Mkurugenzi Mkuu wa EWURA,Haruna Masebu akizungumza leo wakati akitangaza bei mpya ya huduma za Umeme nchini.

Tarehe 9 Novemba 2011, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipokea maombi la dharura kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kuidhinishwa ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa. Maombi haya yalisajiliwa Namba TR-E-11­-012.

Kulingana na maombi yaliyowasilishwa, katika mwaka 2010 na 2011 Tanzania ilikuwa na hali mbaya ya mvua katika maeneo ya mabwawa na hivyo iliathiri uzalishaji wa umeme. Hii ilisababisha nchi kuwa na upungufu mkubwa wa umeme na kuathiri sio tu hali ya kifedha ya TANESCO, bali pia na uchumi kwa ujumla wake.
Ili kumaliza tatizo hilo, TANESCO ilisaini mkataba na IPTL kuzalisha Megawati 100 kwa kutumia mafuta mazito (HFO); ilisaini mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Symbion LLC kuzalisha Megawati 112 kutumia gesi asilia na mafuta; na ilisaini mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Aggreko kuzalisha Megawati 100 kutumia mafuta ya dizeli.

Vilevile, TANESCO inatekeleza mradi wake wa Megawati 150 ambao utatumia gesi asilia pamoja na mafuta (dual fuel plant) na mradi mwingine wa Megawati 70 ambao utatumia mafuta mazito (HFO). Ukiacha miradi ya TANESCO ambayo itakamilika mwaka 2012, umeme unaozalishwa kupitia mikataba tajwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mgao wa umeme hapa nchini. Hata hivyo, juhudi za kumaliza mgao wa umeme zimeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji za TANESCO.

Katika kukabiliana na hali hiyo, TANESCO iliwasilisha maombi ya dharura EWURA ikiomba kuongeza bei za huduma zake kwa 155.

Kulingana na kifungu Na. 15(1)(3) cha Mwongozo wa Uwasilishaji Maombi ya Bei wa mwaka 2009 (Tariff Application Guidelines of 2009), Waziri mwenye dhamana (kwa hali hii) wa Nishati na Madini, aliwasilisha Hati ya Dharura (Certificate of Urgency) EWURA ili maombi husika yaidhinishwe haraka na sio kwa utaratibu wa kawaida.

Tarehe 11 Novemba EWURA ilipokea Hati ya Dharura kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini na hivyo kuanza mchakato wa kupitia maombi ya TANESCO baada ya kupata maoni ya wadau.

Kulingana na Kifungu Na.19(2)(b) cha Sheria ya EWURA (Sura 414 ya Sheria za Tanzania), tarehe 2 Desemba 2011, EWURA ilifanya mkutano jijini Dar es Salaam wa kukusanya maoni ya wadau, kuweka maombi husika katika tovuti ya EWURA, pamoja na kuwaandikia wadau wachache ili waweze kutoa maoni yao kuhusu uhalali wa maombi yaliyowasilishwa na TANESCO. Pia maombi tajwa yalitangazwa katika vyombo vya habari mbalimbali.

Baada ya kufanya uchambuzi wa maombi yaliyowasilishwa pamoja na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA ilikutana tarehe 12 Januari 2012 na kufanya uamuzi, pamoja na mambo mengine:

(a) Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kupunguza makali ya maisha kwa wa Tanzania kwa mosi; kufuta kodi ya mafuta kwenye mitambo, itakuwa inalipia Sh. bilioni 18 gharama za mitambo IPTL (Capacity Charges) na kusamehe deni la Sh. bilioni 136 kwa TANESCO.

(b) Kutokana na ukokotoaji uliofanywa na EWURA, kwa kuzingatia mzigo ambao Serikali imeubeba na pia kwa kuzingatia hali ya hewa ambayo inaweza kufanikisha upatikanaji wa mvua kwa wingi na hivyo kujaza kwenye mabwawa, bei ya umeme itaongezeka kwa wastani wa asilimia 40.29 kwa wateja wote isipokuwa wateja wanaotumia uniti 0 – 50 (0 – 50 kWh) kwa mwezi na ZECO, bei imepunguzwa kwa kwa asilimia 10. Na wafanyakazi wa TANESCO watalipa kama wateja wengine. Bei hizo zitaongezeka kama inavyoonekana katika Jedwali hapa chini.

(c) Bei zilizoidhinishwa zitaanza kutumika tarehe 15 January 2012 mpaka hapo uchambuzi wa kina utakapokamilika na hivyo kutolewa kwa Order nyingine.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Michuzi ilo jedwali la kupanda kwa bei ya umeme liko wapi?

