Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji (ambayo katika uamuzi huu itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai 17 mwaka huu, baada ya kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika mashindano ya Kombe la Kagame kama zilivyowasilishwa mbele yake imefikia uamuzi ufuatao;

1. Kwa mujibu wa mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu, Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji kama Sekretarieti ilivyofanya katika barua yake ya Julai 14 mwaka huu ulikuwa sahihi.

2. Kamati ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.

3. Aidha Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho la kisheria haupo.

4. Hata kama kamati ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu.

5. Kisheria utata huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati akiwa huru.

Kutokana na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012.

Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 20, 2012

    Mbona kila siku mnasisitiza kuridhia kwenu kwa Yondani kuichezea Yanga wakati wa kombe la Kagame? Ina maana baada ya Kagame hamtaridhika tena au? Semeni mmeridhia aichezee Yanga kwa kipindi fulani, haijalishi anachezea michuano gani.

    Simba wenzangu jamani, tusiweweseke sana na kuondoka kwa Yondani, ni maisha tu haya. Hata maofisini watu wanahama kutoka kampuni moja kwenda nyingine kila leo, tena makampuni ya kishindani. Sisi tuna uwezo mkubwa sana tu wa kuliziba pengo lake, na iwe funzo kwetu kuwa makini zaidi siku za usoni. Huyu mtu ana familia na majukumu yake jamani.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 20, 2012

    Safi sana TFF kwa kuangalia sheria inasemaje na mchezaji kupewa haki yake siyo kama mambo ya kizamani ambapo FAT ilikuwa inafungia wachezaji ovyo ovyo .Ikumbukwe pia kipaji cha Yondani kitaisadia Taifa stars ,hivyo simba kaeni kando Yondani alikuwa huko na mmeshindwa makubaliano ,mpira wa sasa ni maslahi zaidi ,hivyo Yanga ina maslahi zaidi na Yondani ameridhika kuitumikia ,hivyo wana msimbazi fungeni mjadala huu .Mdau big Joe

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 21, 2012

    Simba wenzangu nini hii!!!Achana na Yondani tafuteni wachezaji wengine shida nini Simba timu kubwa jamani watu wataingia na kuitoaka.

    Tumeona wangapi wanaondoka halafu wanao,ba kurudi!

    Mambosasa aliondoka na kurudi,Kaseja aliondoka na kurudi,Deo aliondoka na kurudi hata kwa wenzetu vivyo hivyo cha ajabu nini kuondoka Yondani.Mwacheni akacheze Yanga.

    Ila mimi ningekuwa kiongozi walioondoka kamwe wasingerudi tena kwenye klabu yetu.Shida ni nini bwana wachezaji wote hawa duniani!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...