Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imepokea taarifa kupitia matangazo yanayotolewa na chuo kinachojiita “Japan Bible Institute Graduate School of Theology” kikijitangaza kwamba kinatoa shahada mbalimbali za uzamivu (PhD) kwenye nyanja za dini na jamii.  Chuo hiki kinajitangaza kwamba kinawakilisha tawi la taasisi iliyopo nchini Marekani na kwamba makao yake makuu kwa bara la Afrika yapo Dar es Salaam, pamoja na kwamba eneo halisi ofisi zao zilipo haijaelezwa kwenye matangazo yao.

Tume inachukua fursa hii kuuarifu umma kwamba chuo hiki hakitambuliki kwa mujibu wa sheria na kwamba wamiliki wa Japan Bible Institute Graduate School of Theology hawana kibali cha kutoa elimu ya chuo kikuu ambayo inatambuliwa hapa nchini. Tume inatoa tahadhari kwa umma kuepuka ulaghai ambao unafanywa na watu katika eneo hili la elimu ya juu na hivyo umma unashauriwa kuchukua tahadhari kwani vyeti watakavyotolewa havitambuliwi na Tume na hivyo haviwezi kutumika hapa nchini.

Pia, wamiliki wa chuo hiki na wawakilishi wake waliopo Tanzania wanapewa onyo kuacha mara moja kutoa matangazo ya shahada za aina hiyo hapa nchini bila kufuata taratibu. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye kwenda kinyume na tangazo hili.

Aidha, Tume inapenda kuwaarifu watu wote wenye lengo la kuanzisha vyuo vikuu nchini au kutoa programu za vyuo vikuu wawasiliane na Tume ili kupata maelekezo juu ya taratibu zinazotakiwa kufuatwa. Pia umma unasahauriwa kutoa taarifa kwa Tume ama vyombo vingine vya dola pale ambapo wana wasiwasi na uhali wa programu ama tuzo inayotangazwa au kutolewa na taasisi yoyote bila kufuata taratibu.

Imetolewa na:
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
S.L.P. 6562
DAR ES SALAAM

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. dini hapa ni kivuli cha ulaji, wameelewa somo la wakoloni. nao pia dini ilikuwa ulaji, ila sisi imetudaka vizuri.

    ReplyDelete
  2. PHD za akila Dr. Slaa

    ReplyDelete
  3. Hii yote ni Njia ya Mkatao ambayo Wanasiasa wengi Dunia nzima hupendelea sana mipango ya namna hii ili kufikia Malengo ya viwango vya Elimu kwa njia fupi.

    Daima Mwanasiasa Duniani ni mtu mpenda kufikia malengo kwa njia ya mkato!

    ReplyDelete
  4. Upigaji umezidi sana Bongo, kila kukicha na mabunduki mapya ya kiusanii.

    Mamlaka zimelala usingizi wa kukoroma.

    Ohhh yetu macho!

    ReplyDelete
  5. Marekani wanahangaika kusambaza uongo kwa aina yeyote ile. Hapa Afrika wanajua wala hamjui kudhibiti utitiri wa makanisa na vyuo vinavyoibuka kila kukicha. Vichochoro hivyo ndivyo vinavyotumiwa kuparaganya amani ya nchi. Watanzania wenye uchu wa elimu wanaingia kichwa kichwa.

    ReplyDelete
  6. Hili ni tatizo kubwa nchini watu kubeba shahada feki na wakapewa misifa.

    Tume ya Vyuo vikuu ianze pia kuwashughulikia wale waliotajwa na kufahamika kuwa wana PhD za kubumba tunawafahamunhata wakijinyamazia leo. Ipo siku atakuja mtawala asiyeangilia nyani usoni mtaumbuka kwa kutakiwa kulipa fedha na hadhi yote mliyopewa ambayo hamkustahili kwa ajili ya kuonyesha vyeti feki!!!

    Wachungaji na Maaskofu kuweni macho msiingie mkenge na hicho chuo cha Uongo na kweli wala msisogee katika mahafali yake!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...