Na  Mwandishi Maalum

New York

Mwana-Diplomasia mkongwe na mzoefu katika tasnia ya  Uhusiano wa Kimataifa, Bw. Jan Eliasson  raia wa Sweden  (pichani) ndiye atakayeshika    wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  ametangaza uteuzi wa Bw. Eliasson mbele ya waandishi wa  habari mwishoni wa wiki, ambapo amesema Msweden huyo   anayechukua nafasi itakayoachwa na Naibu Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Asha- Rose Migiro ataanza majukumu yake  Julai Mosi  mwaka huu.

  Naibu Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Asha-Rose Migiro  ataendelea kuwapo hadi June mwaka huu ili pamoja na mambo mengine kusimamia kipindi cha mpito na maandalizi ya Mkutano wa kimataifa kuhusu Maendeleo  Endelevu maarufu kama RIO+20 mkutano huu utafanyika mwezi June huko Rio de Janeiro nchini Brazil.

Kabla ya uteuzi wake, Bw. Jan Eliasson ambaye  si mgeni katika  Umoja wa Mataifa , amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za  Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu   kuhusu Darfur, amewahi  pia kuwa Rais wa Baraza kuu la 60 la Umoja wa mataifa,  na amewahi pia kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu  kuhusu Haki za Binadamu.

Kwa sasa Bw. Eliasson  anasimamia  utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) 

Aidha  Bw. Jan Eliasson  utumishi wa serikali yake     amewahi pia kuwa  Balozi aliyeiwakilisha nchi yake ( Sweden ) nchini Marekani,  na New York, na amewahi pia   kuwa Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje   na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden.

Pamoja na  kumtangaza  Bw. Eliasson kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya, Ban Ki Moon pia  amemtangaza  Bi. Susana Malcorra raia wa Argentina kuwa  Msimamizi Mkuu mpya wa Ofisi yake.

Kabla ya uteuzi huu Bi Malcorra alikuwa akiongoza  Idara  inayohusika na  usambazaji wa vifaa  na  misaada  katika  Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa  Mataifa. Anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bw, Vijay Nambiar ambaye anakuwa  Mshauri  Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu  Myanmar.

Aidha katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Ban Ki Moon amebainisha kwamba uteuzi wa  maafisa wengine wa ngazi za juu na ambao  mchakato wake umekwisha kuanza watatangazwa  baada ya taratibu za kuwapata kukamilika.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...