Ngorongoro Heroes imewasili salama hapa Khartoum jana saa 4 usiku kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. 

Mechi hiyo itachezwa Jumamosi kuanzia saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ni wa nyasi bandia, na hakutakuwa na kiingilio kwa
watazamaji.

Awali Ngorongoro Heroes ilitarajiwa kuwasili saa 2.10 usiku, lakini ndege iliyokuwa ipande Nairobi kuja hapa ilichelewa kuondoka kwa saa moja na nusu kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kulikosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha uwanjani hapo.

Mara baada ya kuwasili Taka Hotel ambapo imefikia, Ngorongoro Heroes ilifanya mazoezi ya saa moja kuanzia saa 4.30 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi dhidi ya Sudan. Ngorongoro Heroes ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hoteli ya Taka ndipo pia timu ya El Merreikh ya hapa Sudan imeweka kambi yake kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).El Merreikh ililala mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Lubumbashi.

Kwa mujibu wa kocha Kim Poulsen, wachezaji wote wako katika hali nzuri na kikosi kitakachoanza kwenye mechi hiyo kitajulikana kesho (Ijumaa) baada ya mazoezi ya mwisho yatakayofanyika saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum.

Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Aishi Manula, Ramadhan Singano, Hassan Dilunga, Frank Damayo, Frank Sekule, Issa Rashid, Hassan Ramadhan, Saleh Malande, Said Zege, Emily Mugeta, Jerome Lambele, Samir Ruhava, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Atupele Green, Dizana Yarouk, Jamal Mroki na nahodha Omega Seme.

Mwamuzi Aden Abdi Djamal wa Djibouti ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Djamal atasaidiwa na Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah. Waamuzi hao watawasili kesho (Ijumaa) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakati Kamishna wa mechi hiyo Patrick Naggi kutoka Kenya atawasili leo (Alhamisi) saa 2.10 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.

Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza mechi ya raundi ya pili dhidi ya Nigeria. Mechi ya kwanza itchezwa Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa kati ya Agosti 10 na 12 mwaka huu.

Ikifanikiwa kuitoa Nigeria, Ngorongoro Heroes itacheza mechi ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Afrika Kusini na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya Septemba 21 na 23 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 03, 2012

    Hawa vijana watunzwe,tuna matatizo makubwa kwenye timu ya wakubwa inayozeeka sasa..Na wale U17 wakuzwe,bila hivyo hatuendi kokote.

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...