Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitumia
salamu za rambirambi familia ya Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni la Rajani
Group of Companies, Mzee Jayantilal Pragji Rajani kufuatia kifo cha mzee huyo
kilichotokea jana, Jumatano, Novemba 21, 2012, mjini London, Uingereza.
Katika
salamu zake kwa familia hiyo, Rais Kikwete ameeleza masikitiko na huzuni yake
kufuatia taarifa za kifo cha Mzee Rajani akimwelezea Mzee huyo kama mmoja wa
watu waliochangia sana maendeleo ya nchi yetu kupitia shughuli za biashara,
viwanda na mashirika ya kujitolea.
“Nilipata
kumjua Mzee Jayantilal Pragji Rajani wakati wa maisha yake. Alikuwa
mfanyabiashara mwenye bidii na aliyejituma sana katika maisha. Ni mmoja wa
Watanzania wenzetu ambaye amechangia sana maendeleo ya nchi yetu kupitia
shughuli za biashara, viwanda na Shirika la Kujitolea la Rotary. Tutamkumbuka
kwa mchango wake huo katika maendeleo ya nchi yetu,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nawatumieni
salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa ambao taarifa zake
nimezipokea kwa masikitiko na huzuni. Naelewa machungu mlinayo kwa kuondokewa
na mhimili na mkuu wa familia yenu kwa miaka mingi. Naungana nanyi katika
maombolezo. Aidha, namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu katika
kipindi hiki na naungana nanyi katika kumwomba aiweke pema peponi roho ya
Marehemu Rajani. Amina.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22
Novemba, 2012


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...