TAARIFA YA UFUATILIAJI WA MCHELE ULIOLALAMIKIWA MKOANI KILIMANJARO NA AMBAO ULIINGIZWA NCHINI BILA KUZINGATIA TARATIBU ZA KISHERIA


Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyoundwa chini ya Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi No. 1 ya mwaka 2003, ili kudhibiti ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi, na vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya ya jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo. Ili kutimiza wajibu huo, TFDA inasimamia pamoja na mambo mengine udhibiti wa uingizaji wa vyakula kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kulinda afya za watumiaji. 

Katika udhibiti wa vyakula kutoka nje ya nchi michakato mbalimbali hufanywa na TFDA ili kuwa na uhakika juu ya usalama wa bidhaa  kwa kufanya tathmini na uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za bidhaa na baadaye kuzisajili baada ya kujiridhisha juu ya usalama wake, kutoa vibali vya kuingiza nchini, kufanya ukaguzi katika vituo vya forodha kabla ya  kuingizwa nchini na maeneo ya kuuzia baada ya kuruhusiwa kuingizwa nchini.

Aidha, TFDA imeweka milango wazi kwa Umma kuwasilisha  taarifa na malalamiko yoyote juu ya usalama na ubora wa bidhaa inazozidhibiti. Mnamo tarehe 3/5/2012 kulitolewa taarifa kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro juu ya uwepo wa mchele ulioingizwa nchini kutoka nchi jirani bila kuzingatia utaratibu wa kisheria na ambao ulisadikika kuwa hauna ubora na usalama unaokubalika. 

Ufuatiliaji wa mchele huo ulifanywa na kikosi kazi kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa ambacho kilihusisha Afisa wa TFDA (Kanda ya Kaskazini), Maafisa Afya kutoka katika Manispaa ya Moshi, Maafisa wa TRA, Maafisa Biashara na Polisi.  Ufuatiliaji wa mchele huo ulibaini kuwa mchele uliingizwa nchini kutoka nchi jirani pasipo kibali cha TFDA.

Katika ukaguzi huo jumla ya mifuko 150 yenye ujazo wa kilo 25, ilizuiliwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro. Aidha sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.  Matokeo ya uchunguzi wa kimaabara yalionesha kuwa mchele huo unafaa kwa matumizi ya binadamu. Hivyo TFDA na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro tumejiridhisha kuwa mchele huo ni salama na unaweza kutumiwa na binadamu. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya walioingiza mchele huo kinyume cha utaratibu.

Rai kwa wafanyabiashara inatolewa kuzingatia taratibu za uingizaji wa chakula nchini ili kuepusha uwezekano wa kuingiza bidhaa ambazo zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa walaji. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote ambao watabainika kuingiza vyakula nchini bila ya kuzingatia taratibu za kisheria.
TFDA inatoa wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika jukumu la kulinda afya za walaji kwa kutoa taarifa pale wanapouziwa au kuhisi kuwepo kwa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba duni na bandia ambavyo havikidhi viwango vya ubora na usalama au pale sheria inapovunjwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.

Imetolewa na;
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Barabara ya Mandela, Mabibo External,
S.L.P 77150
Dar Es Salaam, Tanzania
Simu:              +255 22 2450512/2450751/2452108
Fax:                 +255 22 2450793
Barua pepe:    info@tfda.or.tz
Tovuti:            www.tfda.or.tz

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 14, 2012

    Hivi kwanini mnaagiza mchele nje kwani tunaolima sisi hautoshi au?mambo mengine sielewi jamani muwe mnatusaidia kufuta ujinga, najua mbeya na shinyanga wanalima mpunga sasa why tuagize nje tena? ukute na ndizi zinatoka china mweee tufwile wa Tanzania

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...