
Watu wengi, kwa mamia, waliiunga mkono familia ya Mzee Kabululu katika kipindi hicho kigumu cha msiba huu mkubwa wa mkuu huyo wa familia kwa miaka mingi. Familia yake, inaomba radhi kwamba inakuwa vigumu kwa familia hiyo kumshukuru kila mtu kwa ubinafsi wake na kwa mchango wake mkubwa. Inaomba itoe shukurani za jumla kwa wote walioshiriki, kwa namna moja ama nyingine, kujaribu kuokoa maisha ya Mzee wao na hatimaye kwenye mazishi na msiba wake.
Familia ikiongozwa na Mama yetu, Mama Verdiana Kashumba Kabululu inapenda kutoka shukurani zake kwa madaktari na wauguzi wote wa Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa jitihada na juhudi zao za kujaribu kuokoa maisha ya Mzee Kabululu jioni ile ya Aprili 11, 2012. Familia inawashukuru sana kwa jitihada zao.
Familia pia inapenda kutoa shukurani kwa Wana-Chato kwa kuiunga mkono familia, kwa hali na mali, wakati wote wa msiba na mazishi ya Mzee Kabululu. Tunawashukuru majirani na marafiki, wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume kwa kumsindikiza vizuri Mzee Kabululu.
Tunakishukuru kikundi cha Wananzengo wakiongozwa na Bwana Musiba Magoma, tunamshukuru Baba Paroko wa Parokia ya Chato Father Henry Mlinganisa na Baba Paroko Msaidizi, Father Gratian Kipara kwa uongozi wao wa kiroho. Tunaishukuru Kwaya ya Parokia ya Chato ikiongozwa na Ndugu Edward Otto kwa jitihada zao wakati wote wa msiba. Tunawashukuru Wanajumuia wote wa Kanisa Katoliki Chato. Tunawashukuru waonyeshaji video na wapambaji ambao wote kwa pamoja walishiriki kikamilifu kwa siku zote nane za msiba. Tunamshukuru Mshereheshaji Dkt. Msafiri kwa mchango wake. Tunaushukuru uongozi wa Wilaya ya Chato kwenye ngazi mbali mbali– Serikali na Vyama vya Siasa- kwa mchango wao mkubwa. Kwa wote tunasema shukurani sana.
Tunawashukuru wote, ndugu, jamaa na marafiki, walioshiriki katika msiba na mazishi ya Mzee Kabululu. Walitoka sehemu nyingi na tofauti. Walitoka ndani na nje ya nchi. Walitoka mikoa mbali ya nchi yetu. Walitoka miji ya Dar es salaam, Mwanza, Bukoba, Biharamulo na Muleba na kutoka maeneo na vijiji vya Mikoa ya Kagera na Geita – Katoke, Kimbugu, Ruhanga, Kamachumu, Ngote, Bunena, Buganguzi, Kashekela, Bushaju, Kagoma, Katende, Bwanga na Buzirayombo. Wote walijitokeza kwa wingi kumzika Mzee wao na tunawashukuru kwa dhati ya moyo wao wa upendo.
Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa msada wake katika msiba huo. Alitoa mchango mkubwa sana kwetu na tunamshukuru sana kama familia.
Sambamba na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunawashukuru watumishi wa Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) pamoja na watumishi wengine wa Ikulu kwa mchango wao mkubwa katika msiba huu. Tunasema asanteni sana kwa kutuunga mkono. Tunathamini sana heshima yenu kwetu.
Tunaishukuru Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa mchango wao mkubwa na kwa kutuunga mkono. Asanteni sana kwa mchango wetu.
Tunashukuru sana marafiki wa watoto, wajukuu na vitukuu wa Marehemu Mzee Kabululu katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Chato, Geita na Sengerema. Tunawashukuru sana wote kwa michango na ushiriki wao katika msiba wa baba yetu.
Kama tulivyosema mwanzo, ni vigumu kumshukuru kila mmoja wetu. Tunawaomba kwa heshima na tahadhima kupokea shukurani wetu za jumla. Msiba wa baba ni mgumu sana lakini wa kwetu ulifanywa rahisi kidogo kwa misaada na michango yetu ya hali na mali. Asanteni Sana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...