MKURUGENZI wa Makumbusho ya Taifa, Jackson Kihiyo (pichani) amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi huyo alisema aliitwa na mkubwa wake wa kazi, ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na kufahamishwa kuwa amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwani kuna tuhuma kuhusu utendaji wake katika ofisi hiyo.

“Baada ya kupewa taarifa hizo, juzi(jumanne) nilikabidhi ofisi na hivi sasa nipo nyumbani. Cha muhimu ni kuwa sijafukuzwa ila nimesimamishwa na ninaendelea kupata mshahara wangu kama kawaida haid pale watakapomaliza huo uchunguzi wao,” alisema Kihiyo
Kihiyo alisema, hakutaka kumhoji mkuu wake wa kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kwa sababu alitaka wawe huru na wafuatilie kwa kina bila kuingiliwa, hivyo hadi sasa hafahamu kilichomsimamisha kazi.

“Najua wakimaliza watanijulisha, sina mashaka yeyote kwa sababu najua hakuna kibaya nilichofanya, nikiwauliza uliza watadhani ninataka kuwaingilia katika uchunguzi wao. Waache wafanye uchunguzi kwa utaratibu na kwa uhuru wakimaliza watanieleza kilichopatikana,” alisema Mkurugenzi huyo. 

Chanzo cha habari kutoka katika ofisi hiyo kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake kilibainisha kuwa mkurugenzi huyo amesimamishwa baada ya wafanyakazi kupeleka malalamiko kwa katibu mkuu, Maimuna Tarishi, ikiwemo utata katika ukusanyaji wa mapato na maslahi ya wafanyakazi.

“Mkurugenzi alitoa amri ya kukusanya mapato katika vituo vyote na kisha mapato hayo katika akaunti ya makao makuu. Hili jambo lilizua maswali kwa sababu tutapelekaje mapato yote makao makuu, vituo vitajiendesha na nini? Lakini lingine ni maslahi duni ya wafanyakazi, hatujaboreshewa mishahara kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa malalamiko mengine kuhusu utendaji wa mkurugenzi huyo ni kitendo cha Ofisi kutumia Menejimeti ya Umma kumuadhibu mfanyakazi badala ya kutumia Kamati ya Nidhamu jambo alilodai linasababisha uonevu mkubwa kwa wafanyakazi.

Shutuma nyingine dhidi ya Kihiyo ni upandishwaji wa vyeo kwa wafanyakazi usiozingatia sifa stahiki na kutokuwepo mipango endelevu ya mafunzo kwa wafanyakazi. 

Kabla ya Kihiyo kushika nafasi hiyo, Mkurugenzi wa Makumbusho alikuwa ni Nobert Kayombo, ambaye alifariki Novemba 30, 2010.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 27, 2012

    Ankal,Mkuu huyu simfahamu lakini kwa nilivyosoma hapo juu, mpaka hapo sioni kosa lake!

    NYIE WAFANYAKAZI MLIOPELEKA MAJUNGU NAYO YAKAPOKELEWA, NATAMANI SANA NDIO MNGEKUJA KWANGU KUNILETEA YAANI UMBEA SITAKI NINGEWAULIZA YAFUATAYO;

    (1) JE, mna chama cha wafanyakazi au mliwahi kuthubutu mkanyimwa?

    (2) Je, mlishawahi kujipima utendaji wenu wa kazi uko vipi kisha ndio muweze kufananisha na kiwango mtakacho? Nyie nanyi si kama wale wafanyakazi wa Serikalini ambao ofisi inawafanyakazi 300 lakini wanaofika kazini na kuwajibika ni 100 tu? Wengine walipo haijulikani?

    (3) Kuitisha mapato yote sehemu moja ni vizuri sana, hii ni kwa ajili ya Control. Hii ingesaidia kujua kila kituo kinapata kiasi gani kisha ndio muombe hiyo nyongeza ya mshahara.

    (4) Vipi kupiga soga na utendaji mbovu meshaacha?

    Niko kwenye sekta binafsi na nimejiajiri, nanaiheshimu kazi yangu, naipenda na kuitumikia. Kila siku natamani Wadanganyika wote kama ninyi mungeweza kubadili utendaji wenu Hivi nani angewanyima mishahara minono?

    WATANZANIA WENGI NI WAVIVU MNO KAZI YAO KULINGANISHA MISHAHARA. KAMA MWAJIRI HATAKI KUKUSOMESHA, JINYIME WEKEZA KISHA JISOMESHENI.

    MBONA SIE WENZENU, TUMEJINYIMA NA KUJISOMESHA MWANZO MWISHO, NA SASA TUNATAKA KUELEKEA KWENYE PHD, HATUNA AJIRA, NI BIASHARA ZA KIMACHINGA NDIZO ZINAZOTUWEKA MJINI?

