MECHI YA TWIGA STARS, ZIMBABWE YAFUTWA
Mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) na Zimbabwe iliyokuwa ichezwe keshokutwa (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imefutwa.
Uamuzi huo umefanywa na Chama cha Mpira wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) ambayo sasa imeamua kucheza mechi ya kirafiki na Zambia. Mechi hiyo itachezwa Aprili 28 mwaka huu jijini Harare.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na jitihada za kuitafutia mechi za kirafiki Twiga Stars kabla ya kucheza mechi ya mashindano dhidi ya Ethiopia ambayo itafanyika Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.
MTIBWA SUGAR YAPOTEZA MECHI DHIDI YA AZAM
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemuondoa mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma kwenye orodha ya waamuzi kwa kuvuruga mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyochezwa Aprili 23 mwaka huu.
Pia waliokuwa waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo; Samuel Mpenzu na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha nao wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Vilevile Kamati imeipa Azam ushindi wa mabao 3-0 kwa mujibu wa Ibara ya 31 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa kanuni hiyo, timu itakayohesabika kupoteza mechi (Mtibwa Sugar) itakuwa imefungwa mabao 3-0.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom kifungu cha 22(3-6) Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000, imepoteza mapato yote ya mchezo huo na inatakiwa kulipa faini hiyo kabla ya mechi inayofuata.
Nao makamishna watatu; Abdallah Mitole wa Dar es Salaam, William Chibura (Musoma) na Omari Mawela (Mwanza) wameondolewa kwenye orodha ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kufika kwenye mechi walizopangiwa kusimamia bila taarifa.
Makamishna hao wametakiwa kutoa maelezo ya maandishi wakieleza sababu za kutofika kwenye mechi. Mechi walizokuwa wamepangia ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mitole), Kagera Sugar vs Yanga (Chibura) na Kagera Sugar vs African Lyon (Mawela).
Nayo Moro United imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya wachezaji wake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadirishia (dressing rooms) wakati wa mechi namba 171 kati yao na Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 8(16).
Pingamizi la Villa Squad dhidi ya African Lyon kuwa wakati wa mechi yao ilitumia wachezaji wawili (Mohamed Samata na Benedict Jacob) ambao mikataba yao imemalizika limetupwa kwa vile wana leseni halali za kucheza ligi.
Pia mwamuzi wa mechi namba 160 kati ya Moro United na Oljoro JKT, Nathaniel Lazaro wa Kilimanjaro amefungiwa miezi sita na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa kutozingatia kutunza muda kwa mujibu wa kanuni ya 26(1)(f).
Vilevile Kamishna wa mechi ya Moro United na Oljoro JKT, Ali Mkomwa wa Pwani na Said Mnonga wa Mtwara aliyekuwa mwamuzi msaidizi mechi kati ya Villa Squad na Coastal Union wameandikiwa barua za onyo wakitakiwa kuwa makini kwenye michezo wanayosimamia.
9 POLISI WAPIGWA FAINI MIL 1/- KILA MMOJA
Kamati ya Ligi ya TFF imewafungia mechi tatu na kuwapiga faini y ash. milioni mmoja kila mmoja wachezaji tisa wa timu ya Polisi Dodoma baada ya kumpiga mwamuzi Martin Saanya kwenye mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu mjini Dodoma.
Wachezaji hao walioadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25(g)(iii) ni Noel Msekwa, Frank Sindato, Abdallah Matila, Bantu Admin, Salmin Kisi, Madope Mwingira, Sihaba Mkude, Kaliyasa Mashaka na Ibrahim Massawe.
Iwapo wachezaji hao watahama Polisi na kujiunga na timu nyingine, watahama na adhabu zao.
Vilevile timu ya Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri. Pia timu hiyo imepewa barua ya onyo kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi yao na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam ni mabingwa wa mezani!
ReplyDeleteHello TFF, badala ya kujenga mnabomoa. Zitafuteni sababu zinazosababisha haya yote na mvumbue njia za kuzuia. Tafadhali msisahau kusafisha nyumba yenu kwanza na kuonyesha mfano.
ReplyDeleteMwamuzi Msangi alijua adhabu itakayompata lakini bado aliamua kufanya madudu, bila shaka alipima kati ya faida za kuwa mwamuzi na kitu anachopata mara moja kwa kufanya madudu na akaamua kilicho bora kwake. Ndio uzuri wa sheria za soka kwamba maamuzi ya mwamuzi ni mwisho hata kama kafanya makosa ya wazi!!!
ReplyDeleteTFF aka AZAM aka SIMBA acheni danganya toto. Ina maana refa aliyechezesha mechi ya Azam na Yanga hakuvurunda? pamoja na kushindwa kuwaadhibu wachezaji wa yanga waliomfanyia vurugu? Tumeambiwa refa aliyechezesha mechi ya Azam na Mtibwa alichanwa mdomo na Salum Swedi vipi mbona hatuoni Swedi kafungiwa mwaka mmoja? Vipi mbona wachezaji wa Yanga waliodaiwa kumpiga/kumfanyia vurugu mwamuzi walifungiwa wengine mechi sita wengine miezi sita mpaka mwaka mmoja lakini wale wa polisi wanaodaiwa kutenda kosa hilo hilo wanafungiwa mechi tatu tu? Kwa namna yoyote ile iwayo mambo haya ndio yanayolifedhehesha soka letu na kujenga imani kwa wapaenzi na washabiki wa mchezo huu kwamba kuna mchezo mchafu unaendelea kwenye uendeshaji wa ligi yetu, na tuuyaache hayo kwa maana matokeo yake yameshaanza kuonekana kwenye mechi ya Yanga na Polisi HABARI NDO HIYO. (Kwa asiyefahamu aulizie mapato yaliyopatikana kwenye mchezo huo)
ReplyDelete