Steven Kanumba akiwa ofisini kwa Ankal alikokuwa
akimtembelea mara kwa mara

Si kawaida yangu kuwaingilia wadau watukufu katika ukurasa huu na kuanza kumwaga mistari kama sina akili nzuri, isipokuwa labda likitokea jambo kubwa ama kama kuna jambo la msingi au  tangazo muhimu. 

 Ankal akiwa na Frank Eyembe wa Urban Pulse huko Reading, Uingereza,  wakati akimalizia kutengeza filamu ya 'Lovely Gamble' ya Steve kanumba aliyocheze jijini London
 Ankal akiwa na Steve na DJ Bonny Luv ndani ya Thai Village jijini Dar. Kama alivyo Ankal STEVE alikuwa hanywigi wala havutigi. Alikuwa CLEAN
Ankal akiwa na Steve Kanumba na John Mashaka katika hafla ya Tanzania Mitindo House Hellenic Club jijini Dar

Kifo cha rafiki yangu Steven Charles Kanumba si jambo dogo.

Naandika nikiwa na huzuni moyoni, nikiwa siamini kwamba rafiki yangu wa karibu ambaye tulikuwa tunashauriana mambo mengi, hususan ya kutumia mitandao ya jamii (naona fahari kusema nilimshawishi, naye alikubali, kuanzisha blog yake mwenyewe miaka 4 iliyopita  BOFYA HAPA) kwa manufaa yake binafsi na wapenzi wake lukuki ndani na nje ya Tanzania.

Usishangae kuwa nimechukua muda mrefu kabla ya kuandika haya kwani hata bado siamini kwamba sintopata tena simu ya Steve akiniuliza haya na yale, kubwa likiwa: “Umeangalia blogu yangu leo? Aisee picha zinanisumbua, haziwi kubwa kama zako – nifanyeje??” Au saa ingine, usiku wa manane, ananipigia na kuniuliza “Kaka lini ntapata nafasi ya kuonana na Mzee (JK). Nataka niwawakilishe wenzangu kumuomba atupe tafu katika tasnia ya filamu – we si unacheki uhuru wa kuwa wajasiriamali anaotusisitiza vijana tunavyoutekeleza kwa vitendo??”

Ni kweli kwamba mtu anapotutoka tunakuwa na maneno mengi mema juu yake, lakini si uwongo kwamba haya niyaandikayo hayako katika tafsiri hiyo. Ni ya kweli na yanatoka ndani ya kilindi cha moyo wangu unaougulia hivi sasa; Steve alikuwa mcheshi, asiyependa ubishoo japo ni nyota katika jamii, na mdhalilifu mno unapoongea naye kiasi cha kukufanya ujisikie vibaya kana kwamba unamwonea vile. Najua wengi hamkujua kwamba Steve alikuwa mtu wa aibu sana awapo ‘uraiani’ au  mbali na lensi ya kamera. Kama hamjazoeana alikuwa hajui aseme nini mbele yako.

Hilo nalijua kwa sababu nilipokutana naye kwa mara ya kwanza miaka 7 iliyopita, tukiwa katika saluni ya Bitebo Hair Designer pale Magomeni Mapipa ‘Lango la jiji’ jijini Dar, alipata kigugumizi nilipothubutu kumsemesha wakati tukinyolewa nywele tukiwa tumeketi juu ya viti jirani. Kumbe yeye pia alikuwa amesikia jina langu toka zamani sana na kazi zangu alikuwa anazitambua kama ambavyo mimi nilikuwa nazihusudu za  kwake yeye, ambapo kila mmoja alikuwa anamhusudu mwenzie kwa kazi zake kimya kimya. Baada ya kumaliza kunyolewa hapo hapo  tulipinga  kuwa marafiki kwa kubadilishana namba za simu. Kuanzia siku hiyo niliweza kuona upande wa pili wa Steve kirahisi mno, kwamba pamoja na ustaa wake, ndani na chini kabisa alikuwa mtu wa kawaida sana sana. Huwezi amini!

Steve hakuwa mpenda umaarufu wa kirahisi (cheap publicity) na amini usiamini pamoja na urafiki wetu wa karibu, hakuwahi kunikubalia kufanya naye mahojiano ili nimnadi kwa mashabiki wake, akidai kila mara kwamba neno  la mdomo (word of mouth) kwake linatosha.  Hata kuandikwa kwake kila mara katika magazeti, hasa ya udaku, hakuwahi kuhojiwa ana kwa ana. Stori nyingi, alinihakikishia, zilikuwa  za kutungwa.  Naye hakujali akisema kila mara kwamba MUNGU ndiye mwelewa wa yote.

