Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi akisisitiza jambo wakati akifunga mafunzo ya siku saba kwa wakufunzi wa Sensa ngazi ya Taifa jana Mjini Dodoma.
 Baadhi ya Wakufunzi wa Sensa ngazi ya Taifa wakisikiliza na kunukuu baadhi ya mambo ya msingi wakati wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Hayupo pichani) alipokuwa akifunga Mafunzo ya siku saba ya wakufunzi hao yaliyofanyika Mjini Dodoma kuanzia wiki iliyopita. Picha zote na Jery Mwakyoma

Na Salama Njani –Dododma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rehema Nchimbi, amesema zoezi la Sensa ya watu na makazi hufanyika kwa maslahi ya Taifa na sio kikundi au watu Fulani kuitumia fursa hiyo kama njia ya kampeni kwa maslahi yao binafsi.
Amesema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kupenda kutumia fursa zilizopo na zinazojitokeza katika Taifa kwa kupigia kampeni za utashi wa makundi yao bila ya kujali faida na maslahi Taifa zinazotokana na fursa hizo.
Mhe Nchimbi ameyasema hayo huko Dodoma katika ukumbi wa chuo cha mipango wakati wa ufungaji wa mafunzo ya wakufunzi wa  Sensa ya watu na makazi kwa ngazi ya Taifa.
Amesema mafanikio ya zoezi la Sensa yatafanikiwa sana kwa kuwepo mashirikiano ya pamoja  kati ya wananchi na viongozi wa ngazi zote, na kuacha dhana ya kutegemea zoezi hilo kuligeuza  kuwa kama kiwanja cha  kuchezea kwa maslahi binafsi.
“Tulitendee haki zoezi la Sensa kwa maslahi ya Taifa na tuache kutumia fursa hii kwa kampeni au kuligeuza kuwa kama kiwanja cha kuchezea na kusahau faida zitokanazo na zoezi hili”amesema.
Akizungumzia suala la baadhi ya watu kutoa na kusambaza taarifa zisizo sahihi, Mhe Nchimbi amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kwa kutoa taarifa katika taasisi zinazohusika  dhidi ya wale wote watakao husika na kupotosha taarifa za ukweli kuhusu Sensa.
Amefahamisha kuwa taarifa sahihi pamoja na takwimu za uhakika zitokanazo na zoezi la Sensa zitasaidia  Taifa kwa kiwango kikubwa kuwa na maamuzi sahihi ya kupanga mipango ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa ya mwaka 2022.
Amesisitiza kuwa tegemeo la Taifa ni kuwa Takwimu za Sensa hii pia ni kiashirio cha kuonyesha ubora wa matunda ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania ambayo wengi watakuja kujifunza.
Akiwaasa wakufunzi wa mafunzo hayo ,Mhe Rehema Nchimbi amesema serikali imewapa dhamana ya kwenda kuwafundisha walimu wa makarani wa Sensa kwa kutegemea kupata makarani walio bora hivyo ni vyema kutumia juhudi na maarifa katka kufanikisha kazi hiyo.
Aidha amewakumbusha viongozi wote wa vyama na serikali kuhamasisha Umma kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi,pamoja na wananchi kuwa tayari kutoa taarifa za maswali watakayoulizwa kwa lengo la kupata Takwimu sahihi.
Mafunzo hayo ya wiki mbili ambayo yalifunguliwa na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda, yamewashirikisha washiriki wapatao 150 kutoka katika wizara,idara na Taasisi mbali mbali za Serikali,vyuo vya elimu ya juu na vyama vya watu wenye Ulemavu, yanalenga kuwawezesha wakufunzi hao kuwa walimu wazuri wa kwenda kuwafundisha wakufunzi wengine wa makarani wa Sensa katika ngazi za Mikoa,Wilaya,Kata na shehia kwa Tanzania nzima.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...