SERIKALI MKOANI RUVUMA IMESIKITISHWA NA TUKIO LA MAANDAMANO YA VIJANA YASIYO HALALI

Serikali imesikitishwa na tukio la kundi la Vijana waendesha pikipiki maarufu kama yebo yebo kufanya maandamano katika Mitaa ya Manispaa ya Songea na kusababisha vurugu kubwa na uhalibifu wa mali.

Akitoa tamko hilo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameeleza kuwa kwa muda wa siku tatu zilizopita kumekuwepo na tetesi za kutokea mauaji kwa imani za kishirikina zenye kulenga zaidi akinamama kuondoa sehemu za mwili kuwasaidia mambo ya kibiashara hivyo kupelekea watu kufariki.

Kufuatia matukio hayo mkoa uliagiza Jeshi la polisi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa wanaojihusisha na mauaji hayo kazi inayoendelea hadi sasa. Katika maandamano ya leo watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wakiwarushia mawe polisi wa kutuliza ghasia.

Aidha Mkuu wa mkoa amewasihi wananchi wa Songea na Ruvuma kwa pamoja wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu  ili vyombo vya ulinzi na Usalama viendelee kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wote wanaojihusisha  na biashara hii haramu wanachukuliwa hatua za kisheria.

  Ametoa wito wananchi kuwabaini watu wanaondesha uhalifu kwa njia ya uchawi na ushirikina na ambao wanaishi katika Mitaa yetu kwa kutoa taarifa zao kwa viongozi wa Mitaa na vyombo vya ulinzi na Usalama mapema.

“Serikali haimini kuhusu ushirikina wala uchawi.Inaelewa kuhusu tiba asilia na kwa tiba hizi hufanywa na watu wanaopewa vibali na serikali” alisema na kusisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma wakatae ushirikina wa kiwango hicho pia uendeshaji wa ramli chonganishi zenye lengo la kugombanisha ndugu,jamii na Taifa kwani madhara yake ni kutokea mauaji kama haya kwa wasio na hatia.

Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Ruvuma kutoa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na Usalama katika kipindi hiki kwa kuwabaini wote wanaojihusisha na kuendeleza uhalifu huu kwa vigezo vya uchawi na ushirikiana.

Amewaagiza watendaji wa Mitaa,kata na Tarafa kuhakikisha ulinzi kwa kushirikiana na Polisi wanaoendesha operesheni hiyo katika Mitaa yote na nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wahalifu wote huku hatua za kisheria zikichua  mkondo.

“Sote tukiungana hawa wachawi,waganga wa jadi na majambazi wanaodandia humo tunaweza kuwadhibiti ili mauaji yakome na Songea irudie utulivu wake kama kawaida” alisema Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi jumla ya watu watano hadi sasa wameripotiwa kuuwawa kwa hisia za ushirikina na uchawi katika maeneo ya Lizaboni, Bombambili na Matarawe kati yao wanawake watatu na wanaume wawili.Hata hivyo kati yao hakuna hata mmoja aliyeondolewa kiungo cha mwili kama wanavyodia baadhi ya wananchi waliondamana.

Imetolewa na
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
22 Februari 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. polisi wafanyie kazi kwa haraka madai ya wananchi. hata km serikali haiamini uchawi inatakiwa kutochukulia mambo hayo kwa mzaha. talk to ward leaders, mara nyingi wanajua masuala haya katika wards zao.

    ReplyDelete
  2. Sasa muheshimiwa inakuwaje askari kutumia risasi na kusababisha vifo???Tunajua kama serikali haijakubali hayo maandamano kwanini msiwe na utaratibu mwingine wa kutatua haya mambo bila ya maafa??

    ReplyDelete
  3. kwaio shoot to kill bongo imeruhusiwa si ndio? Au ndo askari wao wako juu ya sheria? Inasikitisha sana kuona jeshi la polisi lisivyothamini maisha ya mtanzania asiyekua na cheo cha mheshimiwa. Napenda kuwakumbusha askari wanao tulindia amani kwamba wao ni kioo cha jamii. Ikumbukwe kwamba "with great powers come great responsibilities.." Ehh Mungu ibariki Tanzania yetu. Leo ni siku nyingine ya maombolezo.

    ReplyDelete
  4. Halali maana yake nini? Viongozi mnapopeleka nchi hii ni pabaya sana sana na haivumiki tena!!!!!

    ReplyDelete
  5. Ndio muue? nani katoa hiyo ruhusa? hao vijana mbona hawakuwa na silaha yoyote mbali na silaha ya moto?

    ReplyDelete
  6. Mheshimiwa unaposema imeripotiwa watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi... unajisikiaje?? na hatua gani unachukua hao askari wenu waliofanya hivyo? Inamaanaa maabomu ya machozi yalishindikana kabisaaaa hata kutumia risasi za moto? inasikitisha sana. Songea si mji kama Dar ambao unaweza kuwashinda kutumia vifaa ambavyo visingeweza kusababisha vifo vya watu hao. Uongozi muangalie kwa undani zaidi. Hapo walioathirika ni wale wenye kipato cha chini na si wenye uwezo, ni wale wanaohitaji msaada wenu zaidi kama serikali. risasi za moto?? Songea? Haingii akilini... Tutafika kweli?? Eeeh Mwenyezi mungu tusaidie wanyonge wa nchi hii.

    ReplyDelete
  7. Mpaka itakopofika siku serikali ikatatua shida za watu kwa wakati, mambo kama haya hatutarajii yatakwaisha yenyewe. Siku zote ukisikia Jamabazi ameuwawa na wananchi wenye hasira, maana yake wananchi hawana tena imani na jeshi la polisi hivyo kuamua kuchukua hatua stahikim wao wenyewe, ingawa mara kwa mara hatua hizo huwakuta wasiohusika

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...