Nilishangaa mwaka 2009, mara tu aliporejea toka Afrika ya Kusini kwenye Big Brother House, alikoalikwa kama mmoja wa nyota wanne wa  filamu wa Afrika, alipokubali nimhoji. Siku hiyo (angalia video hapo chini) kulikuwa na bonanza la michezo, nakumbuka, katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe jijini Dar es salaam. Natumai mahojiano hayo mdau mpendwa umeyaona na kuyasikiliza. Hakika yanatia huzuni, ikizingatiwa kwamba alikuwa akilalamikia Watanzania wenzake ambao wengine walitengeneza hata matangazo ya redio na SMS kibao za kumponda kwa kutoongea kiingereza kwa ufasaha, wakati ukweli ni kwamba Steve alikuwa na uwezo mkubwa kutema ‘yai’ kuliko pengine hata hao waliokuwa wakimponda.

Naandika haya nikikukumbuka neno lake  la mwisho katika mahojiano hayo, aliposisitiza haja ya Watanzania kupendana na kutiana moyo pale mwenzetu akiwa amefanya vyema, jambo ambalo kwa kweli limeota mizizi miongoni mwetu kiasi cha kutia kinyaa. Yaani baadhi ya Watanzania wako kama ‘Nyoka wa Mndimu’, yaani nyoka huyo aliye juu ya mti wa ndimu hataki mtu achume ndimu japo kuwa yeye hazili. Kwa lugha nyepesi ROHO YA KOROSHO ama ROHO MBAYA bila sababu ya msingi.

Japo nalia kwa uchungu, lakini nina furaha ya kusherehekea maisha ya rafiki yangu mpendwa Steve, ambaye mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa juzi, baada ya kurusha youtube ya mahojiano yetu, akisema “Aisee, siamini kwamba ni mimi yule, nilikuwa naongea utadhani pastor!  Yaani safari hii ndio nimeifaidi hiyo video – bila shaka Watanzania watakuwa wamepata ujumbe na kuamua kuanza kupendana”.

Naweza kujaza kurasa mia za Globu ya Jamii lakini nisiwe nimeeleza robo tu ya sifa za Steve. Naomba nimalizie hapa kwa kuomba Watanzania popote mlipo duniani mkiisoma Globu ya Jamii, tujipeleleze, tujiulize na tuchukue hatua ya kuanza KUPENDANA. Kanumba amefariki dunia akiwa anatupenda, kuna ugumu gani na sie tusherehekee maisha yake kwa KUPENDANA??
Kaka Steve Kwa heri ya kuonana.  Hupo nasi kimwili lakini tutakuwa nawe Kiroho milele. Mwisho kabisa naomba nikubalie nisikuite Marehemu ama Hayati Steven Charles Kanumba.

Acha tu niendelee kukuita STEVE. 

-MUHIDIN ISSA MICHUZI





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 37 mpaka sasa

  1. KAKA MICHUZI NIMEFURAHI MWENYEZIMUNGU AWEKE MAHALI PEMA PEPONI MWILI WA KANUMBA INSHALLAH NA ROHO YANGU IMEFURAHI KWANI SIKU ULIVYOWEKA VIDEO ILE JUZI NILIKUWA MIONGONI NILIOFURAHIKIWA NA COMMENT YAKE YA MWISHO KUHUSU KUPENDANA NA NIKAWACHA COMMENT. TUENDELEE KUPENDANA KWANI WENGI WETU SIKU HIZI HATA HIYO MIAKA 40 INAKUWA NGUMU KUFIKA CHUKI ZA NINI? MZ

    ReplyDelete
  2. nimeumia sana kanumba kututoka. kweli watanzania TUPENDANE tuwe na umoja tushikamane kwa hali na mali,kwa kuwa sote ni wamoja wa taifa moja. kanumba tutakukumbuka sana.Tulikupenda sana ila Mungu baba kakupenda zaidi ipo siku tutaonana.

