Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Novemba Mosi, 2012, amezindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania unaojulikana kama Mradi wa Uboreshaji Miji ya Tanzania (Tanzania Strategic Cities project – TSCP) utakaogharimu mabilioni ya fedha. 

Aidha, Rais Kikwete amezidua rasmi Jiji la Arusha katika sherehe ya kufana iliyofanyika kwenye Mnara wa Azimio la Arusha katikati ya jiji hilo. Mradi wa TSCP unalenga kuboresha huduma za msingi katika miji saba na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kujenga upya, kukarabati na kupanua miundombinu pamoja na kuijengea uwezo wa kukusanya na kusimamia mapato ya miji husika. 

Mradi huo ni mmoja ya miradi mitatu inayogharimiwa na Benki ya Dunia kwa nia ya kuboresha miji ya Tanzania. Mbali na TSCP, miradi mingine ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project - DMDP) na Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP). Mpaka sasa Benki hiyo imekwishakutoa sh bilioni 8.76 kati ya sh bilioni 34.7 za TSCP. 

Chini ya TSCP ambao unagharimu kiasi cha sh bilioni 191.3 miji itakayonufaika ni Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya, Mtwara na CDA ambayo ndiyo itakayopata pesa kubwa zaidi kuliko mjini mingine. Aidha, chini ya TSCP, miji hiyo itajengewa miundombinu ya barabara zenye jumla ya kilomita 141.2, ujenzi wa madampo matano, ununuzi wa vifaa vya kusimamia taka ngumu, vituo vya mabasi sita, vituo viwili vya kuegesha malori na kilomita 15.9 za mitaro ya maji ya mvua. Katika mji wa Arusha, kiasi cha barabara za lami zenye urefu wa kilomita 7.23 zitajengwa, mtaro mkubwa wa maji ya mvua wa mita 800 utajengwa, zitafungwa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara tatu ambazo ni Sokoine na Viwandani, Sokoine na Esso na Kanali Middleton na Makongoro. Katika awamu ya pili, kiasi cha barabara zenye urefu wa kilomita 7.8 zitajengwa katika Jiji la Arusha. 

Miji itakayonufaika na ULGSP ambako Benki ya Dunia inatoa mkopo wa dola za Marekani milioni 255 na unatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha ni Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba, Lindi, Njombe, babati, Kibaha, Mpanda, Geita, Korogwe na Bariadi. DMDP kwa ajili ya Jiji la Dar Es Salaam, itahusika wilaya zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 75. 

Baada ya kuzindua mradi huo wa TSCP, Rais Kikwete amezindua Jiji la Arusha ambalo linapanda hadhi kutoka Manispaa. Katika uzinduzi huo, Rais amezindua nembo ya Jiji pamoja na kukabidhi cheti cha kulipandisha hadhi Jiji hilo. Rais Kikwete amezindua miradi hiyo ikiwa ni shughuli zake katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha. Rais amewasili Arusha mchana wa leo kutoka Dodoma.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. John Mongella kuzindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha
Rais Kikwete akizindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha
bango la mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania
Rais Kikwete akisalimiana na Mbunge wa  Arumeru Mashariki Mhe. Joshua Nassari katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha
Wakaazi wa Arusha wakimshangilia Rais Kikwete  alipowasili katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania 





Waziri wa Ujenzi  Dkt. John Pombe Magufuli akitoa neno katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Vijijini vipi, maana serikali inaonekana kujikita zaidi kutatua matatizo na kero za watanzania wa mijini.

    Si bure sote tutahamia mijini kufuata mataa na lami huku kukiwa hakuna ajira mijini.

    Pamoja na pongezi kuonesha serikali inaweza kukamilisha miradi mijini basi na serikali itafute njia ya kujenga mifumo ya umwagiliaji mashamba (Canals),umeme, afya , elimu na masoko kwa mazao ili tujiajiri mashambani.

    Mdau
    Kijijini Malampaka

    ReplyDelete
  2. Anonymous wa kwanza hapo juu post yako inaonesha unachofata mjini sio hizo huduma ulizozitaja bali unafata Lami na Mataa.. So hata kama huduma zote za afya nk zitawekwa vijijini wewe bado utakuja mujini kufuata mataa na Lami, au sio?

    ReplyDelete
  3. Mkuu huu mradi haufadhiliwi na Benki ya Dunia peke yake bali pia serikali ya Denmark kupitia ubalozi wao hapa nchini nadhani jamaa hawajaitendea haki Serikali ya Denmark

    ReplyDelete
  4. Hongera mwaya JK

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...