Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani almarufu 'Profesa Majimarefu' (mbele) akianza kuingia kwenye maji yaliyofurika kutokana na mto Pangani (Ruvu) kujaa maji kupita kiasi na kusababisha kivuko kinachokwenda katika kitongoji cha Majengo kilichopo kijiji cha Manga-Mtindiro kusombwa na maji, wengine katika picha nyuma Mkuu wa wilaya ya Korogwe Bw. Erasto Sima na katikati mmoja ya wajumbe wa serikali ya kijiji hicho, Said Juma.
Mbunge wa Korogwe vijijini Profesa Majimarefu akikiongoza mwenye chombo hicho baada ya nahodha wake Bw. Paul fedreck kushindwa kukimudu hatua ambayo ilibidi mbunge huyo ashike upondo na kukiongoza hadi kwenye kitongoji cha Majengo ambako aliwapa pole wananchi hao kabla ya kutoa sh. 200,000 kwa ajili ya kuvushwa kila siku hadi hapo maji yatakapopungua kisha serikali kutafuta utaratibu wa kujenga upya kivuko hicho.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Bw. Erasto Sima (aliyevaa shati jeusi), akiogopa kuzama baada ya chombo walichopanda akiwa na Mbunge wa korogwe Vijijini Profesa Majimarefu (nyuma yake), kupigwa na wimbi kisha kusogezwa pembeni ya mto Ruvu hatua ambayo iliwagopesha kiasi cha kutaka kurudi walikotoka, lakini hata nohodha wa mtumbwi huo Bw. Paul fedrick kuwatuliza baada ya kukimiliki vema chombo hicho tena, mwingine mbele ni Katibu wa UVCCM mkoa wa Tanga Bw. Acheni maulid akitaka kushika mti ili ashuke.
Nahodha wa mtumbwi Bw. Paul fedrik 'Mamba' akikivuta majini chombo hicho ambacho kimewapakiza Mbunge wa korogwe vijijini Proffesa majimarefu (wa kwanza kulia), Mkuu wa wilaya ya Koogwe Bw. Erasto Sima (katikati) na Katibu wa umoja wa vijana wa CCM mkoa wa Tanga Bw. Acheni Maulid.
Na Mashaka Mhando,Korogwe
ZAIDI ya kaya 250 za kitongoji cha Majengo kilichopo katika kijiji cha Manga-Mtindiro kata ya Mkomazi wilayani hapa, wamekumbwa na athari kubwa za kijamii kwa kutenganishwa na mawasiliano ya kata baada ya mto Pangani (Ruvu) kufurika maji na kusomba kivuko walichokuwa wakikitumia kwenda ng'ambo ya pili ya mto huo.
Wananchi hao ambao sasa wanalazimika kuvuka na mitumbwi ambayo si salama kwao, pia wanakabiliwa na tatizo la kuumwa ugonjwa wa tumbo kila mara kutokana na maji wanayotumia kuchafuka kutokana na mafuriko hayo ambayo yametokana na mvua kunyesha kwenye milima ya Pare na maji kutiririka kwenye mto huo na kujaaa kupita kiasi.
Wakizungumza wakati Mbunge wa jimbo la Korogwe vijijini Bw. Stephen Ngonyani 'Profesa majimarefu' aliyeambatana na Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Erasto Sima, walisema tangu mto huo kujaa hadi sasa wamekuwa wakipata shida kubwa hasa huduma za jamii kama unga, sukari, mafuta na bidhaa nyingine, zimeongezeka bei kutokana na wafanyabiashara hao kupata shida ya kuvuka katika mto huo.
Mtendaji wa kata ya Mkomazi Bw. Yusuph Mtoi katika taarifa yake kwa mbunge alisema kuwa jumla ya ekari 1,177.2 zilizokuwa zimelimwa na kupandwa, zimeharibika kwa kusombwa na maji ambapo kati ya ekari hizo ekari 67 zilikuwa zinakaribia kuvunwa hivyo serikali inahitajika kusaidia haraka chakula kwa wananchi hao ikiwemo mbegu.
Mbunge huyo ambaye alivuka kwa kutumia ngalawa wanazotumia wananchi hao, alijionea tabu na shida wanayopata wakiwa wamepanda ngalawa hizo ambazo haziwezi kuchukua zaidi ya watu watatu kwa vile maji ya mto huo yamekuwa yakipita kwa nguvu kiasi cha wakati mwingine kama nahodha na abiria wake watashindwa kutulia, basi kuna uwezekano mkubwa wa chombo kujaa maji kisha kuzama.
"Mheshimiwa, tulieni tu hakiwezi kuzama, ila mkae chini kabisa mtulie maana tukipita hapa mto wenyewe unapokatisha huko kwengine kuna nafuu, na hapa kuna kina kirefu tukizama ni balaa," alihadharisha abiria wake nahodha wa chombo kimoja ambacho alipanda Mbunge, Mkuu wa wilaya pamoja na katibu wa UVCCM mkoa wa Tanga Acheni Maulidi anayeitwa Paul frank 'Mamba'.
Akizungumza na wananchi hao alipofika kwenye kijiji hicho kujionea namna walivyoweza kuathirika na mafuriko ya mto huo, mbunge huyo alisema kuwa yupo pamoja nao na atahakikisha anatafuta ufumbuzi wa tatizo la kivuko hicho kwa kuwabana viongozi wa serikali ili kuhakikisha kwamba mara baada ya kukauka jitihada nyingine za kujenga kivuko kipya au daraja ziweze kufanyika.
Mbunge huyo ambaye alitoa sh. 200,000 zitumike kuvusha watu kwenda upande wa pili ambako ndiko kunakopatikana huduma za jamii ikiwemo shule, zahanati na huduma nyinginezo, aliwataka wananchi hao wasivuke kama hakuna sababu za msingi za kwenda huko ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea endapo watavuka kwa wingi kwenye mitumbwi wanayotumia.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya alisema kuwa mafuriko hayo yametokea kutokana na mvua kunyesha katika milima ya pare na mto huo kujaaa maji hatua ambayo alisema enmdapo mpango uliopitishiwa na serikali mwaka 2003 wa kujengwa bwawa kubwa katika bonde la Mkomazi pengine suala la mto kujaa hadi kufurika namna hiyo usingetokea baada ya kiasi cha shilingi bilioni 10 kutengwa lakini wananchi hao walikataa.
sinema tupu
ReplyDeletenatoa marekebisho kwamba huo mto Pangani kwa eneo la Korogwe unaitwa Luvu na sio Ruvu. Yaani unaweka "L" badala ya "R"
ReplyDeleteAsante habari nzuri, tupo pamoja Ankal
AISEE UKISEMA TANZANIA TUNA WATU WAJINGA UTAANZA KUTAFUTWA ILA UNA MWENYEWE..
ReplyDeletekama wabunge wote wangekua wanafanya hvi kila kisu, nadhani tungekua mbali kabisa...
ReplyDeleteWhat a vacation! Mheshimiwa alienda kutalii kidogo si ethi eeenhe?
ReplyDelete