    ReplyDelete
  3. Umekua nikama vile mshumaa uliowashwa kwenye chumba kisicho na upepo baada ya madirisha yake kufungwa, mara ghafla madirisha yanafunguka kwa kimbunga kilichopita kwa kasi nje, kimbunga ambacho kimepelekea kuzima mshumaa uliokuwepo ndani,
    Yatasemwa mengi ila ukwel utabaki kuwa Kanumba hatuko nae kimwili, ijapokua naamin roho yake itadumu nasi mpaka tutakapotwaliwa nasi na kwenda kukutana tena huko aliko tangulia.
    Pumzika kwa amani KANUMBA.

    ReplyDelete
  4. stivie-u.sApril 07, 2012

    Good words Ankal.

    ReplyDelete
  5. Yani jana tu ndo nilipata nafasi ya kuangalia ile video ya mahojiano na kwa kweli nilihuzunika sana nikajisikia vibaya hasa nikikumbuka zile message za kumkashfu, Then asubuhi nasikia hatunaye tena kwa kweli sikuamini kabisa and i still cant beleive... kwa kweli watanzania wenzangu tunahitaji kupendana na si kukatishana tamaa.

    ReplyDelete
  6. Issa Michuzi (Ankal) umeandika mambo mazito sana ukitumia maneno machache. Umetumia lugha fasaha ya Kiswahili.Umeongelea mambo muhimu kwetu Wanadamu kama : urafiki,huzuni, kumbukumbu("legacy") mapenzi na mahusiano ya karibu. Hukupoteza muda kuongelea kipaji au sanaa au utamaduni- umezungumzia mambo ya msingi sana- ambayo marehem Steve Kanumba na umaana wa maisha yake mafupi yametuachia utajiri.

    ReplyDelete
  7. Issa "Ankal" Michuzi umetukumbusha mambo mazito ya msingi kwa kutumia maneno machache. Ukatumia lugha fasaha ya Kiswahili, ukaturudisha ndani ya "boma" la hisia za huzuni, urafiki, mahusiano ya karibu na kupendana wanadamu. Ukaturejesha ndani ya umaana wake Steve Kanumba- kama mwanadamu na Mtanzania aliyezingatia kupeana moyo na kusifiana pale mwenzako anapotenda zuri. Ahsante kwa ukweli na mafunzo...

    ReplyDelete
  8. I am still in Shock! This is very sad news. Kanumba was a very talented young Man, one of the best Actors in Africa. I was so previledged to work with him on Lovely Gamble Movie when he came to UK back in 2009. He was such a funny and humble guy.
    Kanumba, you will forever be missed by many and may the lord rest his soul in Peace
    Susan Mzee

    ReplyDelete
  9. pole kaka michuzi kwakumpoteza rafiki yako mpendwa yaani mimi hapa mpaka sasa hivi ni kama naota tu sijuii hata niseme nini bali tu NISEME MUNGU AMETOA NA MUNGU AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE AMINA

    ReplyDelete
  10. Jamani msinilize zaidi ya hapa ninavyolia. Kaka Freddy Macha (ambaye bila mdogo wako Ndesanjo Macha kunitambulisha mambo ya Libeneke kule Helsinki Septemba 8, 2005 nisingekuwa hapa) nashukuru sana kwa kauli yako. Najua wewe na wadau wengi wengine mtashangaa naiba ukurasa wenu wa maoni; kifo cha STEVE kimenigusa mno. Katika maisha yangu nimeguswa hivi mara mbili, na hii ni ya tatu. Kwanza Baba yangu (Mola amrehemu) alipoaga dunia. Pili ni siku Mama yangu (Muumba mpe raha ya milele) miaka kibao ilopota. Tatu ni hii ya kuondokewa na STEVE. Sijabahatika kujuana naye kwa muda mrefu (miaka saba tu)lakini maono yetu (ideals) yalikuwa mamoja. KUPENDA Watanzania na kujipennda kama WATANZANIA. Nimeamua kupigania hili hadi kieleweke ili kumuenzi rafiki yangu STEVE.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amen kaka, Mungu atusaidie tupendane watanzania. Mungu ampe nafasi njema ameni

      Delete
  11. kaka michuzi umeniliza tena kwa sababu neno MPENDANE ndilo neno la mwisho aliloniachia marehemu baba yangu.R I P Kanumba kweli watu tupendane

