Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mh. Joseph Simbakalia akihutubia wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mjini Mtwara leo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia akitoa maelekezo kwa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo.
Wadau wa mkutano huo wakifuatilia mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akigaua fomu zinazojazwa katika Hospitali ya Ndanda kwa wanachama wa Mfuko huo wakati alipotembelea.
Mkurugenzi Mkuu, Emanuel Humba akiwa na wakurugenzi wake wakihakikisha uhalali wa vitambulisho vya wanachama katika Hospitali ya Ndanda mkoani Mtwara.
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Mh. Joseph Simbakalia amesema kuwa uendelevu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii unategemea usimamizi wa viongozi serikalini hivyo akawataka viongozi wa Halmashauri mkoani humo kubuni mipango ya kuhakikisha mifuko hiyo inaimarika.
Amesema kuwa Mifuko hiyo ni ya muhimu kwa afya za Watanzania hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatimiza wajibu wake hasa kwa kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko hiyo lakini pia kusimamia huduma katika vituo vya kutolea matibabu ili ziwe bora.
Simbakalia aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa NHIF uliokutanisha wanachama, watoa huduma, viongozi wa kiserikali, madhehebu ya dini, viongozi wa kisiasa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi.
"Ndugu zangu wanasiasa, viongozi wa dini hili suala la afya ni letu sote hivyo tuzungumzeni kwa maslahi ya mwelekeo mmoja ili hatimaye Watanzania waweze kuwa na bima za afya," alisema Mh. Simbakalia.
Alisema kuwa gharama za matibabu zimekuwa ni ngumu kuzimudu kutokana na upandaji halali hivyo njia pekee ya kuwakomboa wananchi ni kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii hivyo akawataka wadau hao kujadili na kuona ni namna gani itawezesha suala hilo.
"Kuna haja sasa ya kuwepo kwa sheria ili uchangiaji wa Mfuko huu uwe wa lazima, wenzetu wa nchi jirani kama Rwanda wamefanikiwa sana na wakati tukiliangalia hili ni vyema pia tukaweka mikakati ya kuboresha huduma zetu ili wananchi waone umuhimu wake," alisema Mh Simbakalia.
Aidha alitumia mwanya huo kuwataka watoa huduma mkoani humo kutumia lugha nzuri kwa wanachama wa Mifuko hiyo wakati wanapokwenda kupata matibabu kwa kuwa huduma hiyo wameilipia.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa Uongozi wa Mkoa huo utaendelea kutoa ushirikiano kwa Mfuko huo lakini pia kuzifuatilia Halmashauri katika utendaji wake hasa suala la uhamasishaji kwa wananchi na matumizi sahihi ya fedha zitokanazo na Mfuko huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alilisitiza umuhimu wa matumizi ya fedha zitokanazo na Mfuko ambapo alisema kuwa endapo zikitumika vyema zitaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la ukosefu wa dawa.
Alisema kuwa lengo la Mfuko ni kuzisadia Hospitali au Vituo vya kutolea matibabu vya serikali kuboresha huduma zake lakini imekuwa kinyume chake kwa kuwa vituo vya binafsi ndivyo vimekuwa vikipata mapato makubwa kutokana na kutoa huduma bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...