    FANYENI KAZI, ACHENI MAJUNGU!!!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 28, 2012

    We mdau hebu soma kwanza hiyo habari vizuri. Inasema amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa Tuhuma dhidi yake.. Hivyo haijalishi kaonewa au kafanya kweli hukumu haijatolewa ndio maana wamemsimamisha kazi ili kufanyia uchunguzi tuhuma, rudia tena "tuhuma".
    Kingine ndugu yangu watanzania sio wavivu asilani, ni wapambanaji na wapiganaji wa ukweli mfano wafanyakazi wanajitahidi kufanya kazi kwa bidii licha ya kupambana na ubovu wa miundombinu na ugumu wa usafiri unaowafanya wengi wao kulipa nauli kubwa ili kuwahi makazini,kero za riba kubwa ya mikopo wanazokutana nazo benki hli inayowafanya waishi nyumba duni na zilizo mbali na maeneo yao ya kazi, bei kubwa ya umeme,shida kubwa ya maji,huduma mbovu za afya,mazingira mabaya ya kazi sera mbaya za hifadhi za jamii, rushwa kwenye huduma mbalimbali, na mishahara midogo kwenye jamii yenye mfumuko mkubwa wa bei lakini unawaona bado wanafuraha na wanaamka alfajiri kuwahi makazini na jioni wengi wao hujisomea masomo ya ziada kwa gharama zao.
    Hayo mambo ya kujipima utendaji wa kazi kupiga soga si ya wafanyakazi bali ni mfumo kwa kiutawala kazini na si kosa la wafanyakazi bali utawala waulize menejimenti.
    Kingine ndugu yangu unapozungumzia mshahara mnono unamaanisha nini maana navyojua mimi kampuni binafsi nyingi hulipa kadiri ya perfomance ya kampuni na scale za nchi kwa kampuni zinazofanana kwenye nchi kihuduma,vinginevyo unono wa mshahara wako unatokana na "michongo" unayopiga kwenye idara yako. Hata hiyo base ya mafanikio ya kampuni ni kwa sababu ya mfumo na kufanya kazi kwa bidii kwa hao hao watanzania unaowasema wewe ni wavivu. Acha kutukana watanzania sababu tatizo sio wao kua wavivu kama unavyotuambia bali ni kukosa mfumo sahihi na watu sahihi wenye dhamana

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 28, 2012

    Napingana na mdau wa kwanza.

    Nakubaliana na mdau wa pili kwa kiasi fulani. Mdau wa pili umesema watanzania si wavivu ila ni mifumo mibovu. Kwa hili nakubaliana na wewe kwa asilimia 60 lakini sikubaliani na wewe kwa sililimia 40 kwa sababu wavivu wapo wengi tu kutoka kwa raia wa kawaida hadi serikalini. Mifumo mibovu imetokana na uvivu wa kufikiri na kutenda kwa baadhi ya watanzania. Kwa upande wa viongozi, wapo wanafanya kazi kwa mazoea huku wakijitahidi kulinda vyeo vyao na maslahi yao kwa gharama yoyote. Hawana ubunifu (creativity) wa aina yoyote. Ndio maana inapotokea mifumo iliyowekwa haina faida kwa taifa, wao hukimbilia kupambana na wanaopinga mifumo hiyo badala ya kurekebisha ili iwe na tija kwa wananchi. Kwa maana nyingine hawakubali kukosolewa ama wao wenyewe ama mifumo wanayofanyia kazi.

    Kwa upande wa wananchi, wapo wachapakazi na wapo wavivu pia. Kitendo cha kuona mifumo ni mibovu lakini hakuna hatua yoyte mnayochukua ni aina nyingine ya uvivu wa kufikiri na kutenda. Jiulize wewe kama mwananchi wa kawaida ni mchango gani umetoa katika kuhakikisha nchi inakuwa na mifumo mizuri? Je umetimiza wajibu wako hata pale ambapo mifumo ni mizuri? Je kila kitu tuwaachie viongozi? Na kama tutashindwa kutimiza wajibu wetu, tusilalamike tuwaache viongozi wafanye wanavyotaka.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 28, 2012

    Nyie wote mlioandika maoni ni
    utumbo mtupu kama chupi chafuuu.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 30, 2012

    uchunguzi utakapokamilika itajulikana, kwani tuhuma zake ni nyingi na sidhani kama ndizo zilizoandikwa humu. Jamaa hakuna alichokifanya si kwa nasafi aliyopewa baada ya Dr KaYOMBO kufariki, hata kituo chake cha kazi hakuna alichokifanya zaidi ya kubagua wafanyakazi na kunyanyasa juhudi za wale wanaotaka kuliendeleza shirika. Jiulize ni kiongozi gani mwenye uchungu na raslimali za shirika anayeruhusu baa kujengwa hadi kwenye ofisi kisa ana kamisheni na mwenye baa!! Mabango kuziba kabisa kijiji bila aibu, ni kiongozi anayefaa huyo. acheni uchunguzi ufanyike ndio mtaona kama kweli anafaa kuwepo. hayo ni machache tu yapo mengi saaaaana

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 30, 2012

    Mmmmh yapo wapi majigambo yake "mimi nimeshaonwa, nini kuwa na PhD bwana"! Sasa mwisho wa ubaya na visirani ndo huo, jifunze kufanya kazi na waliokuzidi bila kuwanyanyasa, kwanza jiulize Cheti cha kukaa kiti kile unacho? je, mshahara unaopokea ni halali kwako? je, wanaostahili mishahara kwa kisomo na uzoefu walionao ulimudu kuwatetea au uliwakandamiza na kuwanyima fursa wenye nia ya kujiendeleza! Loh tusubiri uchunguzi baba haki itajulikana tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...