    ReplyDelete
  12. Michuzi pole sana kwa kumpoteza rafiki. Ni pigo kwa jamii nzima kuona kijana aliyekuwa na ubunifu kama huo anaondoka akiwa bado mdogo hivyo. Pia nikupongeze kwa kumlilia kwa staili ya kusherehekea maisha yake kama ulivyomfahamu. ndugu yetu SK RIP.
    Sasa hoja KUPENDANA. Nieleze maoni yangu kwa kifupi: kupendana ni utamaduni na ni utamaduni mzuri. Lakini utamaduni haudondoki kama mvua bali unatengenezwa. Unatengenezwa na sera za kiuchumi na kijamii. Ikitokea sera hizo zikawa zinapendelea kundi moja au baadhi ya makundi na kuyasukumiza mengine pembezoni (yaani hakuna fairness), basi matokeo yake ni wanajamii kuanza kuchukiana. Kwa maoni yangu hiki ndicho chanzo kikuu cha Watanzania kuwa na hii hali ya ROHO YA KOROSHO na tunakoelekea utamaduni huu utaota mizizi.

    ReplyDelete
  13. Ankal pole sana kwa kumpoteza rafiki yako, I can tell by what you wrote the pain that you have is unbearable. M'Mungu akupe nguvu pamoja na familia na marafiki wote wa Kanumba. Poleni watanzania wenzangu popote mlipo

    ReplyDelete
  14. Watanzania tumepoteza nyota wetu.Yaani niliposoma hii habari nilikuwa km nimechanganyikiwa nisijue Kanumba ni nani na kujaribu kutaka kutoa jina kwa mtu mwingine.Yaani nilikuwa sikubaliani na ukweli ninaouona mbele ya kioo.Kapumzike kwa amani kaka Kanumba

    ReplyDelete
  15. Watanzania wenzangu, ni kweli kabisa upendo kati yetu sisi haupo, mara nyingi upendo NI wa kinafiki sio wa ndani ya miyoyo yetu. Kwa nini umchukie mtu bila sababu? Usichukie maendeleo ya mwenzako bali fanya bidii nawe utafanikiwa. Bila upendo hatufiki mbali, tupendane, tuwe na uzalendo, mpende mtanzania mwenzako na msaidie kutoka na utajiwekea hazina mbinguni. TUWE WAZALENDO tumwenzi KANUMBA & baba wa Taifa hili. Michuzi tunakushukuru kwaku tupa updates za mara kwa mara kuhusiana na huu msiba mzito.

    ReplyDelete
  16. Binafsi simfahamu na sijawahi kuona movie yake kwani toka nihamie USA ni miaka 13 sasa, ila nilitegemea nikija nyumbani TZ mwakani ningepata kuona movie zake. Inasikitisha sana maisha ya kijana mdogo namna hiyo kupotea kirahisi, imenisikitisha sana kuona nyota iliyokuwa ikiwaka kuzimika ghafla, MUNGU ampe pumziko la milele.

    ReplyDelete
  17. Michuzi ngoja nami nieleze mazuri uliyonayo wakati bado unaishi. Unayo mengi mazuri na mimi binafsi umenisaidia sana kimawazo na hata kiuchumi, hasa wakati wa mkutano wa Sullivan pale Arusha miaka mitano iliyopita. Mwaka jana mwishoni tukiwa Kampala ukanipiga tafu bila hata kukuomba. nilishangaa sana kwa kweli. Naomba na wewe Mungu akibariki. Unapenda sana kushangilia mafanikio ya watu wengi na una wivu wa maendeleo. Nakuombea Mungu akuzidishie kwani duniani hapa ni kupendana tuu kama alivyosema Kanumba. Japhet Sanga rafiki yako mkuu ataniunga mkono kwa hili. Nadhani umeshamgundua anayeandika ujumbe huu. Usimwage jina langu pliiiz

    ReplyDelete
  18. Nawe pia Muhidini Michuzi, Mungu aendelee kukubariki na kukuongoza siku zote.

    ReplyDelete
  19. Well said. RIP STEVE

    ReplyDelete
  20. Hivi Ankal Nikikuuliza Swali? Utaweza Nijibu? Ni kitu Gani kilifunya Ile Juzi upost hii Video ya Steve Kanumba kwa Blog yako? This video Itawafungua wengi sana, Nakuambia Hata Kama Kanumba Angekuwa Hajafa hii Video ingewabadilisha wengi sana kuhusu Kanumba,Ujue mimi Binafsi nilikuwa siijawahi hata Siku mmoja sikia interview yake au akiongea tu...Hapa aliongea Sense mno alijielezea yeye kama yeye ambavyo alikwanza na Sisi watanzania wenzake,Wish kama hii video ungepost siku zile zile. Huyu jamaa wala simsifii sababu amekufa au lah,Nasema toka moyoni mwangu kuwa He wa the GREAT kwa kweli.Mimi ni mmoja ktk wale ambao tulikuwa na image tofauti ya Kanumba,Lakini Juzi after angalia hii video nilibadilika kabida na nikamwambia mke wangu kwamba laiti ningekuwa na email/simu ya Kanumba ningempigia na kuongea nae,Inshort nilikuwa nafikiria kumtafuta siku mmoja niongee nae nimpe some ideas ili ajiendeleze zaidi. Rest In Internat Peace My Brother S.K, Maneno ulioyasema kwa Video hii ni Mazito sana nitayafanyia Kazi. Your still the Great!. Love YOU.

