Jamani Wakubwa Zangu,
Poleni na safari.

Naamini kwenye taarifa ya gesi asilia lile kosa la kuiita "gesi asilimia" ni la kibinadamu lakini hili la kusema "katika Tanzania" ni kosa la kisarufi ambalo lilianza kuvuma na Ubalozi wetu wa New York na sasa linashika hatamu. 

Katika sarafu ya Kiswahili hakuna neno linaloweza kutafsiriwa kumaanisha "in Tanzania" kama ambavyo tungependa. Neno la Kiingereza "in" halina neno halisi na moja tu kwenye Kiswahili, ndiyo maana linaweza kutafsiriwa kwa zaidi ya neno moja na pia kwenye miundo mingine linaachwa kabisa.

Sentensi sahihi si: ...kugundua gesi katika Tanzania.
Bali ni: ...kugundua gesi nchini Tanzania.
Au unaweza kusema pia: ...kugundia gesi Tanzania.
Na pia: ...kugundua gesi katika nchi ya Tanzania.

Kiswahili si tafsiri ya Kiingereza bali Kiswahili ni lugha na Kiingereza ni lugha na hazilazimiki kufanana kimiundo na kwa hesabu ya maneno na mpangilio wake.

Neno "katika" huenda na wanachoita Waingereza "common noun" au tuseme nomino ya kawaida, kama nchi, mji, kijiji, n.k.

Sijui nani kaandika lakini umfikishie ujumbe huu. Akipenda somo zaidi nitakuwa tayari, bure bure. Ni sisi ndio wenye Kiswahili na ndio tunaopaswa kukilinda na si Wakenya au Wakongo au Waganda. Kishakufa kwenye vyombo vya habari, lakini tunaweza kukiokoa.

MDAU Mwenye Kukipenda KISWAHILI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Asante mdau..Kugundua gesi katika Tanzania nakubaliana na wewe si Kiswahili sanifu na sentensi haitiririki vizuri mdomoni.

    Na neno gesi si linatokana neno la kiingereza gas au?Neno gas halina Kiswahili chake?

    David V

    ReplyDelete
  2. Mdau David V, ni kweli kuwa hakuna neno la Kiswahili la "gas" kama vile neno hilo si la asili ya Kiingereza. Katika Etymology (Etimolojia: yaani, elimu ya asili ya maneno), tunaona kuwa neno "gas" lilitungwa na mkemia Mbelgiji J. B. van Helmont karne ya 17 akichukua mzizi wa neno hilo kutoka neno la kiyunani/kigiriki "khaos". Mimi mtaalamu wa lugha (linguist) Mwafrika, Mtanzania na mpenzi wa Kiswahili.

    ReplyDelete
  3. 100% confidence levelFebruary 22, 2012

    Asante kwa mchango wako kupitia blogu ya jamii.Lakini nikisoma ujumbe wako kuanzia mwanzo hadi mwisho,kuna makosa ya kisarufi,kumuundo na kimaana kwenye baadhi ya sentensi ulizozitumia.Mathalani,
    1.Mstali wa tano kutoka chini umeandika"sijui nani kaandika........"siyo sahihi,ulipaswa kuandika;Sijamjua ni nani aliyeandika...
    2.Mstali wa nne kutoka chini,umeandika"Ni sisi ndiyo wenye Kiswahili........."siyo sahihi,ulipaswa kuandika;Sisi ndiyo tunaotumia lugha ya Kiswahili...au,sisi ndiyo watumiaji wa lugha ya Kiswahili...ama;sisi ndiyo watumiaji wakubwa wa lugha ya Kiswahili..
    Hitimisho,
    Nakushauri uendelee kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili ili uwe mtaalam zaidi.Baada ya kuwa mtaalam ndiyo unaweza kujinadi kupitia blogu kuwa wewe ni mtaalam.
    Karibu.

    ReplyDelete
  4. Mmmmh mdau na weye; waswahili hunena kuchamba kwingi..... eti katika "SARAFU YA KISWAHILI" teheheheheheheh SARAFU ya Kiswahili. akha, Sheikh SARAFU au SARUFI???

    Miye napita tu.

    Mdau HK

    ReplyDelete
  5. popobawa mzee wa majunguFebruary 22, 2012

    we mwenyewe hujui kiswahili. kwa namna unavyotoa maelezo yako hapa ninapata hofu na weledi wako juu ya Lugha hii adhimu.unaposema "kugundia gesi" unamaana gani?( ingawa ni makosa ya "kiubinadamu" na si kibinadamu).
    kwenye kiswahili sanifu hatutumii maneno kama "naamini" bali "ninaamini". pia kusema "ni sisi ndio wenye" ni matumizi ya lugha za kimakabila na wala si usahihi wa lugha ya kiswahili.
    " kazi ya ualimu ni wito"

    ReplyDelete
  6. Unaposema "ni sisi ndio wenye Kiswahili .... na si Wakenya au Wakongo..." una maana gani. Kwamba asili yake ni Tanzania au vipi. Ushahidi wa kiutaalam, kiisimu na kihistoria unaodhihirisha kwamba asili ya Kiswahili ni pwani ya Kenya, na wala si Tanzania.
    Wabongo tuendelee kujidai tu kwamba Kiswahili ni chetu. Lakini hatuoni wenzetu wanavyopiga hatua kwenye Kiswahili sasa. Tunajidanganya kwa kuamini sisi ndiyo wenye Kiswahili.