    ReplyDelete
  2. Mmmhhh hiii nchi tunapolekwa itajulikana nda cmrefu matokeo yake.

    ReplyDelete
  3. Inakuwaje serikali isamehe deni kwa TANESCO wakati wao ndiyo waliyoiweka kwenye predicament hiyo? Mikataba feki yote ni kwa nguvu za serikali.

    Vile vile TANESCO wacheni kujipendelea mulipie umeme kama sisi wateja wenu, kwa nini nyinyi mupewe bure wakati munalipwa mishahara vile vile? Angalau mungekuwa munapewa discount ya 10%, lakini unit 700 bure hiyo ni gharama kwetu sisi wateja.

    ReplyDelete
  4. Inakuwaje serikali isamehe deni kwa TANESCO wakati wao ndiyo waliyoiweka kwenye predicament hiyo? Mikataba feki yote ni kwa nguvu za serikali.

    Vile vile TANESCO wacheni kujipendelea mulipie umeme kama sisi wateja wenu, kwa nini nyinyi mupewe bure wakati munalipwa mishahara vile vile? Angalau mungekuwa munapewa discount ya 10%, lakini unit 700 bure hiyo ni gharama kwetu sisi wateja.

    ReplyDelete
  5. wacha tuone kama kuna wabunge watatutetea sisi walala hoi na ongezeko la umeme

    ReplyDelete
  6. Iweje serikali isamehe Tanesco wakati serikali ndiyo iliyo na malimbikizo ya bili za umeme. Hii ni porojo

    ReplyDelete
  7. Haya wabunge zungumzeni sasa kutetea wapiga kura wenu au ndiyo mtajiongezea posho kwa kisingizio cha ugumu wa maisha?

    ReplyDelete
  8. Acheni utani Serikali itasameeje deni wakati wao ndio vinara waliyosababisha yote haya. vilevile kuwalipisha umeme watumishi wa Tanesco mbona mpango huu ulichelewa nadhani Tanesco kwa hesabu za haraka haraka wako takriban 4,000 ukijumlisha na vibarua wao zidisha mara (kwh 700) uone jinsi shirika lilivyo hujumiwa. Hivi mfano kama wafanyakazi wa Shirika la Posta wangetuma Barua na vifurushi bure unadhani shirika lingekuwa wapi kutowatoza garama za Umeme watumishi wa Tanesco ulikuwa niuongo na uzandiki wa Menejiment na Bodi ya Tanesco ukweli nikwamba wananchi ndiyo waliokuwa wakilipisha garama hizi za watumishi hawa wasunbufu wa Tanesco. sasa subirini uchakachuaji maana Wananchi mkiwapandisha garama wao kimya hawalalamiki ila ukimya sio ujinga kuna jambo.

    ReplyDelete
  9. Haki ya Mungu yaani tunalipa DOWANS hivi hivi bila kupenda!....

    ReplyDelete
  10. tumeisha hii nchi inapoelekea ni pabaya sanaaaaaaaaaaaa

    ReplyDelete
  11. Aisee, hii nchi inazama sasa! Hivi EWURA/TANESCO ina "thinkers"? Kuongeza bei za "energy products" maana yake ni kukaribisha mfumuko mkubwa wa bei. Energy ni input katika uzalishaji na usambazaji wa kila product. Sasa umeme, mafuta bei juu! Tusubiri anguko la uchumi..!! Waathirika wakubwa ni wananchi maskini - kwa sababu hawana resources za kutosha kuweza kukabiliana na hizo athari.

    ReplyDelete
  12. SINA MENGI LEO ILA NASEMA KUWA MWISHO WA HAYA YOTE HAUPO MBALI.... KITAELEWEKA TU 2015. AMKENI WATANZANIA SASA TUMECHOKA KUIBIWA HAKI ZETU NA KUNYANYASWA CHUKUENI HATUA KUELEKEA 2015 MWENYE AKILI KANIELEWA!!!

    ReplyDelete
  13. Bei mpaka mtangazie MOVENPICK?

    ReplyDelete
  14. Jamani tangu tupate uhuruhadi leo, hatujaweza kutatua tatizo la umeme jamani?

    Miaka nenda miaka rudi, tatizi hili liko pale pale. Mpaka lini tutagemea mvua? Mpaka lini tutaambiana uongo?Mpaka lini tutaendelea kuvumilia?
    Na sisi pia tunaweza kufanya kama yale yanayoendelea uarabuni sasa hivi. We can start the African Spring. YES WE CAN!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...