Na
Anna Nkinda – Maelezo, New York
Mshikamano wa pamoja unahitajika
baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa mtoto wa kike
ambaye hajapata nafasi ya kwenda shule anapata elimu, kuwainua wanawake
kiuchumi na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto vinavyotokana na
tatizo la uzazi na ugonjwa wa kansa.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa rais Mama Salma Kikwete wakati
akichangia mada kwenye mkutano wa The
RAND African First Ladies Initiative uliofanyika makao Makuu ya Taasisi ya Ford
mjini New York nchini Marekani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa taasisi mbalimbali za
Kiserikali na zisizo za kiserikali zinafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha kuwa
zinawasaidia wanawake wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha tatizo lililopo ni upungufu wa rasilimai fedha za
kuweza kukabiliana na changamoto hizo hivyo basi ushirikiano wa pamoja unahitajika
ili kuweza kufanikisha malengo hayo.
Aliendelea
kusema kuwa watoto wa kike wakipata elimu ya kutosha watakuwa na silaha muhimu
katika maisha yao ya kuweza kupambana na
matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
maradhi, ujinga na umaskini kwani elimu
ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote Duniani bila ya watu kuwa na na elimu nchi haiwezi kuendelea.
“Ukimuelimisha
mtoto hasa mtoto wa kike ambaye amekosa
nafasi ya kupata elimu ni faida kwa mtoto, Taifa na Dunia kwa ujumla kwani hivi sasa
tumejionea wanawake wengi wakishika nafasi za juu za uongozi kitaifa na Dunia
pia wameweza kujikwamua kiuchumi tofauti
na miaka ya nyuma”, alisema Mama Kikwete.

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na
wake wa marais na wakuu wa Serikali wa Afrika, mke wa rais mstaafu wa Marekani Laura Bush
na mke wa waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Cherie
Blair, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na mashirika binafsi kutoka
nchi wa Afrika na Marekani.
Katika mkutano huo mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja
na kuangalia jinsi gani wake wa maraisi na wakuu wa
Serikali wanaweza kuleta mabadiliko katika nchi zao katika kuimarisha afya ya mwanamke, kuhakikisha kuwa mtoto wa
kike anapata elimu na na kuwainua wanawake kiuchumi pamoja na changamoto
wanazoweza kukabiliana nazo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...