    ReplyDelete
  7. Hata hao waandishi wetu wa khabari, utagunduwa hata baadhi yao hata hicho kiswahili hawakifahamu vizuri, 'wanatupopolea' tu hivyo hivyo, mradi upate maana ya khabari waliyoikusudia, lakini ule ufasaha wa 'lafdhi' khasa ya kiswahili unakuta haupo kabisa!

    ReplyDelete
  8. Popobawa,
    Kwenye Kiswahili kuna miundo miwili ya kitenzi cha wakati uliopo unapotumia nafsi ya kwanza ya umoja ambapo unaweza kusema:
    Naamini au Ninaamini. Kwa kutumia Kiingereza hii inalingana na simple present tense na ya pili inalingana na present continous tense.


    Mdau HK,
    SARAFU ni kosa la uchapaji lakini unaweza kuona wazi kuwa ilimaanishwa neno SARUFI. Hilo si kosa la kisarufi.

    Kuna tofauti ya kosa la kuchapa/kuandika herufi, yaani kosa ambalo hukujua wakati linatokea, na kosa la kudhani kwamba unachofanya ni sahihi.


    100% Confidence,
    Ulichofanya siyo kusahihisha lugha, bali kutoa sentensi mbadala zenye maana potofu.

    Mfano mmoja tu:
    Sijui nani kaandika .....na ya kwako: Sijamjua ni nani aliyendika.

    Angalia:
    1. Sijamjua ni kitenzi cha wakati uliopita na kukamilika sasa (perfect tense) ambao humaanisha tukio limeshatokea na kukamilika. Huo haukuwa ujumbe wangu. Ujumbe wangu ni kwamba: HIVI SASA SIMJUI MHUSIKA AMA SIIJUI HIYO DHANA YA "NANI".

    2. Kusema: ...ni nani... ni kuiga Kiingereza cha "who is ..." lakini kwa Kiswahili cha kawaida, hulazimiki kusema "ni" labda tu kama unaweza msisitizo.

    3. Kwa nini usiseme: Simjui na badala yake upendekeze Sijamjua? Ni makosa hii nayo. Jiulize maana ya nyakati katika vitenzi na jinsi zinavyopeleka ujumbe.


    Mdau.

    ReplyDelete
  9. Heri mimi sijasema!!!!

    ReplyDelete
  10. LOL, nimecheka mpaka ha! LOL again.

    ReplyDelete
  11. Ha haaa nichekeshe,nicheke!!!
    Jamani mambo ya lugha tuongee tu lakini tukitaka kuweka umahiri,tutajikuta tunapata Tohara ya ulimi...Matumizi ya lugha yanategemea vitu vingi ikiwa ni pamoja na:- Unaongea wapi,unaongea na nani,na unaongea wakati gani?Achilia mbali hicho unachotaka kukiongelea...
    Kila lugha ina misingi yake.Sasa msingi mmojawapo wa sarufi ya kiswahuli sanifu ni mpangilio wa maneno katika sentensi, ambao unaonyesha utaratibu wa maneno yanayowiana kisarufi.Upatanisho huo wa kisarufi unategemea taratibu za maneno katika fungu moja na taratibu ya viambishi katika mafungutenzi.Kwakua kiswahili kimechukua maneno mengi ya lugha za kibantu na kila mwongeaji ana asili ya lugha yake ya asili hivyo makosa ya hapa na pale tuyategemee sana.Tuweke bidii tu ya kujielimisha zaidi,vinginevyo yakikushinda kabisa basi kula ugali wako ukalale....

    ReplyDelete
  12. 500 BC ndio mchina alijua jinsi ya kutumia hiyo hewa inayotoka ardhini sababu nchi nyingine walishindwa kujua chanzo sababu ilikuwa inawaka hewani na kuwashangaza kitu gani hawakioni !na haina kiswahili sababu ziko haina nyingi sana sana za gas,natumaini kandoro angetutatulia jambo hili !

    ReplyDelete
  13. Hii tungo "kugundua gesi katika Tanzania" imekamilika na inaonesha kitendo cha ugunzi bado ni endelevu.
    Matumizi ya neno "katika" bado ni sahii na yanakubalika katika kiswahili!!! katika ni kivumishi cha mahali na pia tunajua kuwa jina likiwekewa kiambishi tamati"ni"mwishoni linageuka kuwa kikivumishi cha mahali mfano kabatini(katika kabati)chumbani(katika chumba), kwahiyo unaposema"kugundua gesi nchini Tanzania" na mwingine akasema" kugundua gesi katika Tanzania" ni kitu kilekile kimoja. Mnapokipenda kiswahili basi ni bora kuijua na Isimu yake!! siyo kusikia mtiririko wa maneno katika ulimi tu

    ReplyDelete
  14. Mdau ahsante kwa kulianzisha, wacha tujifunze kutoka kwa wabobeaji wa lugha

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...