Jengo linalokusudiwa kununuliwa na An Noor Community Leicester
 Waislamu kutoka miji mbali mbali waliitikia mwito na kuhudhuria Mhadhara wa aina yake mjini Leicester
 Kwa makini kabisa waliketi na kusikiliza mawaidha yaliyojaa hekima na maarifa

Vijana wadogo nao hawakuwa nyuma, kwa hakika kumbi zote mbili-wa kinamama na wa kinababa-zilifurika hasa na kuleta hisia za umoja na mshikamano. Mashallah! 


Waislamu wamekumbushwa wajibu wao katika kushikamana na Dua na mafunzo mengine yanayotiliwa mkazo katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Katika mhadhara mkubwa ulioandaliwa na An Noor Community Leicester pamoja na Madrassatul Noor Leicester na kuhudhuriwa na waislamu kutoka katika miji ya Leicester, Slough, Coventry, East Ham, Milton Keynes na kwingineko, kilichodhihirika ni ishara ya mshikamano, mapenzi na bashasha miongoni mwa waliohudhuria.
Pamoja na kuwa lengo mahsusi la Mhadhara huo uliofanyika Jumamosi 4 Agosti katika ukumbi wa Hashi, Nedham Street lilikuwa ni kuchangia ununuzi wa jengo la shughuli za Kiislamu mjini Leicester, wahadhiri pamoja na kuhimiza na kukumbusha umuhimu wa kuuunga mkono mradi huo wa kheri, pia walitumia fursa hiyo kusisitiza maadili na mafunzo ya mwezi mtukufu.
Sheikh Kamil kutoka De Montfort University yeye alihimiza umuhimu wa waislamu kumwelekea Allah kwa dua na maghfira, kwani hiyo ni moja ya njia muhimu sana ya kutengenekewa katika maisha yao.
Sheikh Muhammad kutoka East London akasisitiza umuhimu wa wanajamii kuchunga ndimi zao, kwani kwa mujibu wa Mtume SAW matendo mema humezwa na kuyeyushwa na matumizi mabaya ya ndimi za watu pale wanaposengenya, kuzua uongo, kufitini na kusema maneno yoyote yaliyokatazwa katika sheria ya Kiislamu.
Sheikh Nassor wa East Ham yeye alikumbusha kuwa mwezi wa Ramadhan umekuja kuleta mabadiliko katika tabia za Waislamu. Akaendelea kwa kukumbusha kuwa kwa mja kukubaliwa toba yake, kuna nukta za kuzingatia, ambazo ni pamoja na mtu kuzikimbia dhambi na marafiki wabaya na kushikamana na watu wema na mambo mazuri.
Kisha Ustadh Umar Mrisho kutoka Slough alitumia fursa yake kukumbusha umuhimu wa Waislamu kulipa umuhimu suala la kutoa michango yao katika masuala ya kheri, na kwamba ili kujiweka karibu na Allah basi ni lazima wawe tayari kujitolea katika wanavyovipenda.
Mhadhara ulihitimishwa na Ustadh Khamis alipotumia fursa yake kutoa taarifa juu ya mradi wa ununuzi wa jengo la Jamati la Wahindu ambalo Inshaallah litafanywa kuwa msikiti, madrasa, duka la vitabu na maktaba ya Kiislamu. Jengo hilo lipo katikati ya mji wa Leicester na kama litanunuliwa, litaingia katika historia kwa kuwa msikiti wa kwanza katikati ya mji wa Leicester Inshaallah!
Baada ya hapo ikafuatia shughuli ya kukusanya michango, kisha Sala ya Magharibi na hatimaye futari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...