lipton Robison (Jamaica), Florence Arrey (Cameroon), Burton Hall ( Bahamas), Solomy Balungi Bossa (Uganda), Christoph Flugge ( Ujerumani) Bakone Justice Moloto (Afrika ya Kusini) , Ivo Nelson de Caires Batista Rosa ( Portugal)na Aminata Lois Runeni N’gum ( Zimbabwe/Gambia)
Majaji wengine walioshinda katika kinyanyiro hicho ni Theodor Meron ( Marekani), Vagn Prusse Joensen ( Denmark), Alphons Orie (Netherlands), Jose Ricardo de Prada Solaesa ( Spain) Ben Emmerson ( Uingereza), Prisca Matimbe Nyambe ( Zambia), Graciela Susana Ghatti Santana ( Uruguay) na Jean-Claude Antonetti (Ufaransa).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...