TFF YATOA ITC KWA SAMATA, OCHAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji Mbwana Samata na Patrick Ochan waliojiunga na timu ya TP Mazembe wakitokea Simba.

TFF ilipokea maombi ya uhamisho huo wa kimataifa Januari 10 mwaka huu kutoka Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (FECOFA) kwa niaba ya TP Mazembe.

Kwa kupata ITC maana yake ni kuwa Samata na Ochan sasa wanaweza kuichezea TP Mazembe kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo mechi zake za mchujo zinaanza mwezi ujao.

Pia TP Mazembe inatakiwa kulipa asilimia 5 ya mauzo ya Samata ikiwa ni mchango maalumu (Solidarity Contribution) kwa timu alizopitia mchezaji huyo kwani hajafikisha umri wa miaka 23. Timu zitakazopata mgao wa asilimia hiyo 5 ni Kimbangulile FC na Mbagala Market ambayo siku hizi inaitwa African Lyon.

Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho wa wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) fedha hizo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 tangu ITC ilipotolewa kwa mchezaji husika.

TWIGA STARS UWANJANI KESHO
Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) kesho (Januari 14 mwaka huu) inacheza na wenyeji Namibia katika mechi ya kwanza kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayofanyika Uwanja wa Sam Nujoma jijini Windhoek kuanza saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Twiga Stars iliwasili salama jijini Windhoek jana (Januari 12 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ndege ya Air Namibia ikitokea Johannesburg ambapo imefikia Safari Hotel (+264817928904). Baada ya mapumziko jana jioni ilifanya mazoezi.
Leo jioni (Januari 13 mwaka huu) imefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sam Nujoma ambapo ndipo mechi itachezwa kesho. Hali ya hewa ya Windhoek ni baridi kidogo kulinganisha na Dar es Salaam.

USAJILI WA YANGA, SIMBA WAPITA CAF
Wachezaji wote wa klabu za Yanga na Simba walioombewa usajili Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho umepita.

Klabu hizo ziliombea wachezaji 28 kila moja. Hata hivyo Simba ambayo itacheza Kombe la Shirikisho awali iliombea usajili wachezaji 26 kabla ya baadaye kuwaongeza Ulimboka Mwakingwe na Derreck Walulya.

Katika michuano hiyo Yanga imepangiwa Zamalek ya Misri ambapo itaanzia nyumbani wakati Simba itaanzia ugenini jijini Kigali, Rwanda kwa kuikabili Kiyovu Sport ya huko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...