Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Joseph Shiyo akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa Jukwaa la Taifa la Menejimenti ya Maafa ulioandaliwa na Ofisi hiyo, Jijini Dar es Salaam leo.
Washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Taifa la Menejimenti ya Maafa ulioandaliwa na Idara ya Uratibu wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es Salaam leo wakisoma kwa makini vitini vya mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo. Wa kwanza kushoto ni Mchambuzi wa Mradi wa UNDP Bw. Ulf Flink,
Na. Mwandishi maluum.
Sheria Na.9 ya Uratibu wa Misaada ya Maafa ya Mwaka 1990 (Disaster Relief Coordination Act) imeanza kufanyiwa marekebisho ili iweze kuitwa Sheria ya Menejimenti ya Maafa (The Disaster Management Act). Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu wa Maafa, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Joseph Shiyo, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Taifa la Menejimenti ya Maafa lililofanyika Jijini Dar es Salaam leo.
“Sheria mpya, itazingatia mzingo wa menejimenti ya maafa ambao unazungumzia uzuiaji maafa kabla hayajatokea, upunguzaji athari na urejeshaji hali baada ya maafa kutokea tofauti na sheria iliyopo ambayo inazungumzia utoaji misaada baada ya maafa kutokea. Aidha, Sheria hiyo itaainisha taratibu na stahili ya wanaoathirika na Maafa pamoja na namna ya kuhudumia waathirika waliolazimika kuyahama makazi kutokana na Maafa kwa kuzingatia sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 ya Mwaka 1999 (Land Act No. 4 na 5 OF 1999), kwani sheria iliyopo ipo kimya kuhusu masuala hayo” alisema Shiyo.
Alibainisha kuwa sheria mpya itatamka kuwa baada ya Maafa kutokea Serikali itakuwa na wajibu wa kurejesha hali, kwa kuwa kifungu Na. 5 Sehemu ya (1) ya sheria iliyopo hakijaeleza masuala ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Aliongeza kuwa sheria mpya itaruhusu kuanzisha kituo cha kufuatilia mwenendo na kuratibu maafa nchini (Emegency Operation Centre (EOC) ) na itatamka kuunda kamati katika ngazi ya mkoa , Wilaya , Kata na Vijiji.
“Ili kamati hizo ziweze kufanya kazi ya Menejimenti ya Maafa kwa ufanisi, sheria mpya itatamka kuanzishwa kwa mfumo wa kompyuta utakaodhibiti matumizi ya mifuko ya maafa kote nchini kama vile HAZINA inavyoweza kudhibiti HAZINA NDOGO” alisistiza Shiyo.
Sheria Na.9 ya Uratibu wa Misaada ya Maafa ya Mwaka 1990 (Disaster Relief Coordination Act) iliandikiwa Waraka wa Marekebisho tangu mwaka 2009, na mnamo mwaka 2011 Kikao cha Makatibu Wakuu kiliupitia Waraka huo na kutoa maoni yao, halikadhalika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri tayari limepitia rasimu ya Sheria hiyo na kutoa maoni yao na kwa sasa tayari rasimu hiyo ipo inapitiwa na kamati ya ufundi yenye kujumuisha Wizara.
Mkutano huo ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika tarehe 24 Novemba ,2011 ulihudhuriwa na wadau wa Maafa kutoka Wizara, Idara na taasisi za Serikali, mashirika ya Kimataifa pamoja na vyombo vya habari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...