    ReplyDelete
  21. mungu wetu ndie anyejua miaka ya kuishi kwa kila binadamu ktk dunia hii sku ikifika hata maji ya kunywa huwezi kuomba kama kwa ndg yetu kanumba! bnadam anapana na mwenyezi mungu naye anapanga pia lakin maamuzi mungu ndiye pekeee naweza kutoa sisi tunabaki watekelezajiu wa yale anayoyatoa mwenyezi mungu na kawaida hakosolewi wala kusahihishwa kwa liwalo lolote! tulimpenda sana kanumba lakini mungu yeye alimpenda zaidi yetu kilichobaki tumuombeee maisha yenye baraka na rehema juu mbinguni kwani wote tunaelekea huko siku ya mwisho ikifka soote tuje kumkuta mahali patakatifu!!! mungu alitoa na ametwaaa pia jina lake lihimidiwe ameeeen!!!

    ReplyDelete
  22. Pole sana ankal. May his soul R.I.P

    ReplyDelete
  23. Kwa kweli i just woke up n open My iPhone direct to blog ya jamii! I was so touched with u ankal michuzi!! U are à man of truth! À very good man With good words from the heart!!!

    ReplyDelete
  24. ankal unazidi kutuliza wengi,umeongea maneno yenye busara na kwa uchungu mkubwa sana..na siku zote tutamkumbuka rafiki yako kwa neno "tupendane"siku zote kanumba alisisitiza hilo,so hard t take ila namuombea kheri aliko,sisi ni binadamu tunakosa ila naomba Mungu akamrehemu sawa sawa na fadhili zake,asimuhukumu kwa makosa ya ujana wake ila akamkumbuke kwa fadhili na wema wake,Amen

    ReplyDelete
  25. Mdau Sun Apr 08, 02:18:00 AM 2012

    Kuna uhusiano gani kuhamia kwako marekani na kutoangalia movie za kiswahili kutoka tanzania?

    wenzako tunafaidi movie za nyumbani popote duniani

    kwani ulikosa watu wa kukutumia dvd?

    kuangalia movie za kiswahili haihitaji mpaka urudi nyumbani kama ulivyosema wacha mambo ya kitumwa

    rest is peace kanumba tutakukumbuka sana katika mchango wako kwa taifa tasnia ya uigizaji.

    ReplyDelete
  26. Watanzania wa nje nasi tupendane jamani, Kanumba katuachia upendo, nasi tuuendeleze TUPENDANE ukiona mwenzio kakwama kama kuna huwezo msaidie kuliko kusubiri uone anaanguka tupendane tupendane na hiyo ndiyo ilikuwa Tanzania ya Nyerer tanzania ya upendo, watu wote sawa, hatuuulizani kabila wala dini, laini siku hizi sijui tunaelekea wapi. Michuzi hata mimi kifo cha huyu kijana kimenigusa sana, haswa hawsa kwenye kumrudia Mola, kila wakati ni saa, dunia ni mapito, tujitengenezee makazi mema tuendako.

    ReplyDelete
  27. Pole sana Ankal kwa kweli maneno umeongea leo yametuliza wengi japokuwa wengi wao naamini wanamjua Kanumba kupitia cinema zake, watoto wanamlilia Kanumba jamani hili ni pengo kubwa sana. Mimi leo nimepitia blogs nyingi za Afrika na nimeona jinsi wenzetu wako pamoja nasi katika kuombeleza kifo cha Kanumba tena wanamuita "MOVIE STAR" jamani watanzania TUPENDANE ndio jambo kubwa mimi nakuunga mkono Ankal kwa kampni yako ya watanzania tupendane! tutongea mengi sana kuhusiana na kifo cha Kanumba lakini Kanumba yuko mbele ya haki tumuombe dua Mwenyezi Mungu amfutie madhambi yake aliyoyatenda akiwa hai duniani yeye kama binadamu ana kasoro, tena naamini sisi watanzania tukiuungana kwa pamoja kumuombea Kanumba Mwenyezi Mungu atatusikia!!! Rest in Peace Kanumba!

