Eid Mubarak wadau wote.
Kwanza kabisa niombe radhi kwa kuchelewesha mada yetu ya Jumapili ya leo  kutokana na  mnuso kibao niliyoalikwa kwa mpigo katika kusherehekea sikukuu Tukufu ya Iddi. Maana, mara tu baada ya swala ilikuwa kupata staftahi kwa jirani, mpunga saa saba ilikuwa kwa Ba’Mdogo na kwa baadaye tena kwa wakwe.
Kustukia jua limeshazama na ile kurudi nyumbani tu nikajitupa kwenye telemka-tukaze na kuupiga usingizi wa pono. Unajua tena mpunga wa dezo unavyolewesha… Natumai mmenisamehe kwa hilo.
Naam, upigaji wa picha za harusi nashukuru kusema kwamba ni moja ya Nyanja ambazo nimeifanya kwa muda mrefu kiasi, hasa ikiwa kama utachukulia kwamba miaka 20 na ushee hivi si muda mfupi. Ila Kwa kuwa mada hii ni ndefu na pana, naomba ruksa niitawanye katika sehemu kadhaa, nikianza na hii ya kwanza ambayo ni  kutaja aina tatu za wapigaji picha kwenye harusi, na baada ya hapo nianze kuchambua moja baada ya nyingine.
Kwa upande wangu, aina ya wapiga picha wa kwanza ni wale waliokodishwa mahususi kufanya kazi hiyo, na baadaye kutoa albamu kwa maharusi. Kundi la pili ni la wapiga picha ambao hawajakodishwa ila huja na kamera zao na kupiga picha bega kwa began a hao wa kulipwa. Baadaye hutoa albamu ama picha kadhaa kwa maharusi kama zawadi.
Kundi la tatu ni la wapiga picha za binafsi, yaani wale wanaokuja aidha na kamera kubwa ama ndogo, amao simu zao za mikononi ama hata ipad na ma-tablet ya Galaxy Samsung, na kupiga picha za maharusi na hata zao wenyewe kwa kumbukumbu ama kwa kuwatumia jamaa na marafiki kwa njia mbalimbali mtandano kupitia email ama Facebook wakiwa hapo hapo shereheni.
Kwa leo nitazungumzia hili kundi la mwisho, yaani la wapiga picha za binafsi ambao kwa kadri siku zinavyokwenda, teknolojia nayo inaendelea kwa kasi kiasi kwamba wadau hawea nao wanaongezeka idadi yao sio maharusini tu, bali hata kwenye hafla zingine.
Kwa ujumla, si vibaya kuja na kamera yako ya mfukoni, ama kutumia iPhone ama iPad ama Tablet yako kunasa kumbukumbu ya ndugu, jamaa ama rafiki anayeolewa ama anayeoa. Ni jambo jema tu, ila mara nyingi lina mushkeli wake, hasa ikizingatiwa kuwa kundi hili siku hizi linakuwa kubwa kiasi hata linakuwa kero kwa wapiga picha wa kulipwa.
Na sio linakuwa kero tu, bali pia huhatarisha mustakabali mzima wa maharusi kupata picha nzuri na za uhakika, kutokana na kupigana vipepsi na wapiga picha za kulipwa, hasa hasa wakati wa matukio muhimu kama ya kulishana viapo, kuvalishana pete, kusaini hati za ndoa, kukata keki, kugongesheana champeni na hata wakati wa picha za pamoja za familia.
Hawa wapiga picha za binafsi mara nyingi huwa vigingingi visivyo vya lazima sana kwa wapiga picha za kulipwa, kwani hupenda kusimama mahali muafaka na katika wakati muafaka na kuwazibia nafasi wenye kazi zao. Pia aghalab waalikwa huwa wanaambulia kuona migongo na vichogo vyao badala ya maharusi na  tukio husika inavyotakikana.
Halafu tena wadau sampuli hii wengine ni wakali mno kiasi ya kwamba wewe unayelipwa kufanya kazi hiyo ukihoji ama ukiomba usibughudhiwe huwa unabezwa na hata kutolewa kauli zisizofaa, sababu ikiwa yeye ni ndugu wa damu na maharusi, hivyo angalia ustaarabu wako!
Sisemi kwamba wapiga picha za binafsi wasipewe nafasi katika minuso, la hasha. Wawepo ila kwa mpangilio na nidhamu mbele ya mpiga picha wa kulipwa ambaye amepewa dhamana ya kunasa kumbukumbu hiyo baada ya kulipwa pesa kibao.
Si vyema kabisa kumziba mpiga picha maalumu, ama hata kupigana naye vipepsi (kama inavyotokeaga mara nyingi), katika kugombea picha za tukio. Mwisho wa siku utakuta umemtia hasara bwana na bibi harusi kwa kung’ang’ania kupata picha kwa ajili ya Facebook.
Rai yangu kwa upande wa wapiga picha wa kulipwa ni kwamba jaribu kuwa mkarimu na mwenye tabasamu pale inapotokea hao wadau wanaingia anga zako. Haitokusaidia wewe, wao ama maharusi endapo kama nawe utaamua kutunisha msuli ili kupata picha uzitakazo na kuishia kuchafua hali ya hewa kwenye harusi ya wenzenu.

Nadhani nimesomeka, naomba kuwasilisha
Iddi Njema wadau wote
-Ankal



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Tumekusoma ANKAL, hamna noma wala ngendembwe we shusha tu mistali sio twaingojea.IDD NJEMA

    ReplyDelete
  2. Asante sana Ankal, ila vile vile tunaomba kipindi cha masuali na majibu.

    Tuna vimeo vyetu vinatupa shida sana tungependa kupata ufafanuzi, jee itawezekana?

    Natanguliza shukurani zangu.

    ReplyDelete
  3. dah! umenigusa kweli Ankal maana yalinitokea hayo wiki iliyopita tu yaani hivyo hivyo watoto wa mwenye sherehe kila mtu na tablet yake vibeka hovyo hovyo niliboreka sana mpaka nikawaambia walionikodisha kuwa hawa sasa inakuwa kero...!!1

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...