JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MIPAKA YA MSITU WA KAZIMZUMBWI HAIJABADILIKA
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa tahadhari kuwa mtu yeyote atakayekutwa ndani ya Msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbwi ulioko wilayani Kisarawe atachukuliwa hatua za kisheria.
Tahadhari hii inatolewa baada ya Wizara kupata taarifa kuna kikundi cha watu ambacho kinajiandaa kuingia kwenye msitu huo na kufanya shughuli mbalimbali, pamoja na kujenga nyumba za kudumu. Vilevile baadhi ya watu wasiojulikana wameharibu mabango na ofisi ya msitu huo.
Wizara inawakumbusha wananchi kuwa msitu wa Kazimzumbwi ni wa Serikali kuu ambao ulihifadhiwa mwaka 1954 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 306 la tarehe 24 Septemba, 1954.
Mpaka huo unadhihirishwa na maboya yanayotambulisha mpaka wa msitu. Aidha, msitu huo haujawahi kufanyiwa mabadiliko (variation) yoyote ya mpaka, hivyo mpaka uliowekwa wakati wa kutangazwa msitu mwaka 1954 unaendelea kutambulika kama mpaka halali.
Msitu huo umekuwa ukivamiwa mara kwa mara na zimefanyika juhudi mbalimbali za kuwaondoa wavamizi lakini wamekuwa wakirudi tena baada ya miaka kadhaa kupita. Hivyo, kama kawaida Wizara imejiandaa kikamilifu kukabiliana na uvamizi wowote unaoweza kujitokeza katika msitu huo kama ilivyokuwa ikifanya katika nyakati mbalimbali hapo awali.
angalau mmesema jambo
ReplyDelete