WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kukamilika kwa mradi wa kinu cha kukoboa mpunga katika kata ya Mwamapuli kutawasaidia wakulima waache kuuza mpunga na badala yake wauze mchele tu.

Amesema kulingana na mahitaji yatakayokuwepo, wakulima hao kama watajipanga vizuri wanaweza kuuza mchele watakaouzalisha hadi katika nchi za Burundi na Rwanda ambako soko la uhakika lipo.

Amesema hayo jana jioni (Jumapili, Agosti 26, 2012) wakati akikagua kazi ya kuweka mitambo ya kinu cha kukoboa mpunga katika kata ya Mwamapuli na ujenzi wa madaraja ya mto Msadya na mto Kavuo katika kata za Mwamapuli na Majimoto wilayani Mlele, mkoani Katavi. Hata hivyo, ujenzi wa daraja la mto Kavuo bado haujaanza.

Waziri Mkuu ambaye ni Mbunge wa jimbo la Katavi yuko kijini kwake Kibaoni kwa mapumziko mafupi. Alikwenda Mwamapuli kukagua kinu hicho ambacho kimenunuliwa kwa fedha za Halmashauri ili kiwasaidie wananchi wa kata hiyo kuongeza thamani ya zao la mpunga linalozalishwa kwa wingi katika eneo hilo.

Diwani wa kata ya Mwamapuli, Bw. Emmanuel Mpondamali alimweleza Waziri Mkuu kwamba kinu hicho kina uwezo wa kukoboa tani 300 kwa siku kikiendeshwa kwa saa nane kutwa nzima.

Hata hivyo, alimuomba Waziri Mkuu kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya waangalie uwezekano wa kufunga mashine ndogo ya kukoboa mpunga ambayo itawahudumia wakazi wa kata hizo wanaokuja na kiasi kidogo cha mpunga kwa vile kinu hicho kina uwezo wa kukoboa magunia sita kwa mkupuo na siyo chini ya hapo.

“Mchele ukishakobolewa, unapangwa katika madaraja A, B, C, na daraja D zinakuwa ni chenga ambazo zitauzwa peke yake kwa ajili ya wauza vitumbua. Kinu hiki pia kina uwezo wa kutenganisha pumba kwa ajili ya mifugo na kuzipaki katika sehemu ya peke yake bila kuingiliana na uzalishaji wa mchele,” alisema.

Kinu hicho cha kukoboa mpunga, kuchambua mchele, kuupanga katika madaraja manne tofauti na kufungasha kwa madaraja hayo, kinatarajiwa kuanza kazi Septemba mwanzoni mara kazi ya kuuunganisha jenereta itakapokamilika.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Vijijini, Bw. Wilbroad Mayala alisema kinu hicho kimegharimu sh. milioni 96/- wakati jenereta la kuendesha kinu hicho lenye uwezo wa kuzalisha kilowati 120, limenunuliwa kwa gharama ya sh. milioni 86/-.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa daraja la mto Msadya katika kata ya Mwamapuli litakalokuwa na urefu wa mita 28. Kukamilika kwa daraja hilo, kutasaidia wakazi zaidi ya 200,000 wanaoishi kwenye vijiji vya Chamalendi, Mkwajuni na Ukingwamizi kusafirisha kwa urahisi zaidi ya tani 500 za mpunga zinazozalishwa katika bonde hilo kwa mwaka.

Kabla ya ujenzi huo kuanza, wananchi walikuwa wakivuka kwa kutumia daraja la miti kwa malipo ya sh. 500/- kwa mtu mmoja.

Mkandarasi anayesimamia ujenzi huo, Bw. Luis Mamba wa kampuni ya Mamba Contractors alisema ujenzi wa daraja hilo utagharimu sh. milioni 232/- na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba, 2012.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...