Sikinde Ngoma ya Ukae
Wana Msondo Ngoma.
Na Mwandishi Wetu
Bendi kongwe nchini Msondo Ngoma Music na Mlimani Park Orchestra “Sikinde Ngoma ya Ukae” zinataraji kupambana kesho (siku ya Krismasi) mchana hadi usiku wa manane kwenye viwanja vya TCC Club Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo ambalo tayari limevuta hisia za mashabiki wa muziki wa dansi imeandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment chini ya udhamini wa Konyagi.
Onyesho hilo pia ni maalum kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Krisimasi ambapo wapenzi wa muziki watajumuika kwa pamoja kwenye viwanja hivyo kufurahia kumalizika kwa mwaka.
Bendi hizo ambazo zina mashabiki wengi nchini kuliko bendi nyingine zozote, zimeahidi kutowaangusha mashabiki wao kwa kila moja ikijinasimu kuwa itaibuka na ushindi.
Mara nyingi bendi hizo zikipambana huwa ni patashika nguo kuchanika, kwani mbali na mashabiki kushangilia bendi wanazozipenda vibweka na vituko kemkem vimekuwa vikitawala.
Sikinde ambayo iliweka kambi jijini Dar es Salaam imejinasibu kuibwaga Msondo na kudai kuwa hivi sasa haitishi kama ile ya miaka kadhaa iliyopita.
Itakuwa ni mara ya kwanza bendi hizo kupambana Wilayani Temeke na pia sikukuu ya Krisimasi tangu zianzishwe.
Pia katika pambano hilo mbali na kuwakumbuka wanamuziki wao waliofariki, lakini pia itakuwa ni kusherehekea miaka 50 ya Uhuru huku zikiwa bado zinadumu kwani bendi nyingi za rika lao zimeshafutika kwenye ramani ya muziki nchini.
Kiongozi wa bendi hiyo Habibu Jeff jana alisema kuwa hawatishiki na jina la Msondo kwa sababu wao tangu walishawahi kutwaa ubingwa wa muziki nchini mbele ya bendi hiyo.
Wamewataka mashabiki wao wajitokeze kwa wingi bila ya kuwa na wasiwasi kwani watapata burudani ya kutosha kutoka kwao, kwani watapiga zile nyimbo za zamani wakati bendi hiyo inaanzishwa mwaka 1978 kama vile 'Selina', Wiki endi', 'Penzi la Fukara', 'Hiba', 'MV Mapenzi namba 1 na 2 hadi za kisasa kama vile 'Supu Umelitia Nazi' na 'Jinamizi la Talaka'.
Naye kiongozi wa Msondo Said Mabera maarufu kama Doctor amesema kuwa kama kawaida yao Msondo ni bendi isiyoshindwa daima.
Mabera amesema kuwa siri ya bendi hiyo kupata ushindi miaka yote ni ushirikiano wanaoupata wanamuziki na wapenzi wao.
Wamewataka wapenzi wao kama kawaida yao kujitokeza kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu Msondo Ngoma kwani itaporomosha vibao vya enzi za Nuta, Juwata, Ottu hadi Msondo Ngoma.
Baadhi ya nyimbo zao ni 'Nimuokoe nani', 'Zarina', 'Mwanaidi', 'Kanjelenjele', 'Bahati', 'Sesilia', 'Usiue Usiibe', 'Asha Mwana Seif', 'Kauka Nikuvae', Chuma Chikoli Moto', 'Kilio cha Mzima', 'Ajali', 'Suluhu' na nyingine nyingi.
Kikosi cha Sikinde kitakuwa na Hassan Rehani Bitchuka, Hassan Kunyata, Kaingilila Maufi, Tonny Karama, Shaaban Mabuyu, Habib Abassi, Juma Choka, Ally Jamwaka, Athumani Kambi, Mbaraka Othman, Milambo, Shaaban Lendi, Joseph Benard na Ramadhani Mapesa.
Msondo itawategemea akina Shaaban Dede alijiunga hivi karibuni kutoka Sikinde, Mabera, Abdul Ridhiwani Pangamawe, Saad Ally 'Mashine', Eddo Sanga, Huruka Uvuruge, Zahor Bangwe, Ibrahim Kandaya, Ismail Mapanga, James Mawilla, Muhidini Gurumo, Eddo Sanga, Juma Katundu, Hamisi Mnyupe, Roma Mng’ande `Romario’ na Hassan Moshi.



Mpambano Msondo V/S Sikinde,,,,
ReplyDeletePana uwezekano wa aina kama 3 hivi
1.Mtoto anaweza kupigwa na Baba kama ilivyo kawaida ktk siku zote.
AU
2.Mtoto anaweza kuleta upinzani kidogo kwa Baba kwa vile amekua sasa halafu wakatoka sare.(ingawa baba anaweza jitutumua nitakuua wee mtoto, wakati wametoka sare)
AU
3.Mtoto anaweza kugeuza kibao AKAMTWANGA BABA TENA NOKAUTI!
Ahhh sasa hivyo, huyo Mtoto haiwezekani ampige Baba!
ReplyDeleteHata kama atarusha ngumi zake mbili, tatu akamzidi Baba nguvu watatokea Watu watamkamata na ATACHAPWA MAKOFI ATATULIZWA NA ATANYAMAZA, HUKU AKISUBIRI KIKAO CHA WAZEE ILI YEYE KWA UTOVU WA NIDHAMU KUWAJIBISHWA!
Kama kawaida ya Baba leo ni tarehe 26 Disemba atakuwa amesha mwadhibu vilivyo jana mtoto kwa viboko!
ReplyDeleteFamilia zingine utakuta watoto wanafunzi wameacha vitabu vyao kujisomea, wengine wanacheza karata, wanasikiliza redio ,wanatazama TV.
Ile vikisikika viatu vyake baba akiingia ndani ya nyumba yupo barazani hajafungua mlango, utakuta TV inazimwa, karata zinaachwa kuchezwa, kila mtoto ktk kitabu chake anasoma!
Ndio ilivyotokea jana ktk Mpambano Sikinde V/S Msondo.
Baba mchezo?
Ahahah baba anapoingia mtoto inabidi awe na adabu!
ReplyDeleteBaba ya muziki ni shughuli pevu, mtoto lazima atakuwa na dispilini!
ReplyDelete