Mkurugenzi Mkuu na Meneja Mwendeshaji wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko (katikati) akishikilia bendera ya Zambia na Tanzania kama ishara ya uzinduzi wa safari za Lusaka – Zambia wikiendi iliyopita. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu – Wizara ya Uchukuzi Tanzania Bw. John Mngodo na kulia ni Balozi wa Zambia nchini Tanzania Mh. Judith Kangoma-Kapijimpanga
Waziri wa Uchukuzi, Usambazaji na Mawasiliano wa Zambia Mh. Yamfwa Mukanga (wapili kushoto) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kutoka Tanzania Bw. John Mngodo (wapili kulia) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda wikiendi ikiyopita. Pamoja nao ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mh. Grace Mujuma (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu na Meneja Mwendeshaji wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko (kulia). Precision Air ilizindua safari kwenda Lusaka, Zambia.
Lusaka – Zambia. Wananchi wa Zambia wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo Mh. Yamfwa Mukanga wamepongeza hatua ya shirika la ndege la Precision Air kuanzisha safari kati ya Lusaka na Dar es Salaam wakisifia kwamba itarutubisha hali ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
Lusaka – Zambia. Wananchi wa Zambia wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo Mh. Yamfwa Mukanga wamepongeza hatua ya shirika la ndege la Precision Air kuanzisha safari kati ya Lusaka na Dar es Salaam wakisifia kwamba itarutubisha hali ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika dhifa ya ufunguzi katika hoteli ya Taj Pamodzi, Waziri wa Uchukuzi, Kazi, Usambazaji na Mawasiliano wa Zambia Mh. Yamfwa Mukanga (Mb) alisifia mpango wa shirika hilo katika maamuzi ilyofanya ya kuja kufungua milango ya kibiashara ya usafiri wa ndege nchini humo.
“Safari hii ya kwenda na kurudi mlioizindua hivi leo itafanikisha biashara na utalii, pamoja na kuongeza uelewano na ushirikiano baina ya watu wetu. Hakika itakuwa kama nguzo ya nyongeza katika kuimarisha uhusiano wetu na kuufikisha ushirikiano baina ya nchi zetu mbili katika mahali bora,” alisema Mh. Mukanga.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu na Meneja Mwendeshaji wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko alisema kwamba shirika hilo imejidhatiti katika kupunguza kero ya usafiri kwa abiria baina ya Zambia na Tanzania waliokuwa wanatumia masaa 9 na zaidi wakiwa safarini ili kuweza kufika Lusaka au Dar es Salaam kwa sababu ya kutokuwepo na safari za moja kwa moja.
Pia mmoja ya wafanyabiashara kutoka Zambia waliyokuwepo katika dhifa hiyo, Bw. George Makulu, alisema, “Kuna mategemeo makubwa sana katika soko hili na imani kubwa sana katika huduma ya Precision Air kutokana na historia nzuri ya usalama na kuodhoreshwa kwake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.”
“Kama Precision wataweza kuendeleza kusafiri kwa wakati, pamoja na aina zao za ndege ambazo ni nzuri kwa ajili ya kubebea mizigo, hakika tutawapa ushirikiano wa kutosha,” aliongeza.
Pia akizungumza katika ufunguzi huo, Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mh. Grace Mujuma alisifia sana shirika hili la ndege kwa hatua waliofikia. “Habari hizi ziliposambaa mwanzoni kwamba Precision wangeanza safari kuja Lusaka, kulikuwa kuna hali ya kutoamini. Lakini leo mmeweza kuwaziba midomo wote waliokuwa hawaamini, na uhakika mmetuletea sifa kubwa Tanzania.”
Uzinduzi wa safari hizi za Precision Air pia zilioongozana na uwepo wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Bw. John Mngodo ambaye alihakikisha ushirikiano wa serikali katika shirika hili la ndege.
“Kwa niaba ya serikali ya Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, napenda kuhakikisha ushirikiano wa serikali kwa Precision Air na wawekezaji wengine katika sekta hii ya anga ambao wanaweza kudiriki kufanya utafiti unaohitajika na kuja na mipango endelevu yanayoweza kunufaisha uchumi wa nchi zetu mbili,” aliongeza.
“Hakika tunategemea kwamba hatua hii ambayo Precision Air imefikia itazaa matunda zaidi katika sekta hii ya usafiri wa anga kwa ukanda huu pamoja na kupunguza gharama za kufanya biashara na halikadhalika kutangaza ukanda wetu kama vutio na sehemu nzuri ya uwekezaji,” alisema Bw. Mngodo.
Precision Air ilizindua safari baina ya Dar es Salaam na Lusaka wikiendi iliyopita, safari hizo zitakuwa mara tatu kwa wiki; Jumatano, Ijumaa na Jumapili kwa nauli ya kuanzia dola 399 kwenda na kurudi.
Dar es Salaam - Lusaka ni ruti ya sita ya kimataifa ambayo shirika hili la ndege linasafiri. Zingine ni Johannesburg, Hahaya, Nairobi, Entebbe na Mombasa. Kitaifa Precision Air inasafiri kwenda Mwanza, Bukoba, Musoma, Kigoma, Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar, Mtwara na Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...