    ReplyDelete
  28. Rest in Peace Kanumba, sikujui na wala si mpenzi wa sinema za bongo lakini umenigusa vibaya sana sana, Mungu ndie mjua wa yote ni kwanini amekuita na kwa nini kwa njia ile.
    Ndugu zangu naombeni pia tumuombee yule aliyesababisha kifo cha mpendwa wetu, sidhani kama kuna mtu anapenda kujiingiza kwenye matatizo makubwa hivi na sidhani kama alijua kuwa malumbano yao yangefikia hapa yalipo fikia. Tukumbuke pia shetani au watu wabaya pia hutafuta mpenyo mdogo tu ili waweze kupitisha adhma zao mbaya bila ya kujulikana. RIP Kanumba pole pia Ankal wetu na pole kwa wapendwa wote walioguswa na kifo hiki cha mpendwa wetu.

    ReplyDelete
  29. Nimeumia saaaaaana. I did not know this young man personally but I loved him and his contribution to the community. Until we meet again Kanumba my your soul Rest in Eternal peace.
    Pole Ankal

    ReplyDelete
  30. Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi kweli Kanumba tutamkumbuka siku zote he is real the Great

    ReplyDelete
  31. I've never thought,for once in my life to be among commentators in public notices but Kanumba break the thought. and here I am with no hassitation at allto my act...please uncle...the links below are my best way celebrating The Great.
    http://www.youtube.com/watch?v=vjwDMPKjDMA
    http://www.youtube.com/watch?v=-abFh8_kICg

    ReplyDelete
  32. Ni kweli...Tupendane, kama hatuna upendo twafanya kazi bure! Thank you Kanumba! Asante Michu kwa kutuwekea video hii.

    ReplyDelete
  33. Kaka Michuzi,
    Ndio naingia mtandaoni usiku huu. Nimefurahia simulizi yako juu ya Steven Kanumba uliyemfahamu. Inatupa mwanga zaidi, na matumaini pia. Nimeweka kwenye Mjengwablog mahojiano yako na Steven Kanumba.
    Maggid Mjengwa.

    ReplyDelete
  34. ankal nasikitika unatangaza tuu mambo unayotaka wewe, mwenye enzi mungu ampumzishe kwenye pepo tulivu Steve, ameondoka mapema mno.
    sasa wewe ancha bias ya media, umezidi haswa.

    ReplyDelete
  35. Ankal,
    Kwanza naomba nikupe wewe pole za dhati kwa kuondokewa na Swahiba wako!!
    Ankal, sikuwahi kukutana na Steven lakini kila nilichosikia kuhusu yeye ni kama wewe ulivyotoa!!
    Huyu ni moja ya Nyota yetu kubwa iliyozimika ghafla!!
    Lakini, sisi, kama waja tu hatuna la kutenda ilobaki ni kumshukuru Mungu wetu, asaidia Familia ya Ndugu yetu, Rafiki zake na sisi wote!
    Ankal, nakuomba sana kwa niaba ya www.sokainbongo.com unifikishie rambirambi zangu za dhati kwa Ndugu zetu kwa Msiba huu mkubwa!
    MUNGU ATUBARIKI SOTE
    AMINA
    Storming Fo

    ReplyDelete
  36. Poleni,
    Ila Simulizi uliyoandika imetulia sana,umeelezea kiundani,kama ni kitabu basi mtu anatamani kusoma mpaka kurasa ya mwisho.
    Ila nimesikitishwa mno na watu wenye tabia ya kuwanyanyapaa baadhi ya watu iwe wenye vipaji au wasio na vipaji.

    Nadhani tunaweza kubadilika kama kutakuwa na watu wenye malengo ya kuwahoji wasanii na kuelezea hisia za ndani kwa jamii nje ya sanaa na si kuwalaumu tuu.

    Tunaweza kubadilika na kuwa na Upendo kama muhusika alivyosema kwenye mahojiano.
    kama tutaitambuwa kweli.
    Naona mfano kwa nchi ninayoishi,wenyeji wanaungana kama Taifa ndiyo maana wanamafanikio.

    Mungu ailaze maala pema peponi roho ya marehemu Stev Kanumba

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...