GAMBIA YAWASILI KUIKABILI TAIFA STARS
Timu ya Taifa ya Gambia (The Scorpions) imewasili nchini jana (Juni 7 mwaka huu) saa 5.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo wenye watu 31 wakiwemo wachezaji 22 unaongozwa na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo wan chi hiyo, Malang Jassey.

Viongozi wengine ni Ofisa Utawala wa timu Modou Sowe, Kocha Luciano Machini, makocha wasaidizi Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, Kocha wa makipa Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist) Pa Matarr Ndow, Mtunza vifaa Sanna Bojang na Daktari wa timu Kalifa Manneh.

Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.

Gambia ‘The Scorpions’ itafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 8 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume wakati kesho muda huo huo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa.

Kambi ya Taifa Stars iko vizuri ambapo leo jioni timu itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa. Pia kesho itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 11 jioni baada ya Gambia kuwa wamemaliza.

Jumamosi saa 4 kamili asubuhi kutakuwa na mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili; Mdenmark Kim Poulsen wa Taifa Stars na Mtaliano Luciano Machini wa The Scorpions wakiwa na manahodha wao na Waandishi wa Habari utakaofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

TIKETI KUANZA KUUZWA JUMAMOSI
Tiketi kwa ajili ya pambano la Taifa Stars na The Scorpions zitaanza kuuzwa kesho (Juni 9 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Soko Kuu la Kariakoo na Uwanja wa Taifa.

Pia mauzo yatafanyika siku ya mechi kwenye vituo hivyo kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 6 mchana kabla ya kuhamia Uwanja wa Taifa.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni 36,693 kati ya jumla ya viti 57,558 vilivyopo katika uwanja huo wa kisasa. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ni sh. 5,000.

Kwa upande wa VIP C watalipa sh. 10,000 wakati VIP B ni sh. 20,000. Kiingilio kwa jukwaa la VIP A ambalo linachukua watazamaji 748 tu ni sh. 30,000 kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 08, 2012

    Wambura hivi tulituma watu kwenda kuangalia mchezo kati ya Morocco na Gambia Banjui?Nina uhakika wao walituma watu Abijan kutuangalia..Kwenye hao wachezaji wao mnafahamu 'man to watch' ni nani?Mpira unahitaji na mbinu nyingi siyo tu kuingia uwanjani bila kujua unaenda kucheza na nani.Google hata hao wachezaji wa Gambia wengine wanaweza kuwa ufaransa huko.Nina uhakika tutawafunga.

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...