Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Luka Mang’enya ambaye aliaga dunia juzi, Jumanne, Aprili 24, 2012 nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Meja Jenerali Mstaafu Luka Godfrey Mang’enya alilitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa miaka 31, miezi miwili na siku 16 tokea alipojiunga na Jeshi Aprili 13, mwaka 1966 akiwa mwanasheria, hadi alipostaafu Juni 30, mwaka 1997.

Katika salamu zake kwa Jenerali Mwamunyange, Rais Kikwete amemwomba Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi kumfikishia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa familia ya Meja Jenerali Mang’enya na kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi kwa kumpoteza mwenzi wao na kamanda wao.

Rais Kikwete amesema katika salamu zake, “Nimepokea kwa huzuni na majonzi taarifa ya kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Luka Godfrey Mang’enya ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia juzi nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.”

“Nilifahamu vizuri Meja Jenerali Mang’enya wakati wa uhai wake. Alikuwa Mzalendo na mtumishi mwadilifu na mwaminifu kwa taifa letu. Tokea alipojiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwaka 1966 akiwa mwanasheria hadi alipostaafu miaka 31 baadaye akiwa kwenye nafasi ya kijeshi ya Meja Jenerali na akiwa Jaji Advocate-General wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Mang’enya alithibitisha uaminifu wake kwa nchi yetu na uhodari wake kama mwanasheria, mpiganaji na kamanda. Tutaendelea kumuenzi kwa mchango wake kwa taifa letu.”

Rais Kikwete ameongeza: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange salamu zangu wa rambirambi kufuatia kifo cha Meja Jenerali Mang’enya. Naomba pia kupitia kwako uniwasilishie salamu nyingi za rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wa Meja Jenerali Mang’enya ambao wameondokewa na mhimili mkuu wa familia yao.”

“Aidha, kupitia kwako uniwasilishie salamu zangu kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambao yamempoteza mwenzi wao na kamanda wao. Wajulishe wanafamilia, makamanda na wapiganaji wote kuwa niko nao kwa sababu huu ni msiba wetu sote. 

Nawaombea moyo wa subira katika kipindi hiki na naungana nao wote kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema peponi roho ya Marehemu Meja Jenerali Luka Godfrey Mang’enya. Amen.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

26 Aprili, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Poleni sana wanafamilia wote wa Mang'enya, tuko pamoja, Mungu amweke pema peponi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...