Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza udhamini wa Pool kwa mwaka 2012 utakaojulikana kwa “Safari Lager National Pool Champuionshis”.Mazungumzo hayo yalifanyika TBL Dar es Salaam jana.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager leo imetangaza rasmi kudhamini kwa mara nyingine tena mashindano ya taifa ya mchezo wa Pool kwa mwaka huu. Mashindano haya yajulikanayo kama “Safari Lager National Pool Championships 2012” yanafanyika kwa mwaka wa tano sasa, Safari Lager imekuwa wadhamini wakuu wa mashindano haya kwa miaka yote mitano.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo Meneja wa Bia ya Safari Lager Bwana Oscar Shelukindo alisema; “Nia hasa ya kudhamini mashindano haya ni kuibua vipaji kwa vijana na kuwasaidia kiuchumi hasa ukizingatia kwamba kwa sasa michezo ni ajira kama ajira nyinginezo. Mchezo wa pool huandamana pia na burudani waipatayo wachezaji kutokana na mchezo huo”. 

Bw. Shelukindo aliendelea kusema; “Ukiachilia mbali ongezeko la kipato na burudani, mchezo wa pool husaidia kuwakutanisha watu mbalimbali kufahamiana kibinafsi na kibiashara, hujenga afya bora na katika mazingira yetu ya sasa michezo inamsaidia mtu kutumia muda wake vizuri ili kuepuka mambo mengine yanayoweza kumsababishia matatizo kama vile kukaa vijiweni, ugomvi nk”. 

Mashindano yaliyomalizika ya mchezo wa Pool kwa vyuo vikuu mwaka huu yalikuwa na ujumbe; Play Pool, Stay Cool.. hii ikiwa na maana ya kuwashauri wanavyuo kucheza Pool na kubakia watulivu... wasio na matata!.. Mashindano ya kitaifa ya pool kwa vyuo vikuu yalifanyika mkoani Iringa ambapo chuo cha SAUT cha mkoani Mwanza kiliibuka kidedea baada ya kuwachapa chuo cha IFM cha Dar Es Salaam!.

Safari Lager imekuwa wadhamini wa mchezo wa Pool toka mwaka 2008, imedhamini mashindano ya ndani na ya nje ya nchi pia. Imedhamini timu ya Taifa ya mchezo wa Pool kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo wa Pool nchini Ufaransa mwezi wa kumi mwaka 2010 ambapo timu yetu ilifanya vizuri. Mashindano ya kimataifa ya mchezo wa Pool yatafanyika katikati ya mwezi wa kumi nchini Uingereza, katika mji wa Blackpool.

Naye Bw. Amos Kafwinga, katibu wa chama cha mchezo wa Pool Tanzania (TAPA) alisema mashindano ya mwaka huu yana mvuto wa aina yake kwani katika ngazi ya taifa yatahusisha vilabu na sio mikoa kama miaka ya nyuma. “Mashindano yataanzia mikoani kwa Vilabu kushindana katika ngazi ya Mkoa na baadae vilabu vilivyoshinda katika ngazi ya mkoa vitawakilisha mikoa yao na kushindana katika ngazi ya Taifa ili kupata clabu ambayo ni mshindi wa jumla kwa vilabu vya Mikoa yote’.

Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi kutimua vumbi katika mkoa wa Tanga Juni 21 mwaka huu. Mashindano haya yatahusisha vilabu katika Mikoa 16, ambayo ni Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Iringa, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Kagera, Lindi,Temeke, Ilala na Kinondoni. Mashindano ya mwaka huu yameongeza mikoa miwili ambayo ni mkoa wa Tabora na Lindi. Fainali za vilabu kitaifa zitafanyika katika mkoa wa Mwanza mwishoni mwa mwezi Septemba.

Mwaka jana mashindano ya taifa yalihusisha timu za mikoa ambapo Mkoa wa Dodoma waliibuka mabingwa baada ya kuwatoa mkoa wa kimashindano wa Temeke. Mashindano ya mwaka jana yalifanyika mkoani Dodoma. Timu ya Dodoma walijipatia kikombe, medali za dhahabu na jumla ya shilingi milioni tano taslimu.

Akitoa shukrani kwa Safari Lager kwa niaba ya Chama cha Mchezo wa Pool Tanzania (TAPA), Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Isaac Togocho alisema “Taswira ya mchezo wa pool hapa nchini imebadilika kwa kiasi kikubwa na sasa inawavutia vijana mbalimbali kwani si mchezo wa kupotezea muda tena kama wengi walivyodhania, Pool ni miongoni mwa michezo inayokua kwa kasi kubwa na kuwapatia kipato wachezaji na vijana kwa ujumla. 

Hii yote imetokana na Bia ya Safari Lager kukubali kuudhamini mchezo wa Pool table. Kwa niaba ya chama tunatoa shukrani nyingi sana na kuomba Safari Lager iwe nasi ili tuendelee mbele zaidi”.

Bwana Oscar alizitaja zawadi za washindi katika ngazi ya mikoa kuwa timu itakayoshinda itajipatia kitita cha shilingi laki saba, washindi wengine watajipatia shilingi laki tatu na nusu kwa mshindi wa pili, laki mbili kwa mshindi wa tatu na laki moja kwa mshindi wa nne. 

Washindi kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wa kiume watajipatia shilingi laki tatu na nusu kwa bingwa na laki mbili kwa mshindi wa pili. Wachezaji wa kike watachuana pia ambapo washindi watajipatia laki mbili na nusu kwa bingwa na shilingi laki moja na nusu kwa mshindi wa pili.

Timu itakayoibuka mshindi katika ngazi ya taifa itaibuka na kikombe pamoja na medali za dhahabu zawadi hizi zitaandamana na zawadi ya jumla ya shilingi milioni tano taslim. Jumla zaidi ya shilingi milioni hamsini na saba zitatolewa kama zawadi za pesa taslimu katika michuano ya mwaka huu.

Bwana Oscar alimalizia kwa kutoa shukrani kwa wanywaji wa bia ya Safari Lager na wachezaji wote wa mchezo wa Pool kwa ujumla, aliwaomba wachezaji wajinoe zaidi ili kufurahia zawadi za mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...